NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis amesema serikali imesajili miradi 63 ya biashara ya kaboni kupitia sekta mbalimbali.
hamis aliliarifu Bunge jijini Dodoma jana juu ya usajili huo wakati akijibu swali la Mbunge wa Amani, Abdul Yussuf Maalim aliyetaka kujua mpango wa serikali kupanua wigo wa biashara ya kaboni ili kupunguza uharibifu wa ukataji misitu nchini.
Naibu Waziri Khamis alitaja sekta zilizo katika miradi iliyosajiliwa ni pamoja na kilimo (asilimia nane), nishati (asilimia 33), misitu (asilimia 51), mifugo (asilimia tano) na usimamizi wa taka (asilimia tatu).
Alisema kuwa kati ya miradi iliyosajiliwa kupitia sekta ya misitu, minne inahusisha shughuli za upandaji miti, miradi 20 ni kwa ajili ya kupunguza uharibifu na upotevu wa misitu na miradi mitano ni kwa ajili ya kurejesha uoto wa asili.
Khamis pia alieleza kuwa serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024 – 2034) ambao unahamasisha matumizi ya nishati safi za kupikia, ikiwamo gesi asilia, nishati jadidifu, mkaa mbadala na umeme ambazo zinaweza kuchangia katika biashara ya kaboni na kupunguza matumizi ya kuni na ukataji misitu.
Alisema serikali pia imeandaa na inatekeleza Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu 2024 na Mkakati wa Utekelezaji Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu (2024 – 2034).
"Katika Sera hii ya Taifa ya Uchumi wa Buluu, tumeweka mikakati ya kuhamasisha matumizi ya hati fungani za buluu na biashara ya kaboni katika shughuli za rasilimali za uchumi wa buluu kwa lengo la kuongeza wigo wa biashara ya kaboni nchini ili kuimarisha uhifadhi wa mazingira," alisema.
Naibu Waziri Khamis pia alisema serikali inachukua mipango madhubuti kuhakikisha misitu inakuwa sehemu ya mapato kupitia biashara ya kaboni katika vijiji, shehia na wilaya kwa kuwashirikisha wananchi katika kuihifadhi.
Akijibu maswali la nyongeza kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali kuitunza misitu na namna Zanzibar ilivyonufaika na biashara ya kaboni, Khamis alisema Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza kutoa elimu katika ngazi mbalimbali, wakiwamo wabunge, kuhusu fursa zinazopatikana katika biashara ya kaboni kwa upande wa Zanzibar pamoja na kuwaunga mkono katika kuandaa kanuni za biashara ya kaboni.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED