Makandarasi wapigwa msasa usimamizi wa fedha katika miradi ya ujenzi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:43 AM Dec 09 2024
Makandarasi wapigwa msasa usimamizi wa fedha katika miradi ya ujenzi
Picha:Mpigapicha Wetu
Makandarasi wapigwa msasa usimamizi wa fedha katika miradi ya ujenzi

Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) imewanoa makandarasi wazawa kuhusu usimamizi mzuri wa fedha kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi katika mafunzo ya siku tatu yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dodoma na kuwakutanisha washiriki kutoka mikoa mbalimbali.

Aidha, wamesisitizwa kutumia wataalamu wa fani stahiki katika makampuni yao na katika utekelezaji wa miradi ili kuepuka changamoto zinazoweza kuathiri utendaji wa makampuni au utekelezaji wa miradi. 

Lengo la mafunzo hayo ni kuwasaidia Makandarasi wazawa jinsi ya kusimamia fedha kwa kuhakikisha fedha zote zinakwenda kwenye mradi kama inavyotakiwa na kukamilika kwa muda uliopangwa kwa kuzingatia uandaaji wa mpango wa fedha ‘financial plan’ utakaowasaidia kujua namna ya watakavyozipata fedha na watakavyozitumia.

Pia makandarasi wamejifunza kuhusiana na usimamizi na maamuzi katika matumizi ya fedha ‘financial control and decision’ kwa kuhakikisha fedha zinafika katika maeneo husika na kufanyiwa matumizi kwa usahihi.

Aidha, kutokana na miradi mingi kuwa na changamoto ya kutokukamilika kwa wakati kutokana na fedha kupelekwa kwenye miradi isiyokusudiwa, makandarasi wameaswa kujipanga na kuwa na uhakika kuwa wana fedha za kutosha kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi kwa wakati kwani kwa kufanya hivyo italeta faida na tija kwenye kazi zao za kila siku.

Mshiriki wa mafunzo hayo Sophia Mtitime, alisema amefurahishwa kwa mafunzo hayo yaliyompa mwanga mpya wa utendaji mzuri katika usimamizi wa fedha kwenye utekelezaji wa miradi na aliahidi kwenda kuyafanyia kazi kwa ustawi wa kandarasi yake.

"Nimefurahi kuwepo katika mafunzo haya ya usimamizi wa fedha kwani hili limekuwa ni changamoto sana katika makampuni yetu  hali inayotufanya kushindwa kutekeleza miradi kwa ubora ama kupelekea hasara katika makampuni", alisema Mtitime.

Naye, Joseph Saimon, mshiriki mwingine wa mafunzo hayo alisema changamoto kubwa ya watendaji katika makampuni ya kikandarasi imekuwa ni kukosa uwelewa kuhusu matumizi mazuri ya fedha katika makampuni hali inayopelekea upotevu wa fedha, kushindwa kuendelea kwa makampuni na kupoteza mtaji.

 "kupitia mafunzo haya nitakwenda kuongeza ufanisi wa usimamizi wa fedha na uandaaji wa 'financial statement' kwa kuzingatia sheria za ndani na za kimataifa kama zilivyowekwa", alisema Joseph.