NDUGU wa familia wakiwamo wajomba wametajwa kuwa chanzo cha ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto.
Pia ndugu hao wamekuwa wakiwalawiti watoto ambao asilimia kubwa ni wanafunzi kisha kuyamaliza kiundugu, hali inayosababisha watoto kuathirika kisaikolojia, kushindwa kusoma ipasavyo na kutokutimiza ndoto zao za kielimu.
Hayo yamebainishwa juzi na Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Robert Kwela wakati akitoa taarifa ya hali ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye jamii na familia.
Alisema hali hiyo imebainika kutokana na utafiti walioufanya ambako walibaini wajomba kuwaingilia kwa nguvu kingono watoto wa dada zao, endapo wakibainika wanamaliza kimya kimya.
Kwela alisema wameshaweka mifumo rafiki ya kutoa taarifa ya vitendo hivyo kwa lengo la kusaidia kundi la watoto wasiendelee kufanyiwa vitendo viovu ambavyo vinasababisha kuchukia makazi yao na kukimbilia mjini kutafuta maisha wakiwa na umri mdogo, huku wanandugu watakaobainika wanawachukulia hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
“Ukatili unasababisha kuwa na ongezeko la watoto wengi wa mitaani, kwa ripoti ya Novemba mwaka huu inaonesha watoto nje ya ndoa 132 wamefanyiwa ukatili, huku walipo ndani ya ndoa wakiwa 148, watoto waliobakwa ni 60 watu wazima 16 na hakuna ushirikiano wowote zinapofika katika vyombo vya sheria huku zaidi ya watoto 36,564 wakikimbilia mitaani,” alisema Kwela.
Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Kahama, Salumu Rashidi, alikiri kuwepo kwa wimbi la watoto wa mitaani kutoka Burundi na wengi wanafanyishwa kazi za ndani na biashara ndogo ndogo na kinamama.
Hivyo, aliwataka kuacha tabia hiyo kwani sheria inakataza mtoto chini ya miaka 18 kupewa majukumu ya kazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, aliwasihi wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa na kuwaibua waathirika wa ukatili ili wahusika wachukulie hatua za kisheria na kesi zinapofika mahakamani wajitokeze kutoa ushahidi na siyo kumalizana kimya kimya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED