ILI kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu pamoja na malengo mengine ambayo nchi imejiwekea, ni lazima kufanyike uwekezaji mkubwa katika miradi ya kimkakati katika sekta mbalimbali kama nishati, afya, elimu, maji na kilimo na rasilimali watu.
Hata hivyo, serikali za nchi zinazoendelea zina changamoto/uwezo mdogo wa kukusanya mapato ya ndani yanayotosheleza kuendesha nchi. Hivyo basi, inazilazimu nchi/serikali kukopa na kuingia kwenye madeni ili kupata fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati itakayochechemua uchumi na kuleta maendeleo. Hapo ndipo wananchi wanapoanza kusikia kuhusu Deni la Taifa au Deni la Serikali.
Deni la Taifa au Deni la Serikali ni deni ambalo lilikopwa na serikali kutoka katika vyanzo mbalimbali ndani na nje ya nchi na ambalo linapaswa kulipwa.
Madeni mara nyingi hutokana na hali ya mtu binafsi, familia au serikali kulazimika kukopa kwa sababu ya kuwa na bajeti ya matumizi ambayo ni kubwa kuliko mapato yanayotarajiwa kupatikana katika kufanikisha shughuli zilizopangwa kutekelezwa kwa kipindi husika.
Kwa lugha ya kihasibu, makisio/matarajio ya matumizi yanapozidi makisio/matarajio ya mapato, yanasababisha kuwapo nakisi/upungufu kwenye bajeti iliyotayarishwa.
Taasisi ya Kifedha (Corporate Finance Institute) inaeleza kuwa Deni la Taifa ni jumla ya madeni yote ambayo serikali au nchi inadaiwa. Mara nyingi madeni haya hutokana na hati fungani (bonds) pamoja na dhamana zingine za madeni, lakini pia Deni la Taifa hutokana na kukopa moja kwa moja kutoka katika taasisi za kifedha za kimataifa kama vile Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) au nchi zilizoendelea.
Deni la Taifa ni njia mojawapo ya upatikanaji fedha za kujazia nakisi iliyojitokeza kwenye uandaaji bajeti ya taifa ya mwaka husika.
Utaratibu huu unatumika na unakubalika kwenye serikali zote duniani. Serikali zote duniani huwa zinajitahidi kuwa na uwiano wa mapato na matumizi katika kuandaa bajeti zao. Ili ziweze kutimiza azma hii, serikali nyingi zinalazimika kukopa kwa madhumuni ya kuleta uwiano wa mapato na matumizi ya kipindi husika.
Mikopo ya serikali nyingi inapatikana ama kutoka serikali nyingine au taasisi za fedha na benki. Benki zinazotoa mikopo zipo za aina mbalimbali, zikiwamo benki za biashara ambazo riba zake ni kubwa na masharti yake ya kukopa ni magumu zaidi ya benki nyingine.
AINA YA MIKOPO
Mikopo inayochukuliwa na serikali inaweza kuwa yenye masharti nafuu ya riba na dhamana au yenye masharti magumu ya riba na dhamana; pia inaweza kuwa ya muda mfupi au ya muda mrefu wa kulipwa.
Kwa kuwa mara nyingi mikopo ya aina hii ni ya kulipia gharama za miradi ya maendeleo (miradi ya kimkakati) ambayo huchukua muda mrefu kukamilika, inashauriwa aina ya mikopo inayochukuliwa kugharamia miradi hii iwe ya masharti nafuu ya riba (concessionary loans) na iwe ya muda mrefu wa kulipa (long term loans).
Vilevile, inashauriwa kuwa mikataba ya mikopo ya maendeleo iweke uwezekano wa kubadilisha masharti ya awali ya mikopo wakati wa utekelezaji miradi mikubwa ya maendeleo ili yaendane na uhalisia wa hali ilivyo kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia.
Kutekelezwa kwa miradi ya kimkakati nchini husababisha ongezeko la ajira kwa wananchi; huongeza mzunguko wa fedha katika uchumi wa nchi; huimarisha miundombinu ya nchi na kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara; huboresha huduma zitolewazo kwa wananchi na huchochea kasi ya maendeleo ya nchi.
Mikopo ya aina hii mara nyingi hulenga katika kukuza uchumi wa nchi mara baada ya miradi ya kimkakati iliyolipiwa na fedha za mikopo hiyo kukamilika na kuanza kuzalisha bidhaa au huduma.
Deni la Taifa huhusisha madeni ya nje ya nchi na madeni ya ndani ya nchi. Nchi nyingi zinazoendelea hukopa nje aidha kwa mataifa rafiki wa nchi hizo au benki za nje zilizojizatiti kwenye kukopesha nchi zinazoendelea, zikiwamo WB, IMF, Benki ya Maendeleo ya Afrika na Benki ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mikopo ya ndani ya nchi mara nyingi hukopwa na serikali kutoka Benki Kuu ya nchi, mifuko ya hifadhi ya jamii na benki za biashara za ndani ya nchi.
Aina nyingine ya mikopo ya ndani ya serikali ni pale ambapo serikali inapopata huduma ambayo haijalipiwa ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha wa serikali. Deni hilo linaweza kuwa ni la watumishi ambao hawajalipwa stahili zao ilipofika mwisho wa mwaka wa fedha wa serikali au madai ya makandarasi ambao wametoa huduma kwa serikali kwa makubaliano ya kulipwa lakini wanakuwa hawajalipwa mpaka mwaka wa serikali unapokuwa umeisha kutokana na serikali kutokuwa na fedha za kutosha kulipia madeni yake mwisho wa mwaka.
UKUAJI WA DENI LA TAIFA
Ukuaji wa Deni la Taifa unapaswa uendane na ukuaji wa uchumi wa nchi ili deni hilo liwe himilivu. Wakati Benjamin William Mkapa, Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa anamaliza muda wake mwishoni mwa mwaka 2005, Deni la Taifa lilikuwa Sh. trillioni 10.93 wakati uchumi wa taifa ukiwa na thamani ya Sh. trilioni 21.4 (Dola za Marekani bilioni 18.4).
Vivyo hivyo, wakati Rais wa Nne, Dk. Jakaya Kikwete alipokuwa anamaliza muda wake mwaka 2015, Deni la Taifa lilikuwa Sh. trilioni 41.82 wakati uchumi wa taifa ukiwa Sh. trlioni 84.28. Hii inaonesha kuwa, katika kipindi cha Dk. Kikwete, Deni la Taifa liliongezeka kwa asilimia 282.6 (zaidi ya mara mbili na nusu) kulinganisha na deni lililoachwa na Rais Mkapa.
Vilevile, Pato la Taifa lilikua kwa Sh. trilioni 62.88 sawa na asilimia 293.8 kutoka Sh. trlioni 21.44 hadi kufikia Sh. trilioni 84.28.
Katika kipindi cha Rais wa Tano, Dk. John Magufuli, Deni la Taifa liliongezeka hadi Sh. trilioni 72.3 kufikia mwezi Machi 2021 ikiwa ni ongezeko la Sh. 39 trilioni sawa na asilimia 72.8. Deni la Taifa lilikuwa ni asilimia 53.3 ya Pato la Taifa la Sh. trilioni 135.5 mwaka 2021.
Aidha, Deni la Taifa limefikia Sh. trilioni 111.3 mwezi Juni 2024. Ni ongezeko la Sh. trilioni 28.7 sawa na asilimia 54, ambapo uchumi wa taifa unatarajiwa kuwa wa thamani ya Sh. trilioni 230.91.
Ripoti ya Benki ya Dunia, "The World Bank Economic Report on Tanzania 2023", imetoa taarifa njema ya ukuaji uchumi wa nchi wa asilimia 5.2 kulinganishwa na ukuaji uchumi wa nchi mwaka 2022 wa asilimia 4.6.
Mbali na kuwapo ukuaji wa kuridhisha wa uchumi wa nchi, bado hali ya umaskini nchini haijapungua kwa kasi ya kuridhisha kutokana na kasi ya ongezeka la watu kwa kiwango cha asilimia tatu.
UHIMILIVU WA DENI LA TAIFA
Kabla mkopeshaji yeyote -- awe ni nchi, benki au mtu binafsi hajafanya uamuzi wa kukopesha fedha kwa mkopaji yeyote awe ni nchi, taasisi au mtu binafsi, ni lazima mkopeshaji awe na vigezo vya kumhakikishia kuwa mkopo atakaotolewa, utarejeshwa na mkopaji.
Vilevile, mkopaji naye anapaswa kuwa na uhakika wa kuwa na uwezo wa kurejesha mkopo anaotarajia kuuchukua kwa kuwa deni ni lazima lirejeshwe na mkopaji kwa aliyemkopesha.
Hivyo, nchi inapotaka kukopa huwa inafanyiwa tathmini ya uwezo wake wa kulipa mkopo unaoombwa ili mkopeshaji ajiridhishe kuhusu uwezo wa mkopaji kurejesha deni lililochukuliwa.
Vivyo hivyo, mkopaji naye anapaswa kujifanyia tathmini ya uwezo wake wa kulibeba deni analotarajia kulikopa na kujihakikishia kuwa ataweza kuwa na uwezo wa kulilipa deni hilo mara litakapoiva.
Kwa mfano, kwenye hotuba ya bajeti ya mwaka 2024/25, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba (Mb), alisema kuwa kwa mujibu wa tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Desemba 2023, Deni la Taifa bado ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.
"Katika tathmini hiyo, viashiria vinaonesha kuwa kwa mwaka 2023/24; uwiano wa Deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 35.6 kulinganisha na ukomo wa asilimia 55; uwiano wa deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 19 kulinganisha na ukomo wa asilimia 40; na uwiano wa deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 113.2 kulinganisha na ukomo wa asilimia 180," alisema Dk. Mwigulu.
Waziri huyo aliongeza kuwa hadi kufikia mwezi Machi 2024, Deni la Taifa lilikuwa Sh. trilioni 91.7. Kati ya kiasi hicho, deni la nje lilikuwa Sh. trilioni 60.95 na deni la ndani lilikuwa Sh. trilioni 30.75. Deni hili lilikuwa limeongezeka kwa Sh. trilioni 19.4 sawa na asilimia 26.8 ya deni lililoachwa na Rais wa Tano.
VIGEZO KUTATHMINI DENI LA TAIFA
Benki ya Dunia (WB) hutumia Mfumo wa Uhimilivu wa Madeni (Debt Sustainability Factors – DSF) kufanya tathmini ya hatari za uhimilivu wa deni katika nchi zinazoendelea (Developing Countries). Vigezo vinavyotumiwa na WB katika kutathmini uhimilivu wa Deni la Taifa ni pamoja na:
Kwanza; Uainishaji Uwezo wa Kubeba Deni (Debt-Carrying Capacity Classification) – Nchi zinaanishwa kulingana na uwezo wao wa kubeba madeni uliotathminiwa ambao husaidia kubainisha uwezo wa nchi wa kusimamia na kulipa madeni yao kwa ufanisi.
Pili; Viashiria vya Viwango vya Mzigo wa Deni (Threshold Levels for Debt Burden Indicators) – WB huweka viashiria vya viwango vya juu vilivyochaguliwa vya upimaji wa mzigo wa deni kwa nchi husika kama vile uwiano wa Deni la Taifa kwa Pato la Taifa ili kujihakikishia uwezo wa nchi zinazokopa kuwa na uwezo wa kiuchumi kulipa madeni husika.
Tatu; makadirio ya msingi na matukio ya Jaribio la Mfadhaiko (Baseline Projections and Stress Test Scernarios) – Kigezo hiki kinapima namna gani nchi itaweza kustahimili mishtuko ya kiuchumi ya nje na ndani katika kulisimamia deni la nchi vizuri na kuweza kulilipa deni hilo mara litakapoiva.
Nne: Ukadiriaji vihatarishi vya dhiki ya deni (Risk Ratings of Debt Distress) – kwa kuchanganya kanuni elekezi na uamuzi wa wafanyakazi. Benki ya Dunia inazipanga nchi kulingana na viwango vya vihatarishi vinavyoweza kuathiri usimamizi mzuri wa ulipaji madeni ya taifa.
Tano: Ishara za Vihatarishi vya Kiufundi (Mechanical Risk Signals) – Kielezo cha DSF huzalisha mawimbi ya vihatarishi vya kiufundi kulingana na ulinganisho wa viashiria vya deni vya chini ya hali ya msingi na mkazo na vizingiti vinavyohusika kusaidia katika kubainisha viwango vya hatari vya dhiki ya deni la nje na la jumla la taifa.
Sita; Uchambuzi wa Mwaka wa Uhimilivu wa Deni (Annual Debt Sustainability Analysis (DSA)) – Benki ya Dunia huhitaji kila nchi mdeni wake kufanya uchambuzi wa uhimilivu wa madeni ya nchi zinazoendelea kila mwaka ukionesha hali halisi ya uhimilivu wa madeni ya nchi. Takwa hili la Benki ya Dunia huzipa nchi zilizokopa fursa ya kujifanyia tathmini zenyewe ili kujiridhisha kuhusu uwezo wao wa kuhudumia madeni waliyonayo na kujitathmini kama wana uwezo wa kuendelea kukopa.
Saba; Mwongozo wa Uamuzi wa Ukopaji na Ukopeshaji (Guidance for Borrowing and Lending Decisions) - Benki ya Dunia ina miongozo inayoongoza mkopeshaji kumfanyia mkopaji tathmini ya uwezo wake wa kukopa na miongozo inayomwongoza mkopaji kujifanyia tathmini ya uwezo wa kubeba na kulilipa deni analofikiria kukopa.
NCHI BADO INA NAFASI KUKOPA
Kwa kutumia vigezo vya kupima uhimilivu wa Deni la Taifa, Deni la Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bado ni himilivu kama alivyotamka Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu katika hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2024/25.
Deni hili ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu, hivyo serikali ipo kwenye hali nzuri ya kuendelea kukopa endapo kutatokea ulazima wa nchi kukopa.
Watanzania hatuna sababu ya kuogopa kukopa kwa ajili ya kuboresha miundombinu na huduma kwa wananchi na kuchochea kasi ya maendeleo ya nchi yetu.
JUKUMU LA WANANCHI
Kwa kuwa wananchi ndio wamiliki wa uchumi wa nchi kulingana na matakwa ya Katiba ya nchi ya mwaka 1977 (kama ilivyorekebishwa mara kwa mara) Ibara ya 8(1)(a) inayosomeka, "Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii", ni lazima wananchi wawe na wajibu wa kuhakikisha mikopo inayochukuliwa na serikali itatumika kwa maendeleo ya nchi.
Wananchi wana haki ya kujua madhumuni ya mikopo inayochukuliwa na serikali na wana haki ya kijihakikishia kuwa mikopo inayochukuliwa na serikali inatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa na si vinginevyo.
Watanzania wengi walipongeza serikali chini ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uwazi na uwajibikaji wa hali ya juu uliooneshwa kwenye mkopo wa kukabiliana na athari za UVIKO-19 wa Sh. trilioni 1.3 uliochukuliwa na serikali kwa shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.
Uwazi na uwajibikaji wa aina hii ni mzuri na ni dalili za uimarikaji uwajibikaji na utawala bora nchini ambao unasisitizwa uendelezwe kwenye mikopo ijayo.
Ili kuimarisha uwajibikaji katika ukopaji wa serikali na kuongeza uwazi katika usimamizi wa Deni la Taifa, WAJIBU (taasisi anayoongoza hivi sasa) inashauri serikali kuweka wazi kwa wananchi nia yake ya kukopa, vyanzo vya mikopo, masharti ya mikopo pamoja na matumizi ya fedha za mikopo ili wananchi waweze kutambua mchango wa Deni la Taifa katika maendeleo ya taifa.
Hili linaweza kufanyika kwa kufanya mapitio ya Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, SURA 134.
*Mwandishi wa uchambuzi huu ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu. Hivi sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya WAJIBU.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED