MSD inavyopambana Tanzania ijitegemee bidhaa za afya ikizizalisha nyumbani

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:02 PM Aug 15 2024
PICHA Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha Idofi kinachozalisha glovu za uchunguzi, wakiihakiki kwa ajili ya kuifungasha.
PICHA: RESTUTA JAMES
PICHA Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha Idofi kinachozalisha glovu za uchunguzi, wakiihakiki kwa ajili ya kuifungasha.

KIWANGO kikubwa cha vifaa tiba pamoja na dawa zinazotomika nchini huagizwa kutoka nje, ni jambo linaloligusa Bohari ya Dawa (MSD), ikiazimia kufanya mabadiliko.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, serikali inaagiza kutoka nje dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwa asilimia 86 na asilimia 14 pekee ya mahitaji hayo hupatikana nchini. 

MSD yenye jukumu la kupunguza utegemezi huo wa bidhaa za afya, inasema baada ya marekebisho ya sheria inayounda bohari hiyo, imepewa uwezo wa kuzalisha, kununua, kuhifadhi na kusambaza bidhaa za afya na sasa itaanza kutekeleza jukumu hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, anapozungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam, anasema ili kuondoa utegemezi huo, serikali imeipa mtaji wa Sh. bilioni 100.

Na sasa MSD inakusudia kushirikiana na wabia wenye fedha, teknolojia na uzoefu katika kuzalisha bidhaa za afya, ili lengo la taifa kujitosheleza litimie.

Tukai anasema ili kutekeleza sera ya viwanda, MSD imeanzisha kampuni tanzu ya Medipharm Manufacturing Company Limited, itakayosimamia shughuli za kuzalisha bidhaa zote za afya.

Kwa mujibu wa Tukai tayari bodi ya kampuni hiyo imeshazinduliwa sasa inasimamia viwanda vinavyozalisha bidhaa za afya, vinavyomilikiwa na MSD. 

“Kampuni hii itaweza kuingia ubia na wawekezaji wengine. Kwa sasa, itasimamia kiwanda cha mipira ya mikono cha Idofi - Njombe, eneo la viwanda la Zegereni – Pwani na kiwanda cha barakoa - Dar es Salaam,” anasema.

Anasema mipango inalenga viwanda vya Zegereni, vitazalisha dawa za aina mbalimbali, wakati kile cha Simiyu, kitazalisha bidhaa za pamba kama (gozi  na mashuka), kwa ajili ya matumizi ya hospitali.

Kuwapata wawekezaji wenye uwezo wa kifedha, teknolojia na uzoefu, Tukai anasema MSD inafanya mawasiliano na balozi za Tanzania za China, Korea Kusini, Urusi na  Algeria  ili kuwatambua wazalishaji na wawekezaji wenye sifa hizo.

VIWANDA VILIVYOPO

Anasema viwanda vilivyopo ni kile cha barakoa kilichoko Keko, Dar es Salaam kinachozalisha barakoa za kawaida na maalum (N95). Anaongeza: “Kiwanda cha barakoa kimezalisha na kusambaza barakoa zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni nne na kufanya nchi kujitosheleza kwa bidhaa hizo,” anasema Tukai.

Anaongeza kuwa  kiwanda cha kutengeneza mipira ya mikono  au glovu, kimeanza kazi  Februari mwaka huu na hadi Juni, kilikuwa kilitengeneza glovu milioni nne.

“Kiwanda hiki kimetoa ajira 136 kwa wakazi wa  Makambako na kufanya ununuzi kwenye kampuni mbalimbali ziliozopo eneo hilo. Kwa kutengeneza mipira ya mikono ya kiuchunguzi pekee kiwanda kitaweza kuokoa zaidi ya Sh. bilioni 11,” anasema.

Kaimu Meneja wa kiwanda hicho, Shiwa Mushi, anasema wanatarajia kuzalisha mipira ya uchunguzi au glovu hizo  jozi milioni 86.4 kwa mwaka ambayo itakidhi mahitaji ya ndani kwa asilimia 83.4 kwa muda huo.

Anaeleza kuwa  mahitaji ya mipira hiyo nchini ni jozi milioni 104 kwa mwaka hivyo, uzalishaji wa jozi milioni 86.4 utaokoa Sh. bilioni 20 kwa mwaka na kwamba  malengo ni kuzalisha aina nyingine ya mipira hiyo kwa ajili ya wahudumu wanaofanya upasuaji, kazi yote ya uzalishaji inafanyika kwa umakini na kuzingatia ubora katika kila hatua kwa sababu bidhaa za afya zinahitaji usafi wa hali ya juu.

 Tunazingatia vigezo vya ubora kama tulivyoelekezwa na mamlaka za udhibiti,  anasema  mbali ya viwanda vya Keko na Idofi, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa MSD, Etty Kusiluka, anasema viwanda vya Zegereni na Simiyu, viko mbioni kuanza uzalishaji.

UNUNUZI BIDHAA ZA AFYA

Tukai anasema sambamba na ujenzi wa viwanda, bohari hiyo inajenga maghala ya kuhifadhi bidhaa za afya, ili kukidhi kasi ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali kwenye ujenzi wa vituo vya afya.

“Serikali kupitia Bohari ya Dawa imeanza ujenzi wa maghala ya kisasa katika Kanda ya Mtwara na Dodoma ili kukidhi upungufu uliojitokeza. Ujenzi huu ukikamilika utagharimu kiasi cha Sh. bilioni 40. Kwa sasa mradi umefikia asilimia 55 kwa ghala la Mtwara na asilimia 58 kwa ghala la Dodoma. 

Kukamilika kwa ujenzi wa maghala kutasaidia kuimarisha uhifadhi wa bidhaa za afya kwenye viwango stahiki, kusogeza huduma karibu na vituo vya kutolea huduma za afya, kupunguza gharama za uhifadhi na kuimarisha utunzaji wake,”anasema.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, ujenzi wa maghala hayo unatarajiwa kuongeza nafasi ya uhifadhi wa bidhaa za afya kwa mita za mraba 12,000 ambapo kwa ghala lililopo Dodoma mita za mraba 7,200 zitaongezeka na ghala la Mtwara mita za mraba 4,800 zitaongezeka hivyo kufanya ongezeko la uhifadhi kutoka mita za mraba 56,858.57 na kufikia mita za mraba 68,858.57.

Akizungumzia mapato, Tukai anasema maboresho yanayoendelea yamewezesha vituo vya kutolea huduma za afya kuwa na imani na utendaji wa MSD ambapo makusanyo ya fedha yameongezeka kutoka

Sh. bilioni 40.3 mwaka 2022/23 na kufikia Sh. bilioni 118.9 kwa mwaka 2023/24.

Akieleza zaidi Tukai anasema kutokana na maboresho yanayoendelea kufanywa na Serikali, mapato ya Bohari ya Dawa yameendelea kuongezeka kutoka Sh. bilioni 359.6 kwa mwaka 2022/23, hadi zaidi ya Sh. bilioni 510.07 mwaka wa fedha 2023/24 likiwa ni ongezeko la Sh. bilioni 150.43 ambayo ni sawa na asilimia 42.

Mkurugenzi Mkuu Tukai anasema mbali ya ujenzi wa viwanda, MSD imeongeza ununuzi wa bidhaa za afya kutoka kwa wazalishaji wa ndani ambapo kwa mwaka wa fedha 2023/24, bidhaa za afya zenye thamani ya Sh. bilioni 22.1 zilinunuliwa kutoka kiasi cha Sh. bilioni 14.1 mwaka 2021/22 ikiwa ni ongezeko la asilimia 57.

“MSD imeendelea kufanya ununuzi na usambazaji wa vifaa tiba vinavyohitajika katika vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi vituo vinavyotoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini kama mashine za kusafisha damu , za uchunguzi  MRI na  CT- Scan, ultrasound, digital X-Ray pamoja na vitendanishi vyake.

 Uwepo wa vifaa hivi unawezesha utambuzi wa magonjwa kwa usahihi na kutolewa kwa tiba sahihi,” anasema, na kuongeza kuwa  kununua kwa wingi katika viwanda vya ndani, kumeviongezea uzalishaji na kuvutia wawekezaji ambao watatengeneza ajira huku serikali ikiokoa fedha za kigeni, ambazo zingetumika kuagiza dawa nje ya nchi.

MSD IRINGA

Meneja wa MSD Kanda ya Iringa, Robert Lughembe, anasema ofisi yake inahudumia Halmashauri 17 zilizopo katika mikoa ya Iringa (5), Njombe (5) na Ruvuma (7).

Anasema huduma za MSD zimeboreshwa na sasa wanahudumia wateja mara sita (kila baada ya mwezi mmoja), badala ya mara nne kila baada ya miezi mitatu ya awali.