KAMPUNI ya huduma za simu ya Yas kwa mara ya tatu mfululizo leo imetangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya Ookla ya mtandao wenye kasi zaidi Tanzania inayotolewa na kampuni ya Ookla ya nchini Marekani.
Akizungumza wakati wakupokea tuzo hiyo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yas Tanzania, Jerome Albou, amesema mafanikio waliyoyapata ya kushinda tuzo hiyo yanahakisi uwekezaji wao waliouweka katika kuimarisha miundo mbinu ya kampuni hiyo.
"Ni fahari yetu kupata tuzo hii kwa mara nyingine, hii inatokana na uwajibikaji wetu na uwekezaji mkubwa tuliouweka kwenye miundombinu, lakini kwa akipekee inatokana na wateja wetu wa thamani kuwa na sisi na kuendelea kutuunga mkono," amesema Albou.
Amesema kama kampuni wataendelea kuboresha huduma zao na kuendelea kuwekeza kwenye miundo mbinu.
Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa kampuni ya Ookla, Mkurugenzi wa mauzo kwa nchi za Mashariki ya Kati na Afrika, Osama Nawayseh, amesema tuzo hiyo inatokana na utafiti wao katika masuala ya mtandao ambapo kwa Tanzania Yas imeonekana kuwa na mtandao wenye kasi zaidi.
Amesema mchakato wa kupata mshindi ufanywa na jopo la wataalam kwa kupitia vigezo mbalimbali vya kimataifa.
"Tunawapongeza Yas kwa uwekezaji wao ambao umepelekea kupata tuzo hii kwa mara ya tatu, mtandao wao umeonekana kuwa wenye kasi zaidi, tunafurahi kukabidhi tuzo hii kwa mara nyingine," amesema Nawayseh.
Aidha, Mkurugenzi wa Ufundi na Mawasiliano wa Yas Tanzania, Emmanuel Mally, amesema tuzo hiyo imewatia moyo wa kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma bora kwa watanzania na kuendelea kuboresha miundo mbinu yao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED