Maswali matano ya Ado kwa Dk. Nchimbi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 12:42 PM Sep 15 2024
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ado Shaibu
Picha: ACT
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ado Shaibu

Nukuu kutoka katika mkutano wa Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ado Shaibu unaoendelea katika Kata ya Kilindoni Kisiwani Mafia jana Septemba 14, 2024.

"Dk. Nchimbi, Katibu Mkuu wa CCM  amesema kuwa utekaji unaoendelea nchini haufanywi na vyombo vya dola wala CCM bali genge la watekaji wasioitakia mema CCM. Kauli hii ni kutoka kwa Dk. Nchimbi ni nzito na inazalisha maswali matatu ambayo ni lazima yajibiwe. Kwa hakika, haiwezi kupita bila mjadala"

"Mosi, Dk. Nchimbi atueleze genge hilo, ambalo bila shaka analifahamu ndio maana amejenga hitimisho la uwepo wake linaongozwa na nani na lengo lake hasa ni lipi?"

"Pili, Dk. Nchimbi atueleze genge hilo ambalo anasema limefanikiwa sana limeishinda nguvu Serikali? Ni lini Serikali itakomesha vitendo vya utekaji ambavyo anasema vinaongozwa na genge hilo? Ni lini Serikali itatekeleza wajibu wake wa kikatiba  wa kulinda raia na mali zake?"

"Tatu, Dk. Nchimbi atueleze uchunguzi ambao Mh. Rais ameutangaza ufanyike unaongozwa na nani? Unaongozwa na Jeshi la Polisi ambalo ni mshukiwa na mtuhumiwa mkuu au unaongozwa na chombo huru cha uchunguzi? Kama unaongozwa na Polisi, kwa nini mshukiwa amepewa kazi ya kuchunguza analotuhumiwa nalo? Sisi ACT Wazalendo tunaamini uchunguzi ni lazima ufanywe na chombo huru"

1

"Nne, Dk. Nchimbi anataka tuviamini vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo Jeshi la Polisi na kwamba watu wachache kwenye vyombo hivyo wanapokwenda kinyume tusiondoe imani kwa vyombo vyote kwa ujumla wake. Dk. Nchimbi anataka tuendelee kujenga imani hata kama utekaji na mauaji vinaendelea? Tuendelee kutabasamu tukitekwa, kuteswa na kuuawa? Haoni wananchi wanakosa imani kutokana na kushamiri kwa matukio na vyombo vyenyewe vya ulinzi na usalama kuonesha kutojali?

"Mwisho, Rais aliunda Tume ya Haki Jinai iliyomshauri Mh. Rais kufanya mageuzi makubwa kwenye vyombo vya haki jinai ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama. Dk. Nchimbi hakugusia kabisa mageuzi makubwa ya vikosi vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha vitendo vya utekaji havienei. Dk. Nchimbi anaamini majeshi yetu katika muundo wa sasa yanaweza kuleta ufanisi juu ya masuala haya  utekaji na usalama wa raia kwa ujumla wake bila mageuzi ya kimuundo, kisheria na kikatiba?