HILI ni janga linalowanyemelea wagonjwa wengi wanaougua magonjwa mbalimbali, yakiwamo sugu kwa kukatiza dozi wanapoona wana unafuu.
Wataalam wa afya, wakiwamo madaktari, wamebainisha suala hilo lipo katika jamii na husababisha madhara vikiwamo vifo huku wakiwatupia lawama baadhi ya viongozi wa dini wanaowaombea na waganga wa kienyeji kuwa sehemu ya chanzo cha kuwapo hali hiyo.
Kwa mujibu wa matabibu hao, wagonjwa huacha dozi kwa kuambiwa watapona baada ya kufanyiwa maombi, huku waganga wa kienyeji wakidaiwa kushawishi kuacha dawa walizopewa na wataalam wa afya na kuwataka watumie dawa za asili.
Daktari Bingwa kutoka Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma, Dk. Joshua Youze, anasema kutokumaliza dozi hususan kwa wagonjwa wanaougua maradhi mbalimbali, yakiwamo sugu, kunachangia kuleta fangasi na kuongeza tatizo la usugu mwilini.
Anasema moja ya tatizo sugu linaloweza kupatikana kwa mgonjwa aliyeacha dozi ni pamoja na mgonjwa kupata fungasi akiwa na ugonjwa ngozi.
Dk. Youze anasema mgonjwa wa aina hiyo akirejeshwa tena hospitalini inabidi abadilishiwe dozi na kupewa nyingine kali ili ugonjwa wake upone. Anasema baada ya uchunguzi kufanyika, wamebaini suala baadhi ya watumishi wa Mungu kulingana na imani zao za dini ni chanzo kikubwa cha wagonjwa kuacha dozi wanazopewa.
“Hili suala linatuumiza sana madaktari, tunaomba serikali iliangalie suala hili. Dini haikatazwi lakini wasimwaribie dozi mgonjwa aliyeenda katika maombi,” anasema Dk. Youze.
Pia anasema imani za kishirikina nazo huchangia kwa kiasi kikubwa wagonjwa kukatisha dozi wanazopewa na madaktari, hivyo kuiomba kuingilia kati baadhi ya madhehebu ya dini ambayo huchangia wagonjwa kutupa dawa na kuendelea na maombi kitu ambacho siyo sahihi wanatakiwa kuwa na mipaka.
Anasema hakuna mtu asiyesali wala kuomba, lakini inapofika suala la tiba ni lazima ingatiwe ili dawa zilete uponyaji.
Anasema kinachopaswa kufanyika ni pamoja na jamii kujengewa uwezo wa umuhimu wa kutumia dawa pamoja na kupewa elimu kuhusu madhara ya kuachilia dozi ili hali unaumwa.
Anafafanua kuwa kitendo cha viongozi wa baadhi ya madhehebu ya dini kuwakataza wagonjwa wasitumie dawa ili waendelee na maombi ni kuingilia kazi za madaktari.
Jambo hilo limeungwa mkono na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Enock Mlyuka, ambaye anasema baadhi ya watu wanaojiita watumishi wa Mungu wanafanya huduma wanazofanya kwa kisingizio ni huduma ya Mungu.
“Lengo ni kutumia matatizo ya watu kujinufaisha na ili afanikiwe lazima afanye mambo ya kuvutia watu wamuone ni mtu wa pekee.“Hayo mambo yanayofanywa na baadhi ya watu wanaojiita watumishi wa Mungu ni pamoja na kufanya matendo yanayoonekana ni ya kiroho, kama miujiza na kwa kuwa watu wengi wana matatizo na wanapenda miujiza watakwenda.
“Hao wanaojiita watumishi wa Mungu ni kama hawaamini kwamba, Mungu amegawa vipawa, ujuzi na maarifa kwa watu mbalimbali na huo ujuzi na maarifa unatoka kwa Mungu kusaidia jamii. Mfano madaktari na wauguzi hospitalini, ile ni huduma ya Mungu,” anasema.
Dk. Mlyuka anasema watu hao ili kuonekana ni wa pekee, wanachofanya ni kuonesha kule (hospitalini) sio ila huduma zao ndio.
“Na mtu anapokwenda kwao akiwa na matatizo ambayo yatahitaji wataalam wa afya, watamwambia usiende kule utapata huduma ya uponyaji hapa na mwishoe huishia kufa. Huo ni utapeli wa kiroho na haukubaliki na wanachafua kada ya utumishi wa Mungu,” anasema.
HOLELA HOLELA ITAKUKOSTI
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Prof. Said Aboud, anasema kuna utafiti mbalimbali uliofanyika kuhusu Usugu wa Vimelea vya Dawa za Antibiotiki (UVIDA).
“Matokeo ya utafiti huo ni kuongezeka kwa UVIDA, kutopona ugonjwa unaotibiwa, kusababisha kifo, kuongezeka kwa muda wa kukaa hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
“Usitumie dawa yoyote bila ya cheti cha daktari. Kuna kampeni inayoendelea ya kuelimisha wananchi kuhusu UVIDA, inaitwa ‘holela holela itakukosti,’” alisema.
HUCHANGIA VIFO
Mratibu wa Kifua Kikuu Halmashauri ya Wilaya ya Meru, mkoani Arusha, Dk. George Marwa, anasema mgonjwa anapoandikiwa dozi na kutomaliza, kuna uwezekano mkubwa wa kutokupona na kufariki dunia.
Anasema sababu ya pili ni pamoja na vimelea vya ugonjwa kuwa sugu na kutokusikia dawa, huku akitolea mfano wa mtu mwenye Virusi Vya UKIMWI (VVU) ambaye huchangia virusi kushamiri na kutosikia dawa pale anapokatisha dozi ya Kifua Kikuu (TB) na anapobainika kuwa nayo.
“Athari ni nyingi na kwa sababu hiyo ni lazima watu wazingatie kumaliza dozi wanazoandikiwa ili kukomesha usugu, kurudiwa na ugonjwa au wakati mwingine kupelekea kifo,” anasema Dk. Marwa.
Daktari Jimmy Julius wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Tanga - Bombo, anasema kutokumaliza dozi huchangia vimelea vya wadudu kuendelea kuwapo mwilini kutokana na kutokupata tiba sahihi.
Dk. Julius anasema kwa kufanya hivyo huchangia mgonjwa kutumia gharama kubwa zaidi katika kupata matibabu, hivyo kushauri kuzingatia maelekezo ya wataalam wa afya.
Naye Daktari wa Magonjwa ya Afya ya Akili hospitalini hapo, Dk. Wallace Karata, anasema kutomaliza dozi ambayo mgonjwa ameandikiwa husababisha usugu wa dawa mwilini.
Daktari wa Kitengo cha Upasuaji kutoka Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Manyara, Dk. Ludovick Legama, anasema wagonjwa ambao hawamalizi dawa wanazoandikiwa huwa hawaponi na wanaharibu soko la dawa husika na kuwapa nguvu bakteria ya kuendelea kuishi mwilini.
“Bakteria huwa wanaweza kujipanga namna ya kuharibu hiyo dawa kwa kuwa ukiacha dawa wanatengeneza mazingira ya kuikwepa ili isiwadhuru.
“Wale wadudu tukipandikiza na bakteria 10 baada ya siku saba, tunakuta wapo 20 tunajua wamezaliana baada ya hapo tunawawekea dawa kuona kama wamekufa, na iwapo wamekufa tunajua dawa imefanya kazi au kama hawajafa tunajua wamejenga usugu,” anasema.
Daktari kutoka Hospitali ya Rufani ya Kanda KCMC, Dk. Ebenezer Mary, anasema kwa sasa kumekuwa na matatizo ya umezaji wa dawa bila kufuata maelekezo ya matatibu, hali inayochangia matatizo hasa ya usugu wa dawa.
‘Ingawa sina takwimu kamili ila hali ni mbaya kwa jamii, watu wengi hutumia dawa na kukatisha dozi na wengine kutumia dawa kwa hisia wanaumwa ugonjwa fulani, hii inapaswa kukemewa na jamii kuelimishwa kutokana na madhara yanayoweza kutokea,"anasema Dk. Maro.
Aidha, anawataka wanasiasa kutumia muda mingi kuelimisha wananchi kwa lengo la kukuza jamii yenye afya bora.
Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Igalla, Ukerewe mkoani Mwanza, Dk. Jeremia Katwale, anasema wagonjwa wengi hasa wa Malaria hawamalizi dozi kwa sababu ya harufu ya dawa, wingi wa vidonge na siku za kumeza kuwa nyingi, hivyo wakiona wana nafuu huikatisha.
“Dozi ya Malaria ukimeza ya kwanza na dozi ya pili inatibu kwa asilimia 90 na hizo dozi zilizobaki ndio zinamalizia asilimia 10 iliyobaki, ndiyo maana mtumiaji akimeza dozi ya pili unakuta amepata unafuu na kuona hakuna haja ya kumalizia,” anasema.
Dk. Katwale anasema kuwa athari zinazoweza kupatikana ni usugu wa dawa ambapo mgonjwa akipatwa na ugonjwa, dawa aliyoitumia mwanzo inaweza isimtibu.
Anasema changamoto nyingine ni baadhi ya wagonjwa kuwa na Imani na miti shamba wakati ugonjwa alionao mfano Malaria unapaswa kutibika na dawa za hospitalini.
· IMEANDALIWA na Romana Mallya (DAR), Renatha Msungu (DODOMA), Jaliwason Jasson (MANYARA), Tumaini Mafie (ARUSHA), Mary Mosha (MOSHI), Assenga Oscar (Tanga) na Neema Emmanuel, (MWANZA)
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED