DC Kibaha kuanzisha kliniki ya kuibua vipaji vya wasanii

By Julieth Mkireri , Nipashe Jumapili
Published at 12:28 PM Aug 11 2024
MKUU wa Wilaya ya Kibaha Nickson John.
Picha: Julieth Mkireri
MKUU wa Wilaya ya Kibaha Nickson John.

MKUU wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John amesema hivi karibuni kliniki ya kuibua vipaji vya wasanii itaanza katika wilaya hiyo.

Nickson ameyaeleza hayo alipokuwa akizungumza kwenye semina ya wasanii iliyofanyika Mjini Kibaha ambapo amesema kliniki hiyo itahusisha wasanii wakongwe.

Pia mkuu huyo wa wilaya amesema ataanzisha utaratibu wa kuzunguka na wasanii wa wilaya hiyo pindi atakapoenda kufanya mahojiano kwenye vyombo vya habari zikiwemo televisheni na redio lengo likiwa ni kuwatangaza.

Amewakumbusha wasanii kutumia sanaa kama biashara huku aliwasisitiza kuwa na nidhamu kufikia malengo .

Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Sylvestry Koka ameahidi kushirikiana na Mkuu wa Wilaya katika kliniki hiyo na kuwainua wasanii wa Wilaya hiyo.

1
Koka amesema anaungana na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwatambua wasanii huku akiwasisitiza kila mmoja kubuni mbinu za kuinua kipaji chake na kubadilisha kuwa fedha.

Mbunge huyo amewataka wasanii wa mji wa Kibaha kujituma Ili waweze kusaidiwa kwa urahisi kufikia malengo yao.

Mwenyekiti wa Chama cha Wasanii Kibaha Jumanne Kambi amesema kufanyika kwa semina hiyo kumetokana na baadhi ya wasanii kufanya kazi nyingi lakini haziendi mbali.

Kambi amesema katika semina hiyo vyama mbalimbali likiweno Shirikisho la wasanii na bodi walioshiriki semina hiyo ya kuwajenga wasanii wa Kibaha Ili waweze kutumia sanaa yao kama biashara.
2

Afisa Habari na Mawasiliano wa Chama hicho Ally Kinyunyu amesema sambamba na semina hiyo wanaendelea na utaratibu wa kuwatambua wasanii wa Wilaya hiyo.

Kinyunyu amesema kwasasa idadi ya wasanii wa Wilaya hiyo imefikia 400 na kwamba wanaendelea kuwahamasisha kujiunga na vyama vya wasanii Ili waweze kunufaika na fursa zinazojitokeza.
3