NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, amemwandikia Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson barua ya kujiuzulu ubunge.
Kwa barua hiyo ya tarehe 21 Julai mwaka huu, ina maana kwamba Balozi Mbarouk pia amejiuzulu nafasi ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa, Ofisi ya Bunge, Mbarouk ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, amefikia uamuzi huo kutokana na changamoto za kijamii.
"Kwa mujibu wa barua aliyomwandikia Spika, Mheshimiwa Mbarouk amesema amefikia uamuzi huo kufuatia changamoto za kijamii zinazomkabili kwa sasa," sehemu ya taarifa hiyo ya Bunge inasomeka.
Uongozi wa Bunge unanukuu sehemu ya barua ya Balozi Mbarouk, akisema, "Ninalazimika kuchukua uamuzi wa kujiuzulu ili nipate nafasi ya kushughulikia changamoto hizo."
Machi 31, 2021, Rais Samia alifanya uteuzi wa wabunge watatu na kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Balozi Mbarouk akiwa mmoja wa wateule hao.
Balozi Mbarouk amewahi kuwa Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kiislam ya Iran, pia Balozi wa Tanzania Pakstan na Bahrain kuanzia Mei 27, 2013 hadi Novemba 2019.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED