Wakurugenzi, mifuko hifadhi ya jamii walalamikiwa ufujaji mali

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 08:58 AM May 28 2024
Kamishna wa tume hiyo, Jaji mstaafu Sivangilwa Mwangesi.
Picha: Maktaba
Kamishna wa tume hiyo, Jaji mstaafu Sivangilwa Mwangesi.

RIPOTI ya Sekretarieti ya Maadili kwa Viongozi wa Umma imeonesha wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, manispaa, miji na majiji wanaongoza kwa kulalamikiwa kutumia vibaya madaraka na rasilimali za umma.

Iliwasilishwa mwishoni mwa wiki kwa wahariri wa vyombo vya habari na Kamishna wa tume hiyo, Jaji mstaafu Sivangilwa Mwangesi, ikionesha kundi hilo linafuatwa na kundi la watendaji wakuu wa taasisi na mameneja.

Alisema kuna ongezeko la malalamiko ya watendaji wakuu wa taasisi na mameneja kwa asilimia 100 kutokana na ucheleweshaji utoaji huduma kwa wakati hasa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii.

"Mathalani, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita wastani wa uwasilishaji malalamiko kwa mwezi uliongezeka kutoka malalamiko 16 mwaka 2021/22 hadi malalamiko 18 kwa mwaka wa 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 13 na ongezeko hili la malalamiko limesababishwa na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi baada ya kupata elimu," alisema.

Jaji mstaafu Mwangesi alisema kulinganisha malalamiko yaliyotolewa kwa mihimili mitatu, bado taasisi zilizo chini ya serikali zinaongoza kwa kulalamikiwa zaidi zikifuatwa na mahakama na Bunge.

Kuhusu wizara, alisema Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), hasa viongozi walioko katika mamlaka za serikali za mitaa (halmashauri) inaongoza kwa kulalamikiwa zaidi na wananchi.

"Katika mwaka wa 2022/23 viongozi walioko TAMISEMI bila kujali kuwa wanawajibika kwa Sheria ya Maadili, viongozi wanaolalamikiwa waliongezeka kwa asilimia 19 kulinganishwa na mwaka 2021/22, kimsingi bado TAMISEMI imeendelea kuwa na malalamiko mengi,” alisema.

Jaji mstaafu Mwangesi alisema kuwa kwa mwaka 2021/22, Ofisi ya Rais - TAMISEMI kulikuwa na malalamiko 63, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (7), mahakama (5), Wizara yenye dhamana ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana (6), Wizara ya Mambo ya Ndani (12) na Wizara ya Fedha (10).

Alibainisha kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii ilikuwa na malalamiko manne (4), Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (4), Wizara ya Afya (3) na Bunge (6), hivyo kuwa na jumla ya malalamiko 120.

Alisema kwa mwaka 2022/23, TAMISEMI kulikuwa na malalamiko (93), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (16), mahakama (15), Wizara ya Mambo ya Ndani (15) na Wizara ya Fedha (11).

Alisema Wizara yenye dhamana ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana ilikuwa na malalamiko manane (8), Wizara ya Afya (8), Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (7), Wizara ya Maliasili na Utalii (4) na Bunge (2), hivyo kuwa na jumla ya malalamiko 179.