Biashara chuma chakavu imejaa hujuma, hatari ya miundombinu

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 09:28 AM Nov 08 2024
news
Mchoraji: Msamba
Katuni.

BIASHARA ya vyuma chakavu imeenea karibu kila kona ya nchi, watu wanajitafutia riziki kwa kutafuta vyuma hivyo, kuvikusanya na kwenda kuviuza ili wajipatie fedha kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.

  Hata hivyo, ninadhani biashara hiyo inapaswa kumulikwa, kwani baadhi ya watu wanaokusanya vyuma hivyo chakavu, wanaharibu na kuiba  miundombinu mbalimbali ikiwamo ya barabara.
 
 Kwa mfano, unaweza kukuta pembeni mwa kingo za madaraja kumefungwa vyuma, lakini baadhi ya watu wamekuwa wakituhumiwa kujihusisha kuvifungua na kwenda kuviuza kama chuma chakavu.
 
 Wakati vyuma hivyo viking'olewa, wengine wanachukua mifuniko ya chemba za maji ya mvua na kwenda kuiuza kama chuma chakavu, kitendo ambacho ni wazi kuwa ni hujuma.
 
 Biashara ya ukusanyaji, usafirishaji, uhifadhi na urejelezaji wa chuma chakavu si mbaya, kwani kwa namna moja au nyingine unasaidia kutunza mazingira, lakini inapofikia kuharibu miundombinu, ninadhani unageuka kuwa hujuma, hivyo wenye mchezo huo wangemulikwa.
 
 Ni vyema wanaofanya biashara ya chuma chakavu wasiwe chanzo cha uharibifu wa miundombinu ya barabara na maeneo mengine, kwani uharibifu huo sasa umesababisha kusiwapo mifuniko ya chuma kwenye chemba za maji ya mvua katika baadhi ya maeneo.
 
 Limekuwa jambo la kawaida kukuta mfuniko umeondolewa na badala yake limewekwa gurudumu au matawi ya miti kama ishara ya kuwatambulisha madereva kuwa kuna shimo mbele.
 
 Hujuma za aina hiyo, ninadhani ndizo zimesababisha hata mkandarasi anayepanua Barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Ubungo, Dar es Salaam kuamua kuweka mifuniko ya zege kwenye chemba mpya.
 
 Ninadhani ni wakati sasa wafanyabiashara wa chuma chakavu kuwa waaminifu na kuepuka kujihusisha kuhujumu miundombinu. Wafanye kazi na serikali kwa kuwafichua wanaoharibu miundombinu na kuiuza kama chuma chakavu, kwani kitendo hicho ni sawa na uhujumu uchumi.
 
 Binafsi ninaamini kwamba mtu akifanya biashara yake kwa kufuata taratibu, hawezi kujihusisha na hujuma. Hivyo, hata wanaokusanya chuma chakavu kutoka kwa watu mbalimbali, wangekuwa makini.
 
 Katika maisha ya sasa, kuna baadhi ya watu wapo tayari kufanya hujuma ili wajipatie fedha, wafanyabiashara wanatakiwa kuwa makini na watu wa aina hiyo ili wasiwaingize katika mtego.
 
 Biashara hiyo imeongeza ajira kwa baadhi ya vijana wanaopita mitaani na kuokota vyuma hivyo, lakini inawezekana wapo baadhi ambao  wanajihusisha na wizi wa miundombinu na kuiuza kama chuma chakavu.
 
 Kwa hiyo, wafanyabiashara wa chuma chakavu wangejihadhari na ununuzi wa vyuma vinatokana na miundombinu ya serikali, kwani wanaowapa vyuma hivyo wapo tayari kufanya hujuma wapate fedha.
 
 Yapo baadhi ya maeneo, wameiba hadi vibati vya anuani za makazi na kwenda kuiuza kama chuma chakavu. Yote hayo ni hujuma na kuharibu kodi za wananchi zilizotumika kutengeneza vibati hivyo.
 
 Inasikitisha kuona ujenzi wa barabara umekamilika na miundombinu yake, lakini baada ya muda mfupi, mifuniko ya chemba za maji ya mvua haipo au vyuma vya kingo za barabara vimeng'olewa.
 
 Huo sio uzalendo. Kama tunashindwa kulinda miundombinu yetu tunataka aje nani atulindie? Hapa kuna tatizo la ukosefu wa uzalendo kwa kushindwa kulinda na kuthamini vitu vyetu.
 
 Tutafakari kisha tuchukue hatua, kwani hakuna mtu kutoka nje atakayekuja kulindia miundombinu bali ni sisi Watanzania wenyewe, ingawa wengine huwa wanasema hiyo ni mali ya umma au haina mwenyewe.
 
 Mawazo hayo ndio yanayosababisha hata tunapoona hujuma zinafanyika, hatuchukui hatua zozote za kuhakikisha tunazuia, badala tunaona ni jambo la kawaida kukuta mifuniko ya chemba katika barabara imeibiwa huku kukiwa kumefunikwa na gurudumu au majani.