SELEMANI Mzirai (49), mkazi wa Kiluvya, wilayani Kisarawe, mkoani Pwani, anadaiwa kujinyonga akiwa katika mahabusu ya mahakama wakati anasubiri kupelekwa gerezani baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha.
Selemani anadaiwa kujinyonga kwa kutumia shati lake alilolifunga kwenye nondo za dirisha la choo katika Mahakama ya Wilaya Kisarawe, jana.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo, Selemani alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kunajisi na kulawiti mtoto wake wa kufikia mwenye umri wa miaka saba.
"Baada ya kusomewa hukumu, Selemani aliingia chooni kujinyonga kwa kutumia shati lake alilolifunga kwenye nondo za choo hicho," alidai Kamanda Lutumo.
Alisema mwili wa Selemani umehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ukisubiri uchunguzi wa daktari na kukabidhiwa kwa ndugu kwa mazishi.
Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16, inaelekeza adhabu ya kifungo cha maisha kwa anayepatikana na hatia ya kunajisi mtoto mwenye chini ya umri wa miaka 10.
Sheria hiyo katika kifungu cha 130 (1) inaelekeza, "Ni kosa kwa mtu wa jinsia ya kiume kumbaka msichana au mwanamke."
Sheria hiyo inaelekeza katika kifungu cha 130(3) kuwa, "Bila ya kujali masharti yaliyopita ya kifungu hiki mtu yeyote atakayetenda kosa la kubaka msichana wa chini ya umri wa miaka 10, atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha."
Kifungu cha 131(1) cha sheria hiyo kinaelekeza, "Mtu yeyote atakayetenda kosa la kubaka, atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha, na kwa kila kesi ambayo kifungo chake hakipungui miaka 30 pamoja na adhabu ya viboko na faini, na atatakiwa kulipa fidia ya kiasi ambacho kitatamkwa na mahakama, kwa mtu ambaye ametendewa kosa hilo na kwa majeraha aliyoyapata."
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED