KUSOGEZWA kwa matibabu bure ya Macho kwa wananchi wa Kisiwa cha Pemba kutarahisiha wananchi wa kisiwa hicho kupata huduma hiyo ambayo ni gharama kubwa na hali za kipato chao ni duni hivyo wakati mwingine hushindwa kumudu gharama za matibabu.
Wakizungumza jana na Nipashe baada ya kufika katika zoezi la utoaji wa huduma hizo zinazoendelea kutolewa na taasisi ya Bilali mission Tanzania kwa kushirikiana na taasisi ya Tigo-Zantel kisiwani Pemba,wananchi wa kisiwa hicho walisema kusogezwa kwa huduma hizo ni nafuu kwao.
Khamis Mohamed Ussi mkaazi wa Uweleni kisiwanu humo alisema matibabu hayo yamewafikia muda muafaka kwasabu jamii inakabiliwa na tatizo la ugonjwa wa macho na wengi wao hawana uwezo wa kufuata matibabu hayo maeneo ya mbali kutokana na hali ya unyonge walionao.
Alisema kupata matibabu sahihi na bure imewapa matumaini kwasababu jicho ni kiungo muhimu kinachohitaji matibabu pale kinapogundulika kuwa na tatizo la kiafya.
Alisema bado kuna baadhi ya wanajamii wanasumbuliwa na matatizo ya macho ikiwemo uwoni hafifu au mtoto wa jicho lakini wanaimani potofu huku wakihusisha na masuala za ushirikina.
“Nashukuru sana kusogezwa karibu kwa huduma hii, baada ya kupata taarifa nimefika mapema na kupatiwa matibabu tena bila ya malipo tunaomba huduma kama hizi zije mara kwa mara ili kuokoa maisha yetu hasa sisi wananchi wanyonge”alisema Ussi.
Maryam Issa Haji na Mboje Hamad wakaazi wa Mwambe kisiwani humo, walisema ujio wa madaktari bingwa wa magonjwa ya macho kutawarahisishia kupata tiba sahihi na kuondokana na athari za magonjwa ya macho.
“Wengi wetu tunapoanza kusumbuliwa na tatizo la macho tunatumia dawa za asili kumbe wakati mwingine ndio tunaongeza tatizo bila ya kujuwa hivyo ni vyema nawasihi wananchi wezangu kufika kwa watalamu wa afya kupata tiba sahihi”alisema Mariyam.
Latifa Saleh Ali mawanfunzi wa shule ya Uweleni, alizitaka taasisi zinazotoa msaada wa kimatibabu ya afya kufika shuleni kutoa huduma za afya kwa wananfunzi kwa sababu wapo wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo tatizo la macho ambayo matibabu yake yanahitaji fedha ambazo wazazi wao hawana uweo.
Alisema baadhi ya wananfunzi wanatatizo la uwoni hafifu kunakotokana na matizo mbalimbali hivyo kupata tiba sahihi na kwa wakati kutawafanya kusoma vizuri na kupata matokeo mazuri katika mitihani yao ya taifa.
Mkurugenzi wa tasisi ya ya Bilali Muslim mission of Tanzania Kharu Nbanu Alibhai alisema wanatataria kuwafikia wananchi zaidi 3000 katika kuwapatia huduma za matibabu ya macho na kiasi cha shilingi milioni 70 zitatumika katika zoezi hilo la siku tatu la utoaji wa matibabu bure liloanza juzi katika shule ya Sekondari Uweleni Mkoani Pemba.
Mkurugenzi huyo alisema matibabu hayo ni bure na wananchi watapatiwa miwani,dawa na kufanyiwa upasuaji kwa wale watakaogunduliwa na uhitaji huo baada ya kufanyiwa vipimo hivyo aliwasisitiza wananchi kitumia fursa hiyo.
"Kwa mashirikiano na Tigo zantel tumeamua kuanzisha kambi ya matibabu ya macho ya siku tatu katika kisiwa hiki cha Pemba ili kuwasaidia wananchi wanaosumbuliwa na matatizo ya kiafya ya macho na tumekuja na madaktari bingwa”alisema.
Naye Meneja wa kanda wa taasisi ya Tigo Zantel kisiwani Pemba, Said Massoud Ali, alisema lengo la matibabu hayo ni kuwasaidia wananchi ambao wako mbali na vituo vya kutolea huduma hizo kwa kupatiwa huduma ya upimaji wa macho na kupata ushauri wa kitaalamu.
Alisema kambi kama hizo zinafanyika sehemu mbalimbali hapa Zanzibar Unguja na Pemba na wanaamini Taifa lenye wananchi wenye afya ni Taifa lenye nguvu na linaloweza kupata maendeleo ya haraka.
"Kwa vile macho ni kiungo muhimu sana katika mwili wa binadamu ndio maana tukaamuwa kushirikiana na shirika hili kwa lengo la kuhamasisha wananchi kisiwani Pemba kwa ajili ya kutowa huduma hiyo tena bure ili kuwasaidia wananchi hasa wanyonge",alisema.
Sheha wa shehia ya Uweleni Abdalla Omar Mjawiri, alisema hatua hiyo ya utoaji wa matiabu bure ni yakiungwana na taasisi hizo zimeonesha mapenzi kwa wananchi katika kuwapatia matibabu bure hatua ambayo inaungwa mkono na serikali.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED