Wadaiwa kuondolewa vituo vya maboresho ya Daftari la Wapigakura wakachimbe vyoo

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 11:02 AM Sep 10 2024
Wadaiwa kuondolewa vituo vya maboresho ya Daftari la Wapigakura wakachimbe vyoo
Picha:Mtandao
Wadaiwa kuondolewa vituo vya maboresho ya Daftari la Wapigakura wakachimbe vyoo

BAADHI ya wananchi katika Kata ya Mwandoya, Jimbo la Kisesa, wilayani Meatu, mkoani Simiyu wamedai kuondolewa katika vituo vya kujiandisha na kuboresha taarifa za Daftari la Kudumu la Mpigakura.

Wanadai hatua hiyo ni sehemu ya operesheni ya kutekeleza uchimbaji vyoo kwa kila kaya ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu. 

Hata hivyo, hatua hiyo inatajwa kuingilia na kukwaza maboresho ya daftari hilo yalioanza Septemba 3 mwaka huu, yakitarajiwa kuhitimishwa leo Septemba 10, hali inayodaiwa kusababisha wananchi kukimbia makazi yao, msako ukifanywa na mgambo kwa kushirikiana na Idara ya Afya.

Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Mwandoya, Luhende Gamanija alisema msako huo ulianza Septemba 8 wakati maboresho ya daftari hilo yakielekea ukingoni na kuwa watu walianza kutafutwa kwenye makazi na maeneo wanakojiandisha na kupigwa faini huku wengine wakichukuliwa kwenda kuchimba vyoo.

"Hivi karibuni kuliripotiwa mlipuko wa ugonjwa wa kuhara na kutapika katika maeneo yetu, hivyo kuhusishwa na kipindupindu kutokana na watu wengi kutokuwa na vyoo, hivyo hujisaidia vichakani.

"Lakini hakukuwa na operesheni ya namna hii, juzi tu wakati tunaendelea na maboresho wameanzisha opereshini ya kuchukua watu wakachimbe vyoo kwenye makazi yao huku wengine wanaokutwa hawana vyoo wakitozwa faini kuanzia Sh. 50,000 hadi 300,00 ambazo hazitolewi risiti," alisema. 

Alisema kuwa kufuatia hatua hiyo, watu wamekimbia makazi yao na kuacha shughuli za kujiandisha, akiwaomba viongozi kuingilia kati suala hilo ili kutokupoteza haki za watu kushiriki kikamilifu katika uchaguzi.

Akizungumza na Nipashe, Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina, alithibitisha kupokea taarifa hizo na kueleza kuwa, kwa wakati huo alikuwa safarini, hivyo kulazimika kurejea jimboni kuona namna ya kumaliza tatizo hilo.

"Kwa sasa namtafuta Mkuu wa Wilaya ili tujue namna ya kulifanyia kazi na wakati huu ninaelekea jimboni, tunaendelea kuwasiliana ili kama kuna operesheni isitishwe, tuendelee na maboresho ya daftari la kudumu la mpigakura," alisema Mpina.

Mratibu wa Tume Huru ya Uchaguzi Mkoa wa Simiyu, Pius Ngaiza akizungumza na Nipashe alieleza kutokupokea taarifa hizo za watu kuondolewa katika vituo vya kujiandisha na kuahidi kufuatilia katika eneo hilo na kulipatia ufumbuzi.

"Mwenyewe taarifa hizi ninazipata kutoka kwako, hivyo hapa ndiyo unanieleza na mimi ninaanza ufuatiliaji kwa watu walioko katika eneo hilo husika," alisema Ngaiza.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Fauzia Ngatumbura pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi walipotafutwa na mwandishi wa habari hii kwa njia ya simu, ili kutoa ufafanuzi kuhusu operesheni hiyo, simu zao ziliita pasi na kupokewa na wakati mwingine zilikatwa.