RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kuna umuhimu wa kufanya utafiti mwingi ili kupata jawabu la changamoto za kiusalama kwa mataifa mbalimbali duniani.
Pia amesema serikali itaendelea kukiunga mkono Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) ili kiendelee kutoa michango chanya katika masuala ya kiusalama kitaifa, kikanda na kimataifa.
Aliyasema hayo jana katika mahafali ya 12 ya chuo hicho, Kunduchi, Dar es Salaam kwa wahitimu wa kozi ndefu ya mwaka 2023/24. Kati ya wahitimu 57 kutoka mataifa mbalimbali, wanawake walikuwa 12.
Rais Samia alisema serikali itakiwezesha chuo hicho kuwa kituo mahiri cha utafiti wa masuala ya ulinzi wa kimkakati ili kutatua changamoto mbalimbali zilizoko.
“Kuna umuhimu wa kufanya utafiti mwingi ili kupata jawabu la changamoto za kiusalama kwa mataifa mbalimbali duniani. Ni muhimu kuwekeza katika utafiti na kushirikiana na washirika ili kupata matokeo yanayotarajiwa,” alisema.
Aidha, Rais Samia alikitaka chuo hicho kuendelea kuwekeza kimkakati kwa taifa kwa kuunga mkono utafiti wenye tija na kushirikiana na taasisi zingine za utafiti ili kuiwezesha nchi kupata maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Rais aliwataka wahitimu Watanzania na wa mataifa ya kigeni kutoka nchi 15 kuendeleza ushirikiano ili kuweza kupata suluhu za pamoja katika kutatua changamoto za kidunia kwa utaalam.
Kadhalika, aliutaka uongozi chuoni hapo kuhakikisha idadi ya wanawake wanaodahiliwa kusoma kozi ndefu inaongezeka.
Mkuu wa Chuo, Meja Jenerali Wilbert Ibuge, alisema wahitimu hao wamechukua mafunzo ya miezi 10 yaliyoanza Septemba, mwaka jana, na wanatarajia kuhitimu mwezi ujao.
Alisema kati wahitimu hao 57, kati yao 10 walikuwa wakisoma stashahada ya Mafunzo ya Usalama na Stratejia na wengine Shahada ya Uzamili.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED