WADAU wa demokrasia wameibua upya hoja ya mgombea binafsi, wakieleza kuwa itaondoa manyanyaso, udhalilishaji na chuki.
Akizungumza katika maadhimisho Siku ya Demokrasia Duniani yaliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), yaliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mwanasiasa na msomi nguli, Prof. Anna Tibaijuka, alisema iwapo mapendekezo hayo yatafanyiwa kazi, baadhi ya viongozi watarajiwa wanaokutana na manyanyaso ndani ya vyama vyao, watasimama katika uchaguzi.
Prof. Tibaijuka alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika demokrasia angalau kumekuwa na mwamko wa ushirikishwaji wa makundi maalum wakiwamo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga, alisema moja ya eneo mtambuka katika haki za demokrasia ni ushiriki wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika vyombo vya uamuzi na michakato ya kiuchaguzi.
Alisema kwa miaka mingi kama taifa kumekuwa hakuna sheria mahsusi zinazoainisha utaratibu utakaohakikisha ushiriki au kuongezeka kwa makundi hayo ukiondoa ule wa viti maalum ulioainishwa katika Ibara ya 66 na ule wa wabunge wa kuteuliwa na Rais kwa mamlaka aliyopewa na Katiba ya Mwaka 1977.
Dk. Henga alisema licha ya kuwapo wa mfumo huo, bado kumekuwapo na malalamiko ya wadau kutokana na mfumo huo kuwa na mapungufu, eneo la vijana na watu wenye ulemavu bado hakuna mfumo wowote wa kisheria unaoainisha ushiriki wa kundi hilo katika vyombo vya maamuzi.
“Nchi yetu inaelekea kwenye matukio makubwa mawili yanayoshabihiana na demokrasia, lile la uandikishwaji na uboreshwaji wa daftari la kudumu la wapigakura na Uchaguzi wa Serikali wa Mtaa, hivyo siku hii ni maandalizi kuelekea matukio hayo,” alisema.
Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes, alisema demokrasia ni mhimili mkubwa kwa binadamu na kuomba asasi za kiraia vyama vya siasa na serikali kuungana kwa pamoja katika kuijenga.
Alisema demokrasia na maendeleo ni vitu vilivyofungamana kwa pamoja na nchi inapokuwa na uhuru wa kujieleza itasonga mbele na kuwa na maendeleo makubwa kwa kuwa nchi zote zilizoendelea hakukuwa na kuminywa kwa uhuru wakujieleza.
Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA), Catherine Magige, alisema katika ajenda ya maendeleo huwezi kumuondoa mwanamke katika jamii, hivyo kumekuwa na changamoto kubwa katika kufanya siasa mtu wa jinsia hiyo hasa katika vyama vya upinzani kutokana na mifumo iliyowekwa katika uchaguzi.
Alisema kuna mambo mengi ambayo yanaogopesha hususani kwa wanawake na Tume ya Uchaguzi imekuwa ikifinya na kufumbia macho baadhi ya vitendo vinavyojitokeza katika uchaguzi huku mfumo mzima wa uchaguzi ukiwa hauko sawa hasa katika kutumia vyombo vya dola vibaya.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED