WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amesema si jambo zuri kushabikia uhalifu, akiwataka watanzania kuwa makini wasiingie katika mtego ambao maadui zao wanataka waingie wa kuvuruga na kujichukulia hatua mkononi.
Dk. Nchemba alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa kuuaga mwili wa aliyekuwa mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Amani Simbayao aliyepigwa mawe na hadi kupoteza maisha na baadhi ya wananchi wakati akitimiza majukumu yake eneo la Tegeta kwa Ndevu, Dar es Salaam.
"Hili ni jambo baya pamoja na kwamba binadamu yeyote njia yetu ni moja -- ya kuonja umauti, lakini hii njia ya kulazimisha ni jambo baya kwa sababu yoyote ile, ni jambo ambalo halikubaliki nchini! Poleni sana, hili linapaswa kulaaniwa na mtanzania yeyote mpenda mema ya nchi yetu," alisema Dk. Nchemba.
Alisema watumishi hao walijitambulisha kuwa ni maofisa wa TRA, si vitu vizuri kushabikia uhalifu. Hayo si mambo ya kushabikia, hivyo analaani kitendo hicho na kuagiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya watu waliohusika.
"Mwenzetu aliyeshambuliwa kwa mawe alikwenda kufanya jukumu alilotumwa na taifa lake la kukusanya mapato. Amani amekufa kishujaa akitimiza majukumu yake, tuache kufuata mkumbo," alionya Dk. Nchemba.
Pia alisema kitengo cha kupambana na magendo alichokuwa anafanya Amani, na mazingira ya kifo chake, kinatoa ukumbusho kwa maofisa hao kukatiwa bima ili wawe na uhakika kwa sababu ni kitengo kichohusika na kazi ngumu.
Dk. Nchemba alisema anaunga mkono alichokizunguza mkuu wa mkoa cha kuwanunulia hatifungani watoto wa marehemu katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili awasaidie katika maisha yao, mfuko huo uanzishwe na waanze kwa kuchangia Sh. milioni 200.
"Nitawachukua watoto wa marehemu hadi pale haya yote yatakapokamilika ili tuweze kumuenzi shujaa wetu," alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema, "Kuuawa kwa Amani ni hasara, haina mbadala, hatuwezi kusema Amani atapata mbadala kwenye dunia hii, tushapigwa hasara kubwa sana kwa taifa na familia yake.
"Amani amefungua ukurasa mpya kwenye utawala wangu kama Mkuu wa Mkoa na lazima huo ukarasa lazima ujibu na lazima ulete mashahidi… lazima damu iliyomwagika itabeba, lazima eneo lilitokea tukio patasafishwa na nikisema patasafishwa patasafishwaje, sijawahi kuwa kiongozi legelege kwenye mambo ya msingi, siku zote ninabeba uamuzi mzito."
Kamshna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda alisema watumishi wa TRA ambao ni kikosi cha ukusanyaji kodi, watapewa ulinzi wa Jeshi la Polisi ili kuhakikisha usalama wao.
"Kama ambavyo tumekubaliana kuwa hatutatumia nguvu kwenye kusimamia kodi, tutaendelea hivyo lakini kwa kile kitengo cha 'Fast' ambacho kinapambana na walioamua kukwepa kodi, kuanzia sasa hatutawaacha wafanye kazi pekee yao, watafanya wakiwa na polisi," alisema.
Alisema Amani amefariki dunia kwa kushambuliwa kipindi ambacho anatimiza majukumu yake ya kusaidia nchi hii na wananchi wote.
"Alichotendwa hakustahili kutendwa. Sisi tunalaani vikali sana, wale wote waliochukua sheria mkononi kinyume cha sheria hapakuwa na sababu yoyote inayohalalisha kufanya walichofanya, alikuwa anafanya kazi zake kwa mujibu sheria," alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED