KUTOKANA na kuwapo kwa matukio baadhi ya watu kutapeliwa kwa simu kupitia ujumbe wa ‘tuma kwa namba hii’ Jeshi la Polisi limetoa elimu ya namna ya kukomesha vitendo hivyo.
Kwa miaka kadhaa, kumekuwa na ongezeko la visa vya utapeli kwa simu, ambapo matapeli wengine hujifanya wanatoka makao makuu ya mitandao ya simu ili kuhalalisha uhalifu wao. Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na mtandao wa simu wa Vodacom, limeeleza mbinu madhubuti za kujikinga na vitendo hivyo.
Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Beatrice Charles, amewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za uhalifu mara moja pale unapobainika. Alisisitiza kuwa taarifa hizo zinasaidia kufuatilia na kuwakamata wahusika wa utapeli wa mtandaoni.
Aidha, Beatrice amezihimiza taasisi na kampuni kutunza kwa umakini taarifa za wafanyakazi wao ili kuzuia matapeli kupata fursa ya kuzitumia kwa nia mbaya.
"Watumiaji wa simu wanapaswa kuhakiki taarifa za watu wanaowasiliana nao kwa simu kabla ya kutuma pesa kwa namba yoyote. Kitendo cha kuamini kila ujumbe au simu ni chanzo kikuu cha utapeli."
Vilevile, aliwakumbusha wananchi kwamba kushiriki katika vitendo vya kihalifu ni kosa la jinai na kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
Rona Katuma, Mtaalam wa Uchunguzi wa Udanganyifu wa Kiforensiki kutoka Vodacom, alieleza kuwa idadi ya namba za simu zinazotumika kwa utapeli imepungua sana ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
"Kwa sasa, idadi ya namba za matapeli zinazopiga wateja ni ndogo sana, hazizidi 20 kwa siku, tofauti na ilivyokuwa zamani. Tunashauri wateja kutumia namba ya huduma kwa wateja 100 pekee au kuwasiliana kupitia mitandao yetu ya kijamii kama Instagram kwa msaada zaidi," alisema Katuma.
Vodacom pia imebainisha kuwa wanapokutana na changamoto zinazohusu utapeli wa mtandaoni, wanazishughulikia haraka, na pale inapobidi, huzifikisha kwa Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi.
Inspekta Msaidizi Waziri Makang’ila alisisitiza kuwa utapeli ni kosa la jinai linalokiuka sheria za nchi, na mtu yeyote anayejihusisha na utapeli hatakwepa mkono wa sheria. Alitoa mwito kwa wananchi kuwa macho na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama.
Kampeni hii inalenga kuimarisha uelewa wa umma kuhusu mbinu za matapeli, kusaidia kupunguza visa vya uhalifu, na kulinda wananchi dhidi ya hasara zinazotokana na udanganyifu wa simu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED