DCEA yapongezwa mafanikio mapambano dawa za kulevya

By Zanura Mollel , Nipashe
Published at 11:48 AM Dec 07 2024
DCEA yapongezwa mafanikio mapambano dawa za kulevya
Picha: Mpigapicha Wetu
DCEA yapongezwa mafanikio mapambano dawa za kulevya

Naibu Waziri Msaidizi wa Shirika la Kimataifa la Dawa za Kulevya na Masuala ya Sheria (INL), Maggie Nardi, ameipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa mafanikio makubwa ya kudhibiti biashara na usafirishaji wa dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na kuvunja mitandao mikubwa ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kukamata kiasi kikubwa cha dawa hizo.

Naibu huyo ametoa pongezi hizo leo baada ya kukutana na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo.     

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Nardi alisisitiza juhudi za DCEA na serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Aliipongeza DCEA kwa kazi kubwa inayoendelea kufanyika, akiahidi kuendelea kushirikiana na mamlaka hiyo ili kufanikisha vita dhidi ya janga hili.

“Ninawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya katika kuvunja mitandao ya biashara ya dawa za kulevya na kukamata dawa nyingi. Ushirikiano wetu utaendelea kuimarika, na tunatoa pongezi kwa serikali ya Tanzania kwa jitihada zake madhubuti katika kukabiliana na changamoto hii,” alisema Nardi.

Naibu Nardi pia alifurahishwa na hatua zinazochukuliwa na DCEA katika kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya na kutoa huduma za tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya. “Sikufahamu kwamba DCEA pia inafanya kazi ya kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya pamoja na kupunguza madhara ya dawa hizo. Hii ni hatua nzuri ambayo inapaswa kuendelea,” alisisitiza.

Ziara hiyo pia ilijikita katika tishio la dawa za kulevya za kisintetiki, hasa fentanyl, ambapo Nardi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa na kubadilishana taarifa ili kukabiliana na changamoto hii.

“Natumai fentanyl haijaingia kwa wingi hapa nchini, lakini lazima tuchukue tahadhari. Tunaendelea kushirikiana na kubadilishana uzoefu ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya biashara ya dawa za kulevya. Marekani ilijifunza kutokana na kile kilichotokea katika majimbo ya Kaskazini Mashariki, na hivyo walijitayarisha vyema wakati fentanyl ilipokuwa ikienea. Hii inadhihirisha umuhimu wa kushirikiana taarifa mapema,” alisisitiza Nardi.

Ziara hiyo ni ishara ya ushirikiano wa kimataifa unaozidi kuimarika katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya, na DCEA inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kupambana na janga hili na kupunguza athari zake kwa jamii.