Yanga hii kufuru

24Jan 2016
Lete Raha
Yanga hii kufuru

VINARA Yanga wamefanya kufuru kuelekea mwisho wa duru la kwanza la Ligi Kuu ya Tanzania Bara, baada ya kushinda mechi zote 7 za mwisho -- tena bila kuruhusu bao hata moja.

Yanga players cerebrating a goal

Katika mechi hizo ambazo wamekusanya jumla ya pointi 21, Yanga wamefunga jumla ya mabao 16 bila ya wavu wao kuguswa.
Mara ya mwisho Yanga kuruhusu goli ilikuwa ni katika sare ya 2-2 dhidi ya Mwadui mjini Shinyanga Oktoba 28.
Yanga ambao wamemaliza duru la kwanza la ligi hiyo kwa kucheza mechi 15 bila ya kupoteza mchezo sawa na Azam inayoshika nafasi ya pili katika msimamo, ndiyo pia wanaoshikilia rekodi ya kumaliza mzunguko wakiwa wamefunga magoli mengi zaidi (36) na wamefungwa machache zaidi (5).
Mahasimu wao Simba, ambao wanashika nafasi ya tatu kwa pointi zao 33, sita nyuma ya vinara Yanga, katika mechi saba zilizopita wamekusanya pointi 17 baada ya kushinda mechi 5 na sare mbili.
Katika mechi hizo Simba wamefunga jumla ya magoli 15 wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara 5.
Simba imepoteza mechi mbili kufikia mwisho wa duru hilo la kwanza wakilala 1-0 dhidi ya Prisons mjini Mbeya Oktoba 21 na kichapo cha 2-0 kutoka kwa mahasimu wao Yanga Septemba 26.
Azam wanaoshika nafasi ya pili, katika mechi 7 zilizopita imekusanya pointi 19 baada ya kushinda mechi 6 na sare moja.
Katika mechi hizo, Azam imefunga jumla ya magoli 17 ikiruhusu wavu wake utingishwe mara 5.
Rekodi za Yanga katika mechi 7 zilizopita:
Ilishinda 5-0 dhidi ya Majimaji Januari 21; ikailaza Ndanda FC 1-0 Januari 17; ikaicharaza Mbeya City 3-0 jijini Dar es Salaam Desemba 26; ikaichapa 4-0 Stand United Desemba 19; ikaifunga African Sports 1-0 Mkwakwani Tanga Desemba 16; ikatoka 0-0 dhidi ya Mgambo JKT mjini Tanga Desemba 12; ikaifunga Kagera Sugar 2-0 Oktoba 31.
Rekodi za Simba katika mechi 7 zilizopita: Ilishinda 2-0 dhidi ya JKT Ruvu Januari 20; ikaiangusha Mtibwa Sugar 1-0 Januari 16; ikaifunga Ndanda FC 1-0 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Siku ya Mwaka Mpya; ikashikiliwa kwa 1-1 dhidi ya Mwadui mjini Shinyanga Desemba 26; ikatoka 1-1 dhidi ya Toto African jijini Tanga Desemba 19; ikashikiliwa kwa sare ya 2-2 dhidi ya Azam Desemba 12; ikaisambaratisha Majimaji kwa magoli 6-1 Oktoba 31; ilishinda 1-0 dhidi ya Coastal Union Oktoba 28.
Rekodi za Azam katika mechi saba zilizopita:
Ilishinda 2-1 dhidi ya Mgambo Januari 20; ililazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya African Sports kwenye Uwanja wa Azam Complex Januari 16; ikaifunga Mtibwa 1-0 Desemba 30; ikaichapa Kagera Sugar 2-0 Desemba 27; ikaifunga Majimaji 2-1 mjini Songea Desemba 20, iliichakaza Toto African 5-0 Novemba 1; ikaifunga JKT Ruvu 4-2 Oktoba 29.

Top Stories