RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan kesho anatarajia kuzindua taarifa ya tathimini ya utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara nchini (MKUMBI) jijini Dar es Salaam.
Aidha Rais Samia ambaye atawakilishwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, atazindua taarifa ya hali ya uwekezaji nchini ya mwaka 2023, mwongozo wa uanzishaji na uendeshaji wa kanda maalum za kiuchumi nchini, pamoja na mpango mkakati ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Arusha, Waziri Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof.Kitila Mkumbo amesema serikali ilianzisha mpango huo Juni 2019, kwa lengo la kufanya uchambuzi wa kina wa mazingira ya biashara nchini.
Amesema mpango huo ulilenga kuainisha mageuzi na hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika kutatua changamoto na kuboresha mazingira ya kufanya biashara pamoja na uwekezaji nchini.
"MKUMBI imefanikiwa kuainisha maeneo makubwa matatu ya kushughulikia uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini, ikiwemo gharama za kufanya biashara,mlolongo mgumu na mrefu wa kupata vibali vya kufanya biashara na uwepo wa utitiri wa mamlaka za udhibiti zinazorekebu shughuli za biashara nchini,"amesema.
Amesema katika kufanikisha mpango huo serikali iliajiri mtaalamu mshauri wa kufanya tathimini huru na ya kina ya miaka mitano ya utekelezaji wa mpango huo, ambapo tathimini inaonyesha mafanikio yaliyopatikana na changamoto mpya zilizojitokeza na mapendekezo ya hatua za kuchukua, ili kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Hafla ya uzinduzi wa taarifa ya tathimini ya MKUMBI itahudhuriwa na viongozi wa serikali,viongozi wa sekta binafsi na jumuiya za wafanyabiashara,wadau wa maendeleo,waandishi wa habari na wananchi walioalikwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED