Madaktari bingwa 45 watua Musoma kutoa huduma za kibingwa

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 12:31 PM Dec 07 2024
Mafaktari bingwa 45 watua Musoma kutoa huduma za kibingwa
Picha: Mpigapicha Wetu
Mafaktari bingwa 45 watua Musoma kutoa huduma za kibingwa

Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere mjini Musoma, mkoani Mara, imepokea madaktari bingwa 45 watakaoweka kambi maalum ya siku kadhaa na kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi.

 Madaktari hao walipokelewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ambaye aliwataka wananchi kutumia fursa ya uwapo wa madaktari hao kupata matibabu bora.

Kanali Mtambi alitoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezeshwa madaktari hao kuja kutoa huduma kwa wananchi wa mkoa wa Mara, na aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili kufaidika na huduma hizo. Alisema kuwa huduma za madaktari bingwa zimekuwa zikitoa fursa katika mikoa mingine kama Mwanza, lakini sasa huduma hiyo inapatikana kwa urahisi zaidi katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

“Huduma hizi ni za muhimu na tunawashukuru madaktari kwa kujitolea na kutoa huduma hizi bure. Hii ni mara ya tatu kwa mwaka huu madaktari bingwa kuweka kambi mkoani Mara,” alisema Kanali Mtambi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dkt. Osmund Dyegura, alisema kuwa madaktari bingwa wanaohudumu katika kambi hiyo ni kutoka fani mbalimbali, ikiwa ni pamoja na madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake (watano), upasuaji (wanne), watoto (wanne), upasuaji wa mifupa (watatu), pua, masikio na koo (wawili), macho (wawili), mfumo wa mkojo (mmoja), ngozi (mmoja), usingizi (mmoja), kinywa na meno (mmoja), na figo na ini (mmoja).

Dkt. Dyegura alifafanua kuwa kambi za madaktari bingwa zilianza mwaka juzi, zikifanyika awali mkoani Simiyu, na baadaye kuendelea katika mikoa mingine. Kambi hii ni sehemu ya juhudi za kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi na kujenga uwezo wa wataalamu wa afya katika utoaji wa huduma bora.

Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii, Dkt. Zablon Masatu, alieleza furaha ya wataalamu wa afya mkoani Mara kwa ujio wa madaktari hao. Alisema kuwa ujio wa madaktari bingwa utaboresha huduma za afya na kuboresha uwezo wa wataalamu wa afya mkoani humo.

Serikali pia imefanya uwekezaji mkubwa katika vifaa tiba na dawa katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, hatua ambayo itaimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa mkoa wa Mara.