CHAMA cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimemshauri Rais Samia Suluhu Hassan, kuunda tume maalumu ya kuchunguza matukio yote ya kudaiwa kupotea kwa watu, kutekwa na kuteswa.
Pia kimemshauri Rais Samia kuunda tume maalum ya kuchunguza ushiriki wa Jeshi la Polisi katika masuala ya utekaji kwa inachodai kuwa jeshi hilo limekuwa likituhumiwa kushiriki katika vitendo hivyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na juzi na Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi, chama kinasikitishwa na kinalaani vitendo vya kukamatwa, kutekwa na kuteswa kiholela kwa wananchi kunakoendelea nchini bila ya vyombo husika vya dola kuwajibika ipasavyo.
“Kumekuwapo na taarifa mbalimbali za watu kupotea katika mazingira tatanishi, kutekwa na kuteswa na baadaye kuonekana, huku baadhi yao wakiwa wamefariki dunia na wengine wakiwa na majeraha makubwa katika miili yao.
“Tunasikitishwa pia na namna ambavyo vyombo vyetu vya dola hususani Jeshi la Polisi limekuwa likifanyia kazi taarifa hizo. Mara kwa mara Jeshi la Polisi limekuwa likikanusha kutokea kwa matukio hayo, lakini baadaye inakuja kubainika kwamba, matukio hayo ni ya kweli,” alidai Mwabugusi.
Kutokana na matukio hayo, TLS imependekeza kuundwa kwa chombo maalumu cha kudumu cha kuangalia utendaji wa vyombo vya dola ili kuhakikisha vinafanya kazi kwa mujibu wa katiba na sheria.
“Tunalitaka Jeshi la Polisi kufanya kazi yake kwa weledi kwa mujibu wa katiba na sheria ili kuhakikisha usalama na ulinzi wa wananchi na mali zao unaimarika.
“TLS inaendelea kufuatilia matukio haya kwa ukaribu na iko tayari kushirikiana na vyombo vyote vya dola katika kuhakikisha wahusika wote wa matukio haya wanafikishwa katika vyombo mahususi vya haki ili haki ionekane inatendeka,” alisema.
Mwabugusi alisema TLS inatoa rai kwa watanzania wote kuwa makini wakati wote na kutokubali kuitwa au kukutana na watu wasiowajua au kwenda mahali wasipopajua na ikibidi wawasiliane na wakili yeyote kabla ya kukutana au kwenda mahali wasipopajua.
Katika taarifa yao, TLS imedai mara nyingine Jeshi la Polisi limekuwa likiwakamata raia wema wanaotoa taarifa hizo kwa kile kinachosemekana kusambaza taarifa za uongo badala ya kufanyia kazi taarifa hizo kwa mujibu wa Katiba na sheria zinazowapasa kufanya wajibu wao wa kulinda watu na mali zao.
“TLS kwa mamlaka iliyopewa kupitia kifungu cha 4 cha Sheria iliyounda TLS (Tanganyika Law Society Act, Cap. 307 R.E. 2002), inapenda kuvikumbusha vyombo vya dola hususan Jeshi la Polisi kuhusu majukumu yake ya kikatiba na kisheria ya kulinda watu na mali zao,” alisema.
Mwabugusi alisema matukio hayo ni kinyume na Ibara ya 13 (6) (e) na 14 ya Katiba; pamoja na mikataba ya kimataifa inayozungumzia haki za binadamu na inayozuia uteswaji wa watu kama vile Mkataba dhidi ya mateso na unyanyasaji au adhabu nyingine za kikatili au udhalilishaji.
“Kinyume cha Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa. TLS inatambua na kuheshimu taarifa za Jeshi la Polisi zinatolewa zikitaarifu umma kwamba, matukio hayo yamekuwa yanafanyiwa uchunguzi.
“Lakini tunasikitika kwamba hakuna taarifa kamili ya uchunguzi wa tukio hata moja ambayo imewahi kutolewa kwa umma kuhusu hatua zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi juu ya watuhumiwa wa matukio hayo,” alisema.
Mwabugusi alisema hali hiyo inaendelea kutia hofu kwa wananachi kuhusu usalama wao na mashaka ya uwezo wa Jeshi la Polisi kuchunguza na kuchukua hatua stahiki kwa wahusika wa matukio hayo.
“Kupitia tamko hili, tunaambatanisha orodha ya baadhi ya watu ambao wananchi au na vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini vimewahi kutoa taarifa za kupotea au kutekwa kwao. Baadhi yao walipatikana na baadhi yao wakiwa na majeraha huku kukiwa na wengine ambao waliopotea katika mazingira tatanishi na hawajapatikana mpaka leo,” alisema.
Katika taarifa hiyo, TLS imetaja watu 83 wanaodaiwa kutekwa au kupotea kwa miaka minane kuanzia mwaka 2016 hadi 2024.
Waliodaiwa kutekwa na baadhi kupatikana waliowataja ni pamoja na Ben Saanane (Dar), Azory Gwanda (Pwani), Simon Kanguye (Kigoma) na Joshua (Iringa).
Wengine Kombo Twaha (Handeni-Tanga), Kennedy Mwamlima mkazi wa Mbeya Edger Mwakalebela (Dar), James Sije (Nyakato-Mwanza), Joseph Mnyonga (Mwanza), Dotto Kabwa (Ifunga-Iringa) na Yahya Ally (Dar).
Chande Kizega (Dar), Mzee Samuel Mkongo (Geita Mjini), Charles Mwampyate (Dar), William Herman (Kangaye-Mwanza), David Lema (Mwanza), Jerome Kisoka (Kilimanjaro) na Ridhiwani Msangi (Iringa).
Benson Ishungisa (Dar), Hamza Said (Mwatulole-Geita), Yonzo Dutu (Kishapu-Shinyanga), Lilenga Isaya (Mwandiga-Kigoma), Tawafiq Mohamed (Dar), Self Swala (Dar), Edwin Kunambi (Dar), Hemed Abass (Dar), Maseke Mwita (Mara) na Rajab Mdoe (Dar).
Wengine ni Mzee Haji Soft (Dar), Alphonce Bilasenge (Kagera), Albert Selembo na Moloimeti Saing’eu, Ndirango lazier, Joel Lessonu, Simoni Orosikiria, Damian Laizer, Mathew Siloma na Lukas Njausi.
Taleng’o Leshoko, Kijoolu Olojiloji, Shengena Killel, Malongo Paschal, Simeli Korongoi, Ingoi Kanjwei, Sangau Ngiminis, Marijoi Parmati, Morongeti Masako, Kambatai Lulu na Orias Oleng’iyo.
Wilson Kolong, James Taki, Joseph Jartan, Kelvin Nairoti, Lekerenga Orodo, Fred Ledidi, Simon Morintanti wote kutoka Loliondo, mkoani Arusha.
Wengine ni Mohamed Kalebe (Geita), Amon Magige (Mwanza), Aziz Kinyonga na Yusuph Dudu kutoka Dar es Salaam, Kastory Kapinga (Mbinga), Dioniz Kipanya (Rukwa), Shadrack Chaula (Mbeya) na Prosiper Mnjari (Dar).
Pia wamo Thomas Ihuya (Mwanza), Dennis Kantanga (Shinyanga), Damas Bulimbe na Lucas Bulimbe (Geita), Matuki Makuru (Mara), Dastan Nestory na Adinan Mbezi wote kutoka Geita.
Lengaripo Lukumay (Mwanza), Akidu Salim (Dar), Enock Chambala (Tanga), Dioniz Kipanya (Katavi), Nusra Omari (Dar), Theresphora Mwakalinga (Dodoma), Donald Mboya (Kagera), Ilham Makoye, Barack Majigeh, Yusra Musa, Angel Kamugisha, Brighton Emmanuel wote kutoka Dar.
Mwabukusi alisema wanaamini Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola vitafanyia kazi na kuhakikisha watu hao wamepatikana na wahusika wote wa matukio hayo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo husika vya haki ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED