MTOTO Joshua Tarimo (11) ametoweka nyumbani kwa mlezi wake Tandale Kwatumbo, Dar es Salaam tangu Desemba 5, mwaka huu.
Mlezi wa mtoto huyo, Salama Salimu, akizungumza na Nipashe jana alidai kuwa mwanawe huyo alitoweka Desemba 5 mwaka huu asubuhi.
"Niliangalia fedha zangu mahali ninapoweka sikuziona. Baada ya kufuatilia kwa kina, nilihisi mwanangu ndiye kazichukua, nilimwuliza mwanangu aitwaye Asma Mohamed (21) na Joshua.
"Katika kuwahoji ilibainika Joshua ndiye kazichukua fedha hizo na kumtaka azirudishe, ndipo aliamua kuondoka kwenda kusikojulikana kwa kuhofia kupewa adhabu.
"Saa chache ndipo nilipogundua kuwa Joshua hayupo nyumbani, nilimtafuta sikumpata ndipo nilipochukua jukumu la kumwambia mama yake.
"Nilipojaribu kumwuliza mama yake, alisema mtoto huyo hakuwa kwake, tulimtafuta kwa ndugu wa karibu, lakini hatukumpata," alisema.
Salama alisema wameshatoa taarifa kituo cha polisi na kufungua faili namba MBT/RB/6328/2024.
"Ninaogopa sana huyu mwanangu asikumbwe na jambo baya, kwa sasa kuna matukio ya watu kupotea na kutekwa, nina hofu sana, kokote aliko arudi nyumbani," alisema.
Alisema kuwa siku hiyo alikuwa amevaa fulana ya rangi ya chungwa na suruali ya rangi ya kijivu na yeboyebo za rangi ya kijani. Atakayemwona awasiliane na mama huyo kwa namba 0684304142 au 0719058662.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED