‘Amri Nane’ kunusuru Watanzania magonjwa sugu

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 09:12 AM Sep 15 2024
Mwenyekiti wa Chama cha Wagonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA) na Mwenyekiti Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), Prof. Andrew Swai.
Picha:Mtandao
Mwenyekiti wa Chama cha Wagonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA) na Mwenyekiti Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), Prof. Andrew Swai.

KASI magonjwa yasiyoambukiza imewashtua wadau na sasa katika kunusuru taifa kuangamia wamekuja na mambo manane waliyoyabatiza kama ‘amri nane’ kusaidia watanzania kuwa na mtindo bora wa maisha.

Mwenyekiti wa Chama cha Wagonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA) na Mwenyekiti Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), Prof. Andrew Swai, aliyataja mambo hayo juzi mkoani Dar es Salaam katika mafunzo waliyoandaa kwa waandishi wa habari kuhusu magonjwa hayo.

Prof. Swai alitaja la kwanza kuwa ni watu wanapaswa kuzingatia kila mlo wanaokula lazima uwe na aina zote za vyakula.

“Tunakula kujenga na kupata joto/nguvu na kinga ya mwili. Aina tano za vyakula ni nafaka, mizizi, ndizi mbichi za kupika, matunda, mbogamboga, jamii ya mikunde na asili ya wanyama na mafuta,” alisema.

Mtaalam huyo alitaja la pili kuwa ni watu wasichakachue vyakula wanavyokula kila siku.

“Sukari huharibu meno na tatizo la meno kuoza ni kubwa, wengi meno yameharibika kwa sababu ya ulaji wa sukari kwa wingi, asali nayo ni sukari wakati mwingine huwa tunasahau tukifikiria ni salama hapana, imejaa sukari kweli. Tukumbuke vyakula hubadilishwa kuwa sukari tumboni, si mdomoni.

 Alikumbusha kuwa watu wasitumie zaidi ya vijiko vitano vya sukari kwa siku wala kutumia vyakula au vinywaji vilivyoongezwa sukari.

“Oksijeni tunayopumua huunguza sukari mwilini ili tupate joto/nguvu. Jikoni moto ukizidi nyama huungua, mwilini sukari ikizidi mwili huungua,” alikumbusha.

Prof. Swai alitaja jambo la tatu kuwa ni watu wasile kwa wingi hadi kunenepa, huku akielimisha kwamba vyakula vyote huweza kunenepesha.

Alikumbusha kuwa watu wasizidishe kijiko kimoja cha chumvi kwa siku kwa sababu huongeza msukumo wa damu.

“Tumia mafuta kidogo tu ya mimea si ya wanyama kwa sababu mafuta mengi huchangia kuziba kwa mishipa ya damu. Usizidishe vilevi kwa sababu huchangua kuharibu ubongo, moyo, kongosho na ini na matibabu ni gharama,” alisema.

Jambo la nne, alilitaja kuwa ni watu wapende kushughulisha mchana kwa sababu huondoa chumvi mwilini na kufanya mzunguko wa damu usiongezeke, hupunguza unene na msongo wa mawazo, huimarisha misuli/mifupa na kuongeza kinga ya mwili.

Alisisitiza kwamba kila saa mtu anapaswa kushughulisha mwili kwa angalau dakika tano na kutoa jasho kwa angalau dakika 30 kila siku.

“Tano, tupumzike usiku tulale angalau saa saba ili mwili kuweza kujikarabati, sita usitamani vya watu, ukiwa na tamaa mbaya alafu malengo yasipofikiwa huleta msongo wa mawazo na kuna uwezekano wa kupata kisukari, msukumo wa juu wa damu na saratani.

“Saba, epuka tumbaku kama tunavyojua tumbaku huchangia magonjwa mengi na la mwisho chunguza afya kila mwaka,” alisema.

Prof. Swai alisema magonjwa mengi yasiyoambukiza hayana dalili hadi mwili umeshadhurika vibaya, hivyo ni lazima watu kujenga tabia ya kuchunguza afya zao angalau mara moja au mbili kwa mwaka ili kujua hali zao.

Msaikolojia Tiba na Mtaalam wa Afya Akili, Isaac Lema,  ambaye pia ni kiongozi wa Chama cha Afya Akili Tanzania, alisema afya ya akili nayo hutakiwa kuchunguzwa kama magonjwa mengine.

“Tunapozungumzia afya ya mwili na afya ya akili iwe bora na nzuri. Hata tukizungumzia afya ya akili mahali pa kazi tumegundua watu wengi tulianza kazi tukiwa na afya bora ya akili, hatukuanza na afya duni ya akili.

“Ukiitafuta hiyo afya bora nenda kwenye CV (wasifu) yako ulijiandaa. Afya ya akili inaruhusu mwonekano wako uzungumze na mtu unayekutana naye.

“Pamoja na kwamba kuna afya tukumbuke kuna changamoto ya magonjwa, na magonjwa yanapokuja afya inaweza kubaki bora au ikawa duni.