Tshabalala haendi Yanga SC - Barbara

21Apr 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
The Guardian
Tshabalala haendi Yanga SC - Barbara

Ofisa Mtendaji Mkuu wa 'Wekundu wa Msimbazi' hao, Barbara Gonzalez, amewatoa wasiwasi wanachama na mashabiki wa klabu hiyo, akidai kuwa haendi popote na bado ni mchezaji wao halali.

Tangu majuzi zilianza kuzuka tetesi za mchezaji huyo ambaye anaitumikia Simba kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na kuchaguliwa kwenye kikosi bora cha wiki katika michuano hiyo, lakini hata baadhi ya vyombo vya habari yakiwamo baadahi ya magazeti [si Nipashe] yakiandika kuwapo kwa mpango huo.

Lakini Barbara amesema kuwa Tshabalala ataendelea kuwa mchezaji wa Simba.

"Haendi Yanga, ni mchezaji wetu. Ni mchezaji halali wa Simba na Mungu akipenda ataendelea kuwa Simba," alisema Barbara kwa kifupi na msisitizo.

Habari zinaeleza kuwa mchezaji huyo anamaliza mkataba wake kwenye klabu ya Simba mara baada ya msimu huu kumalizika, hivyo klabu ya Yanga inatumia mwanya huo kumshawishi kujiunga na klabu hiyo.

Hata hivyo, tayari klabu ya Simba imedaiwa kumuwekea ofa nono ya kuongeza mkataba wake kwa ajili ya kuendelea kuitumikia klabu hiyo.

Ukiachana na Tshabalala ambaye inaonekana ni ngumu kwa Yanga kumng'oa Simba, lakini habari kutoka ndani ya klabu ya Yanga zinaeleza kuwa inawahitaji pia wachezaji wake wa zamani ambao kwa sasa wako Msimbazi, Gadiel Michael na Ibrahim Ajibu.

Mabingwa wao wa kihistoria inadaiwa kutaka kuwarejesha kundini wachezaji hao ambao wanaonekana hawana nafasi ndani ya Simba kwa ajili ya kukiimarisha kikosi hicho msimu ujao kutokana na kwamba huenda ikashiriki michuano mingi, ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho.

Ajibu na Gadiel ni moja ya wachezaji ambao wanamaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu na huenda Simba ikaachana nao.

Top Stories