KAMATI nne za Kudumu za Bunge zimewaalika wadau kutoa maoni kuhusu miswada minane ya sheria ukiwano Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Hifadhi za Jamii wa Mwaka 2024.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kitengo za Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa, Ofisi ya Bunge, maoni hayo yataanza kupokewa kuanzia Agosti 14 hadi 16, mwaka huu.
Taarifa hiyo ilisema Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria itapokea maoni kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Shule ya Sheria Tanzania wa mwaka 2014 (The Law School of Tanzania).
Mingine ni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa Mwaka 2024, Muswada wa Sheria ya Marekebisho mbalimbali (Na.2) wa Mwaka 2024 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wa mwaka 2024.
Aidha, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii itapokea maoni kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii wa Mwaka 2024 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria zinazohusu Ulinzi wa Watoto.
Taarifa hiyo ilisema kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo itapokea maoni ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ushindani wa Haki wa Mwaka 2024.
Kadhalika, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu itapokea maoni ya Muswada wa Sheria ya Viwanja vya Ndege Tanzania wa Mwaka 2024.
Taarifa hiyo ilisema kuwa kamati zitapokea na kusikiliza maoni ya wadau kuanzia saa 4:00 asubuhi Agosti 15 hadi 16, mwaka huu.
Pia taarifa ilisema Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria itapokea maoni ukumbi wa Frank Mfundo, jengo la utawala Ofisi ya Bunge jijini Dodoma.
Taarifa hiyo ilisema Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii itapokea maoni Agosti 15 na 16, mwaka huu, katika ukumbi wa Pius Msekwa, Ofisi ya Bunge, jijini humo.
“Agosti 14, mwaka huu, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo itakutana katika ukumbi wa Msekwa D, jengo la Pius Msekwa, Ofisi ya Bunge Dodoma.
“Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu itakutana katika ukumbi namba 231, jengo la utawala Ofisi ya Bunge,” ilisema.
Taarifa hiyo ilisema maoni yanaweza pia, kuwasilishwa kwa njia ya posta kupitia anuani ya Ofisi ya Bunge au kupitia barua pepe za [email protected] na [email protected]. Miswada husika inapatikana katika tovuti ya bunge ya www.bunge.go.tz .
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED