MKURUGENZI Mkaazi wa Shirika la WaterAid, Ana Mzinga, amesema bado kuna changamoto ya upatikanaji wa maji hasa katika zahanati na vituo vya kutoa huduma za afya vilivyojengwa jambo ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi.
Mzinga amesema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzunduzi wa mkakati wa Shirika la Water Aid kwa kuwashirikisha wadau wa maji na usafi wa mazingira (WASH).
Amesema maeneo hayo yanawakumba wanawake wengi ambao ndio watumiaji wa vituo vya afya hasa katika mambo ambayo yanahusika na uzazi.
“Tumeona kuna vituo vya afya ambavyo vinaonyesha huduma za maji na usafi wa mazingira hazijafika hili tunaliona ni tatizo ambalo linaweza kutatuliwa kwa pamoja ndio maana tumeamua kuanzisha mpango mkakati wa kuonyesha maeneo ambayo tunaweza kufanya kazi ili kuwasogezea huduma za maji hasa katika vituo vya afya na shule zetu,”alisema Mzinga.
Aidha, amesema mpango mkakati huo waliouanzisha wamejipanga katika kuleta taarifa rasmi ni wapi kunahitajika kufanyiwa kazi.
Amesema wanawekeza zaidi kufanya utafiti na kufuatilia maeneo ambayo yanahitaji kuwekwa kipaumbele na jambo jingine ni kuunganisha wadau ili kupanga kwa pamoja katika kutekeleza mkakati huo.
Naye Mbunge wa Nzega Vijijini, Dk. Hamis Kigwangalla amewataka wadau wa maji na usafi wa mazingira kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa sera na mipango yake ili kuwezesha utoaji wa huduma ya maji na usafi katika jamii.
Kigwangalla ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge wanaopiga vita Usugu wa Dawa Tanzania (UVIDA) alisema licha ya Tanzania kuwa na sera na mipango mizuri, hakuna utekelezaji.
“Kwanza ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa fedha za kutosha kwenye miradi ya maji na usafi wa mazingira kwa ujumla wake na pili ni kuhakikisha wadau wote wanakuja pamoja kusukuma ajenda hiyo ya mazingira kwa lengo la kumpa kipaumbele mwanamke,".
Awali akitoa mada katika mkutano huo, Mkuu wa kitengo cha sera na ushawishi kutoka WaterAid, Christina Mhando, amesema hadi mwaka 2021 vyanzo vinaonyesha kulikuwa na vituo vya afya 8,549 ikiwemo zahanati 7,200 na asilimia 74 zinamilikiwa na serikali.
Amesema karibu nusu ya vituo hivyo havina maji ya bomba na hata vilivyounganishwa na maji ya bomba havipati maji ya uhakika.
“Hadi asilimia 44 ya vyumba vya madaktari na asilimia 42 ya vyumba vya uzazi havina sehemu ya kunawia mikono ili kuwawezesha watoa huduma kufanya kazi kwa usafi.
Amesema hali hiyo inawaathiri watoa huduma walio mstari wa mbele kama wauguzi, wakunga na wanawake wakati wa kujifungua na wagonjwa wengine.
Naye Muuguzi na Mkunga wa kituo cha afya cha Msanga Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Robart Mgema, amesema awali walikuwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kituoni hali iliyowalazima wakina mama kuja na maji kwenye kituo cha afya wanapotaka kutibiwa.
Amesema kwa sasa wanashukuru kupatiwa mradi wa maji na shirika la WaterAid hali ambayo imewanufaisha wanawake kupata huduma sahihi katika mazingira bora.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED