UBALOZI wa China kwa kushirikiana na Kampuni ya Oryx Gas Tanzania wametoa mitungi 800 ya gesi na majiko yake kwa watumishi wa serikali mkoani Arusha, ikiwa ni muendelezo wa jitihada za kuiunga mkono setikali katika kampeni ya kuihamashisha jamii kutumia nishati safi.
Miongoni mwa waliopatiwa mitungi pamoja na majiko ni madereva, walimu, wahudumu wengine wa serikali, pamoja na waandishi wa habari.
Akizungumza leo mkoani Arusha wakati wa hafla ya ugawaji mitungi hiyo Balozi wa China nchini Chen Mingjian, amesema serikali yake inaunga mkono juhudi za Tanzania za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira na uoto wa asili.
Amesema Tanzania ni nchi rafiki wa mazingira na inazingatia uhifadhi wa Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, na kwamba kwa muda wa miaka mitatu amefanya kazi hapa nchini na ameshuhudia juhudi za ajabu ambazo zimefanywa na serikali katika nyanja ya utunzaji wa mazingira.
"Mitungi hii ya gesi sio tu itaboresha maisha ya watumishi bali pia itapanda mbegu za ulinzi wa mazingira katika mioyo ya jamii. Rais Xi Jinping wa China mara nyingi husema maji ya bahari na milima mirefu ni mali ya thamani sana.
"Kama nchi zinazoendelea zinazowajibika, China na Tanzania zote zimekataa kukubali na kukataa kufuata njia ya zamani ya uchafuzi wa mazingira. Badala yake, tumechagua njia mpya ya kipaumbele cha kiikolojia na maendeleo ya kijani," amesema.
Ameongeza kuwa wakati wakiendeleza kwa nguvu mazingira, kwa njia ya uchumi na kuboresha maisha ya watu, pia wamechukua jukumu muhimu la kulinda mazingira.
Amesema Mei mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alipendekeza mkakati wa nishati safi ya kupikia ambao unadhihirisha kikamilifu falsafa ya serikali ya Tanzania ya kujali wananchi wake kwanza na kuishi kwa usawa kati ya mwanadamu na maliasili.
"China na Tanzania ni kaka na dada, pia washirika wazuri. Daima tunasaidiana. Mwezi uliopita, Jukwaa la Ushirikiano wa China na Afrika lilifanya mkutano huko mjini Beijing.
"Wakuu wa nchi, serikali na wajumbe kutoka nchi 53 akiwemo Rais Samia walikusanyika Beijing kushiriki, nami nilifuatana na ujumbe wa Rais katika tukio hilo muhimu," amesema.
Aidha, amesema Rais Xi Jinping alitoa hotuba muhimu, na Rais Samia naye aliiwakilisha Afrika Mashariki, akitoa hotuba kwenye hafla ya ufunguzi, na kwamba alitangaza hatua za ushirikiano kati ya China na Afrika.
Amesema katika ushirikiano wa Maendeleo ya Kijani, zilipendekeza kuwa China inapenda kutekeleza miradi 30 ya nishati safi katika bara la Afrika ili kuzisaidia nchi za Afrika kufikia maendeleo ya kijani kibichi.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania, Benoit Araman, amesema kuanzia Julai 2021, upatikanaji wa suluhisho la kupika imekuwa mada ya umuhimu mkubwa, chini ya uongozi wa Rais Samia, akiahidi kuwa wako pamoja kuunga mkono utekelezaji wa programu ya kuhamashisha matumizi ya nishati safi.
Amesema programu ya nishati safi ya kupikia itachukua miaka 10 kuwezesha upatikanaji wake kwa ajili ya kupikia kwa angalau asilimia 80 ya Watanzania ifikapo mwaka 2034. Hivyo kuna haja ya kuungana kufanikisha juhudi hizo.
“Ukizungumza kuhusu nishati safi ya kupikia kwa wanafunzi wenu na katika mikutano na wazazi itachangia kwa kiasi kikubwa kueneza falsafa ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania.
"Ninyi kuwa watumiaji wa Oryx Gas itasaidia idadi ya watu kuona manufaa ya kupika kwa kutumia gesi. Naushukuru Ubalozi wa China nchini Tanzania, kwa ushirikiano wao, ambao umeruhusu makabidhiano ya mitungi ya gesi na majiko yake 800," amesema.
Naye, Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo Oryx Gas Tanzania, amesema Oryx Gas imekuwa Kampuni ya kwanza kwa Arusha kuonesha dhamira ya dhati ya kuunga mkono kampeni ya Rais Samia na wamekuwa mstari wa mbele katika kampeni hiyo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED