JUKWAA la Waandishi wa Habari Wanawake, (WRIFOM), limezindua rasmi programu ya kuwawezesha waandishi wa habari wa kike kuandika habari za kuibua wanawake waliofanya vizuri kwenye demokrasia Tanzania ambao bado hawajatambuliwa ipasavyo.
Programu hiyo ilizinduliwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Wilaya mstaafu, Betty Mkwasa ambaye pamoja na mambo mengine, aliwataka waandishi hao wa habari ambao wamechanguliwa katika mradi huo, kufanya kazi kwa ubunifu kuwaibua wanawake waliofanya mambo mazuri kwenye eneo hilo la demokrasia na kuacha alama ili watumike kama mabalozi kwa wengine.
Betty alisema wapo wanawake wengi ambao wamefanya mambo makubwa katika eneo hilo ambao endapo wangeibuliwa, wangechangia kuleta chachu kwa wenzao wanaokata tamaa au kuogopa kufanya shughuli za kidemokrasia kutokana na vikwazo wanavyokutana navyo eidha kutokana na mila na desturi, mfumo dume au mazingira wanayokutana nayo.
“Ninachowaomba nendeni vijijini mkawaibue wanawake maana wapo baadhi yao ambao hata katika mkutano unaohusu kujadili changamoto zao labda shida ya maji iliyowatesa kwa muda mrefu na wao ndio wanajua uchungu wake, hawasimami kuzungumza hata kama viongozi wa serikali wameenda kuwasikiliza, wanasubiri eti mpaka mwanaume ndio aseme, mama anaambiwa hapaswi kusema,”alisema Betty.
“Kwa hiyo wapo baadhi yao hata kama wamefanya mambo mazuri wanaogopa kutoka na kuzungumza kwa sababu ya kuogopa hizo mila kwenye jamii zao, hivyo ninategemea kwamba ninyi waandishi wa habari mtafanya kazi nzuri ya kuwaibua wanawake hao.
“Ninawaomba ndugu zangu ninyi waandishi wa habari, unapofanya jambo lolote lile unatakiwa ujitahidi uache alama, usifanye kitu kwa sababu kinafanyika, jitahidi kila unavyoweza na ninaamini mnapokwenda kufanya kazi hii mtaliangalia hilo, mkumbuke kwamba jamii inawahitaji na inawategemea.”
Mwanzilishi Mwenza wa WRIFOM, Chelu Matuzya alisema lengo la kuja na mradi huo ni kuunga mkono harakati za wanawake kwenye demokrasia na kuondoa mitizamo hasi kwenye jamii.
“Ipo mitizamo hasi kwamba wanawake hawawezi kwenye siasa, ukiwapa nafasi hawawezi kufanya vizuri, ipo mingi tunaifahamu lakini lengo la kufanya huu mradi ni kwa sababu tunaamini kwamba habari tutakazokwenda kuziandika zitaleta mabadiliko makubwa,”alisema Chelu.
“Lakini pia zitasaidia kuonyesha uwezo wa wanawake kupitia mambo ambayo wameyafanya na hivyo kubadili mitizamo hasi iliyopo kwenye jamii na kuongeza motisha kwa wanawake hao na wale ambao wanatarajia au kutamani kuingia kwenye nyanja hiyo.”
Chelu alisema changamoto nyingi ambazo baadhi ya wanawake wamekuwa wakipitia hususani wanapoingia kwenye demokrasia zimechangia waone kwamba siasa au mambo ya kidemokrasia hayana maana na kwamba habari za kuwaibua ambazo zitaandikwa na waandishi wa habari zitasaidia kuwatia moyo na hata kuleta usawa wa kidemokrasia.
Alisema wameamua kuja na mradi huo kwa sasa kwa sababu wanatambua kuwa hakuna demokrasia kamili bila mchango wa mwanamke.
Mkurugenzi wa Mfuko wa Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Dustan Kamanzi, alisema wapo wanawake wengi ambao wanafanya kazi kubwa katika maeneo yao kama ilivyo kwa wanaume lakini mchango wao bado haujathaminiwa au kutambuliwa sana.
“Kwa mfano katika baadhi ya chaguzi wapo wanawake walijitokeza kugombea nafasi za juu kabisa tena wengine zilikuwa kwenye nafasi ya urais wakishindana na wanaume lakini pamoja na uthubutu huo hawakupewa nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari lakini hata jamii yenyewe haikuwapokea na kuwakubali kama ilivyokuwa kwa wagombea wanaume,”alisema Kamanzi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED