UTOAJI wa zawadi mbalimbali zikiwamo ng’ombe na fedha kwa wazazi wanaowafanyia ukeketaji watoto wao zimetajwa kushawishi na kusababisha ongezeko la vitendo hivyo.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wameiomba serikali kushirikiana na wadau kudhibiti matukio hayo ya ukatili wa kijinsia yanayovua utu wa binti.
Ombi hilo walilitoa katika kikao cha kuweka mikakati ya kuzuia ukatili wa kijinsia wilayani Tarime, mkoani Mara kupitia mradi wa “Haki Yangu Chaguo Langu”.
Mradi huo unatekelezwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) kwa ufadhili wa serikali ya Finland.
Mkazi wa Kijiji cha Susuni, Penina Samson, alisema ukeketaji hauwezi kwisha kwa haraka kwa sababu wazazi wenye watoto wanapewa zawadi ya fedha, kanga, vitenge na wakati mwingine mbuzi na ng’ombe kama zawadi za kumfanyia mtoto ukeketaji.
Alisema zawadi hizo hutolewa siku ya sherehe za kuwafanyia ukatili mabinti.
Samson alisema ili kuondoa tatizo hilo ni vema kuwafikia wananchi wa vijijini na kuwaelimisha kuhusu madhara yake na baadaye kuanza kuwachukulia hatua kali za kisheria, wazazi na walezi wanaoshiriki kuendeleza na adhabu zao zitangazwe katika vyombo vya habari.
Bhoke Marwa alisema baadhi yao wamekuwa wakiwafanyia ukeketaji watoto wachanga kwa kurubuniwa na wakwe zao na kliniki ya kwanza wanapowapeleka hospitalini au vituo vya afya, anakuwa tayari ameshakeketwa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Korotambe, Kata ya Mwema, Joseph Chacha, alisema kumekuwapo na unyanyasaji unaombatana na udhalilishaji wakati wa ukeketaji kwa watoto wa kike, kwa kuvuliwa nguo mbele za watu, kitendo ambacho sio sawa na kinapaswa kukemewa.
Mratibu wa Haki Yangu Chaguo Langu kutoka WiLDAF, Joyce Kessy, alisema uundwaji wa sheria ndogo katika vijiji utasaidia kukabiliana kwa kiasi kikubwa na tatizo hilo.
Alisema bila kuweka sheria zitazowabana, wahusika wa ukeketaji wataendelea bila kificho wakiamini wanatekeleza mila bila kujua hawatendi haki kwa watoto.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, alisema hata sita kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kuendeleza vitendo hivyo katika jamii, kwani vinavua utu na udhalilishaji wa binti.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED