KADA wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Joseph Fuime amejiunga na Chama Cha ACT Wazalendo.
Kada huyo aliwahi kugombea Ubunge Jimbo la Songea Mjini kwa tiketi ya chama hicho mwaka 2015 na kukosa nafasi hiyo,pia aliwahi kushika nafasi tofauti tofauti ikiwamo Uenyekiti wa Serikali ya Mtaa na Udiwani akiwa Chama Cha Tanzania Labor Party (TLP).
Baada ya kupokelewa na ACT, Fuime alisema, kilichomfanya akikache chama chake ni kile alichodai mambo ya rushwa ndani ya chama (CHADEMA) na kutotendewa haki kwa baadhi ya makada wake.
Fuime aliongeza alijiunga na chama hicho (ACT) ili apate nafasi ya kuwasemea wananchi wanaopitia changamoto mbalimbali pamoja na kuishauri serikali.
"Kwenye mchakato wa uchaguzi lazima haki ndani itendeke, kabla ya kuidai haki ya nje kama ndani utakuwa hutendi haki tutakuwa tunajidanganya wenyewe. Kama unaona chama ulichopo hakina malengo hayo hakuna maana ya kuendelea nacho. Tunaposema rushwa ni adui wa haki kupambana na rushwa ni suala la imani sio tunawasema wengine lakini sisi hatujisemi" alisema Fuime
Alisema kutokana na matukio hayo, alitafakari kwa makini akaona atakuwa anajidanganya akiendelea kusalia CHADEMA.
"Nikajiuliza hivi leo ninaweza kukemea rushwa kama ilivyokuwa mwaka 2015? nisiwe na ukakasi toka moyoni sitakiwi niseme jambo kwa kuwahadaha wananchi wakati hata ndani yetu hatupo vizuri" alisema Fuime
Aliwashukuru ACT Wazalendo kwa kumshawishi na kumpokea ili ajiunge na chama hicho kuendeleza gurudumu la kisiasa.
Alisema kingine ambacho kimemfanya aendelee kuwa ndani ya siasa ni kutoka na shida na mateso wanavyopitia baadhi ya wananchi wanaohitaji kusemewa.
Alisema shida iliyopo wanaopaswa kuwazungumzia na kukemea hali hiyo hawafanyi hivyo.
Awali akizungumza wakati wa kumpokea mgeni huyo, Kiongozi wa Chama hicho, Dorothy Semu alisema watashirikiana naye kuendelea kupigania haki, umoja, utu na demokrasia kwa maslahi ya taifa.
"Tumeamua na kujenga chama cha siasa chenye lengo la kuchochea ujenzi wa taifa lisilo la kinyonyaji kwa kuzingatia misingi ya haki kwa watu wote tunaamni ACT Wazalendo itaendelea kuwa jukwaa sahihi la wanamageuzi wote na walioamua kushiriki katika siasa za kuijenga nchi" alisema Dorothy
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED