MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema kuwa gharama za simu zilishuka kwa asilimia 946 kati ya mwaka 2005 na Septemba mwaka huu.
Aidha, gharama zimeshuka kutoka Sh. 219 kwa dakika mwaka 2005 hadi Sh. 26, Juni 2024 kwenye mtandao wa mtumiaji na kutoka Sh. 292 kwa dakika hadi Sh. 28 mitandao mingine Septemba 2024.
Taarifa iliyotolewa kwa umma na TCRA katika maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru, ilieleza fursa zilizopo kwenye mawasiliano ambazo zimewezesha wananchi kuendesha maisha yao kwa ufanisi kupitia huduma na teknolojia mpya.
Pia, TCRA imesema wananchi wana uhuru zaidi wa kuchagua huduma na kukamilisha miamala kwa gharama nafuu.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari alisema kushuka kwa gharama kati ya mitandao kumewapa watumiaji uhuru wa kupiga simu kwenye mitandao mingine bila kulazimika kuwa na laini za mitandao hiyo.
“Takwimu zinaonesha kuwa kati ya 2019 na 2023 kiwango cha ukuaji wa muda wa maongezi kwenda mitandao mingine kilikuwa mara saba ya kile cha muda ndani ya mtandao wa mtumiaji,” alisema.
Aidha, alisema kushuka huko kumechangiwa na gharama za kuunganisha simu kati ya mitandao kwa dakika, kutoka Sh. 15.6 mwaka 2018 mpaka Sh.1.76 Januari 2024.
“Kukua kwa huduma za simu za mkononi kumewezesha kukua kwa huduma tegemezi, ambazo zimewapa wananchi uhuru zaidi wa kuwasiliana na kufanya miamala mbalimbali,” alisema.
Dk. Bakari alifafanua kuwa kukua kwa akaunti za pesa kwa simu za mkononi, ambazo zimeongezeka kwa asilimia 245 kati ya 2015 na Septemba 2024, na kwamba zilifikia 60,815,533 Septemba, mwaka huu kutoka 17,639,349.
“Huduma za fedha kupitia simu za mkononi zimeleta ufanisi kwa watumiaji na pia zimepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji kwa taasisi,” alisema.
Vilevile, alisema malipo ya kielektroniki yanawezesha mamlaka zinazosimamia mapato kudhibiti mapato ya serikali na sekta ya umma.
“Septemba 2024 kulikuwa na laini za simu 80,662,041 ikilinganishwa na 110,518 mwaka 2000. Kulikuwa na laini 79,646,221 za mawasiliano kati ya watu na 1,015,820 zinazotumika kwa mawasiliano ya mashine zenyewe bila kuingiliwa na binadamu,” alisema.
Aidha, alisema kuongezeka kwa laini za mashine kunaashiria kuenea Tanzania kwa teknolojia za kidijiti zinazojiendesha zenyewe, laini za aina hii zilikuwa 962,928 Juni 2024.
“Simu za mezani zimeongezeka kutoka 16,238 mwaka 1961, ambapo 7,421 au asilimia 54.3 zilikuwa Dar es Salaam pekee, hadi 78,048 Septemba 2024,” alisema.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, ujio wa simu za mkononi na teknolojia mpya umeathiri kuongezeka kwa simu za mezani kwani simu za aina hii zilikuwa 275,591 mwaka 2000.
Aidha, alisema watumiaji wa intaneti waliongezeka kwa asilimia 1,061 kutoka 3,563,732 mwaka 2008 hadi 41,376,545 Septemba 2024.
“Kukua kwa kasi kwa sekta ya mawasiliano kumechangiwa na sera na mipango sahihi; uwekezaji uliofanyika kwenye miundombinu ya huduma, hasa vijijini; usimamizi imara na kuongezeka kwa watoa huduma,” alifafanua.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED