MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) imemuomba Rais Samia Suluhu Hassan aunde Tume Huru ya Kiraia kuhusiana na tukio la utekaji na mauaji wa aliyekuwa Mjumbe wa Sekteterieti wa CHADEMA Ali Kibao.
Mbali na hilo wamemtaka IGP atoe amri kwa Askari wote wa Jeshi la Polisi watumie mavazi rasmi wanapokwenda kukamata mharifu au mtuhumiwa ili watu wengine wanaotumia jeshi hilo vibaya wasipate nafasi hiyo ili Watanzania wabaki salama na huru.
Hayo yamesemwa na Mratibu Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.
Wakili Olengurumwa amesema kuwa kwa mujibu wa katiba Rais ndio mwenye dhamana na mamlaka ya kulinda amani na usalama kwa raia na mali zao kwa kwakuwa ni Taifa la kidemokrasia.
Amesema wamemuomba Rais aunde tume hiyo kwaajili ya kuchunguza kwa kina tukio hilo la mauaji ya Kibao pamoja na matukio yote ya utekaji na mauaji ya nyuma yaliyotokea nchini.
Amesema wanatambua kuwa Rais ana washauri wake ambao wanamshauri lakini na wao kama Watanzania na Watetezi wa haki za binadamu wana wajibu wa kumshauri kwakuwa wao wanajua jamii inataka nini.
“Tunamtaka Rais apokee ushauri wetu ili hata na yeye akae Ikulu kwa amani kuliko kila siku kuna familia zinalia kutokana na matukio ya mauaji na utekeaji” amesema
Aidha walimtaka Rais Samia Suluhu Hassan asikubali hali hii inayoendelea sasa ya matukio ya utekaji katika Taifa lake kwakuwa kwasasa watanzania wamekuwa na hofu na wasiwasi mkubwa kutokana na matukio hayo kushamiri na kufumbiwa macho.
Vilevile aliwataka watanzania kutokukubali kupotezwa kirahisi wafike mahali wawe na uwezo wa kuteteana wenyewe kwa wenyewe katika majanga na wasikubali kuchukuliwa kiholela kutoka sehemu moja kwenda nyingine kinyume na utaratibu kama alivyofanyiwa marehemu Ali Kibao kwa kuchukuliwa bila taratibu za kisheria kwa kutolewa ndani ya gari huku abiria wengmamine wanashindwa kumtetea mtanzania mwenzao.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED