Tusipotoshe maana ya maneno

20Sep 2016
Barnabas Maro
Tujifunze Kiswahili
Tusipotoshe maana ya maneno

KISWAHILI kina maneno yanayotatanisha wengi kwa jinsi yanavyokaribiana au kufanana. Mara nyingi maneno hayo huwatatiza waandishi na wazungumzaji kadhalika.

Mfano ni ‘shaka’ na ‘mashaka.’ Maneno haya yana maana tofauti ingawa wengine hudhani ‘shaka’ ni umoja na ‘mashaka’ ni wingi. Soma sentensi ifuatayo katika moja ya magazeti maarufu nchini.

“Meneja wa kiwanda cha Simba Biscuit kilichopo jijini Mwanza, Suresh Naranjian Somaiya (72) mwenye asili ya Asia, amekutwa chooni akiwa amefariki dunia katika mazingira yaliyoacha mashaka.”

Awali ya yote, sentensi hiyo imetumia maneno mengi yasiyo muhimu. Majina la Suresh Naranjian Somaiya yatosha kujua kuwa ni ya Kiasia. Kwa hiyo hakukuwa na sababu ya kuandika ‘mwenye asili ya Asia’ baada ya majina yake kuandikwa.

Pili ni maelezo kuwa “amefariki dunia katika mazingira yaliyoacha mashaka.” Neno hili la mwisho huwachanganya wengi kwa dhana kwamba ni wingi wa ‘shaka’ kumbe sivyo.

‘Shaka’ ni hali ya mtu kuwa na wasiwasi juu ya jambo; =mushkili; udhanifu (Kamusi la Kiswahili Fasaha –BAKIZA).
Kwa mujibu wa Kamusi ya Karne ya 21, ‘shaka’(nomino) lina maana mbili: 1. Hali ya kujawa na wasiwasi na kukosa uhakika wa jambo; hatihati, wahaka (nah) tia shaka (a) bila shaka (b) pasi na wasiwasi wowote.

2. ‘Shaka’ (kitenzi elekezi) ni fukuza, shunga, winga, furusha. Shakia, shakiana, shakika, shakisha, shakwa.
Neno ‘mashaka’ laelezwa na Kamusi ya Karne ya 21 kuwa ni shida zinazompata mtu katika maisha; tabu. Nalo Kamusi la Kiswahili Fasaha laeleza maana ya ‘shaka’ kuwa ni matatizo au masahibu yanayompata mtu katika maisha.
Kwa hiyo sentensi iliyotumia neno ‘mashaka’ haikuwa sahihi bali ingeandikwa:

“Meneja wa Kiwanda cha Simba Biscuit jijini Mwanza, Suresh Naranjian Somaiya (72), amefia chooni katika mazingira yanayotia shaka.” ‘Mazingira yanayotia shaka’ maana yake ni wasiwasi kuhusu kifo hicho. Je, kajiua au kauawa?

“Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Julai 9 saa 4.00 usiku nyumbani kwake Mtaa wa Barabara ya Nyerere, wilayani Nyamagana.”
Maneno yanayonipa wasiwasi katika sentensi hii ni ‘tukio,’ ‘mtaa’ na ‘barabara.’ Neno ‘tukio’ kwa mujibu wa Kamusi ya Karne ya 21 ni jambo lililotendeka au lililotokea; tokeo.

Kamusi la Kiswahili Fasaha laeleza maana ya ‘tukio’ kuwa ni kadhia yaani jambo linalojiri; jambo la kuhuzunisha.
Je, ‘tukio’ ni tendo lililosababisha kifo cha Somaiya au kugundulika akiwa kafia chooni? Je, mwandishi ametumia neno ‘tukio’ kwa maana sahihi?

‘Mtaa’ ni i) eneo kubwa kuliko kitongoji ambalo limejitenga na mji na ii) ni barabara ya mji pamoja na eneo linalopakana nayo kwa mujibu wa Kamusi ya Karne ya 21. Imetoa mfano kuwa ‘Mtaa wa Msimbazi huanzia barabara ya Morogoro.’

Kamusi hiyo yaeleza maana ya ‘barabara’ kuwa na maana tatu: i) njia kuu iliyotengenezwa kwa madhumuni ya kupitia magari na vyombo vingine vya usafiri wa nchi kavu. ii) ndege mkubwa wa jamii ya hondohondo na iii) ni sawasawa, kama ilivyotarajiwa.

Nalo Kamusi la Kiswahili Fasaha laeleza maana ya ‘mtaa’ kuwa ni sehemu ya mji au kijiji. Kuhusu ‘barabara’ yaelezwa ni i) njia kuu iliyotengenezwa kwa lami; =baraste na ii) ni mtaa katika mji au jiji. Pia ni tamko lenye maana ya kuafikiana na jambo; ndivyo!, sawasawa!, hasa!, Barab-bara =enhe!

Kwa ufupi ni kosa kusema mtaa wa barabara ya Nyerere. Ama unasema ‘mtaa wa Nyerere’ au ‘barabara ya Nyerere.’
Methali: Zito hufuatwa na jepesi.