WATOTO NA SHIDA AKILI: Mbumbumbu darasani, viburi, utundu sana, kuvunja vyombo vyote ni viashiria, fuatilieni

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 09:49 AM Oct 09 2024
 Malezi na makuzi ya mtoto yanahusika moja kwa moja na afya ya akili.
Picha: Mpigapicha Wetu
Malezi na makuzi ya mtoto yanahusika moja kwa moja na afya ya akili.

DUNIA imebadilika mzazi au mlezi, akumbuke kufuatilia watoto wa chini ya miaka saba, umri wa kuanza darasa la kwanza kubaini iwapo wana changamoto za afya ya akili.

Baadhi ya mambo unayoweza kuyapima kubaina kama ana matatizo ni pamoja na kutowaogopa wageni. Anawarukia, kuwazoea ghafla hata wakati mwingine kuwapokonya chakula au kinywaji wanapokaribishwa.

Akiambiwa afanye kazi kama kuondoa sahani mezani baada ya kula anakasirika, kuitupa chini, anapasua vyombo, hana utii wala woga anafanya anachotaka.

Watoto wenzake wanamtenga hawachezi naye, anawapiga na kuharibu vitu vyao. Licha ya kusoma shule za awali tangu miaka mitatu hawezi kusoma, kutamka herufi na kutambua picha.

Kwa ujumla afya ya akili inahusiana moja kwa moja na kile mtu anachokiishi leo na kufunzwa utotoni katika umri wa ‘chekechea’ au shule ya awali.

Mtaalamu wa Saikoloji na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) Dk. Nabwera Rashid, amefanya utafiti na kubaini kasoro za uelewa kwa watoto na shida ya afya ya akili.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti uliohusu: afya ya akili ya watoto wa shule ya awali na uhusiano kwenye matokeo ya masomo ya awali nchini, anasema makuzi ya watoto kuanzia tumboni mwa mama hadi umri wa shule ya awali ni muhimu mno.

Anazungumzia utafiti huo, kwenye mkutano ulioandaliwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wadau wa Afya ya Akili Tanzania (TMH-CoP) ECHO, akisema afya timamu ya akili utotoni inahusisha ustawi wa kihisia, kijamii na kisaikolojia.

Akifafanua zaidi, anasema ni kwa watoto wenye umri sifuri hadi miaka mitano.

Utafiti alioufanya ulihusisha shule 12 kutoka wilaya tatu za Arumeru mkoani Arusha, Kinondoni Dar es Salaam na Nzega Tabora, ukishirikisha watoto 403 wa miaka  ziro hadi saba, kati yao wasichana wakiwa ni asilimia 49.6.

“Mara nyingi mijadala kama hii ya afya ya akili huhusisha vijana sasa huu umelenga watoto nao wanaathiriwa na tatizo la akili. Asilimia 40 ya watoto wanaoishi Afrika, ni kati ya idadi yote ya watu duniani. Wasipolelewa ipasavyo, kuna athari nao ni wazazi wajao.” 

Anasema mtoto anakumbwa na changamoto za kiafya kama tatizo la akili na katika umri huo, hujaribu kukabiliana na hisia zake na masuala mengine ya kijamii.

Na huu ndiyo umri wa kuanza shule kwa mujibu wa sera ya elimu ya Tanzania na pia ni kipindi cha kumtengeneza mtoto amudu kuishi katika jamii. Wengi wa umri huu wanaingia elimu ya awali, wanafundishwa mambo mengi.

Mfano kusalimia, kuwa na marafiki, kunawa mikono na kusema asante au samahani na asipopata elimu atakutana na watu ukubwani, akiwa hana hisia zozote iwe shukrani au huzuni.

Ananukuu Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa, kwenye kila watoto 10 unaokutana nao njiani watatu hadi watano wana tatizo la akili.

Utafiti wake, anasema umebaini kuwa kati ya watoto 403 waliotafitiwa, baadhi wakiwa madarasa ya awali kwa madaraja tofauti, 169 sawa na asilimia 41, hawako sawa katika afya ya akili na kuathiri ujifunzaji.

Dk. Nabwera, anataja maeneo ambayo watoto hao huathirika zaidi ni kuelewa hatua za kusoma kama vile kufahamu ‘fonimu’ mfano K, U na D.

Hawawezi kutaja majina ya picha, ujuzi wa msamiati na fonetiki ambayo ni matamshi ya maneno humtatiza pia.

“Watoto watundu wanaosababisha matatizo kadhaa ni 131 kati ya waliohusishwa kwenye utafiti huu. Nilibaini watoto ni watundu sana yaani hawatulii hata kidogo na darasani pia,” anasema.

Anafafanua kuwa Dar es Salaam Kinondoni alikofanyia utafiti ni miongoni mwa mikoa ambayo wazazi na walezi wana shughuli nyingi na hawana muda wa kulea hawa watoto. 

Anafafanua kuwa katika kila watoto 10 unaokutana nao njiani watatu hadi watano, wana tatizo la akili.

Matokeo yanaonesha kuwa asilimia 58 ambao ni sawa na watoto 235  wa shule ya awali, walikuwa na alama chini ya wastani katika mtihani wa ujuzi wa kusoma  Kiswahili.

Mhadhiri huyo anasema inamaanisha wengi wa watoto wa shule ya awali hawakuwa na ujuzi wa kutaja alfabeti mfano A,B,C,D,E, F…, sauti za alfabeti, kusoma na kuelewa, kushika na kufungua vitabu, utambulisho wa barua na  majina ya picha.

Anasema umri huo ndiyo wa kuanza shule, akisisitiza haja ya watoto wa umri huo, kufuatiliwa uwezo wa uelewa  kwasababu nao huathirika na afya ya akili.

 “Watoto wengi umri huu, ndio wanaingia elimu ya awali, wanafundishwa kusalimia, kuwa na marafiki, kunawa mikono na kusema asante, au samahani na wasipopata elimu hiyo itakuwa tatizo ukubwani ….”

Anasema asilimia 2.8 ya watoto wa umri huo katika utafiti aliufanya, wapo darasani kwa madaraja tofauti kuanzia shule za awali na katika kila darasa moja watoto watano hadi 10 wana tatizo la akili.

Anataja uchokozi, wizi, uongo, hasira hadi wanaojipiga chini kuwa nyuma yake kuna tatizo la akili na mzazi au mlezi ama jamii haijatambua. 

Anakumbusha kuwa labda wakiwa darasani wanaambiwa nenda mbele kasome au nenda kulala hatekelezi maagizo, fahamu kuna shida.

Anaeleza kuwa mtoto anapomaliza kula anatupa sahani chini na kuivunja au  haipeleki inapotakiwa hilo ni tatizo na kwamba anayefanya vizuri ameshaanza kujua kuwa huyu ni mtu mzima na  huyu ni mdogo.

Mhadhiri huyo anasema mtoto aliye na afya duni ya akili akiwa chini ya miaka mitano, akifikia miaka 14 tatizo litaongezeka.

Anasema elimu ya afya kwa watoto hao ni muhimu kutokana na kujumuisha theluthi moja ya watu wote duniani na asilimia 40 kati yao wanaishi Afrika, kwa mujibu wa Mifuko ya Idadi ya Watu wa Umoja wa Mataifa.

Anasema asilimia 2.8 ya Tanzania miaka mitatu hadi sita wanahudhuria shule ya awali akinukuu ripoti ya UNICEF, 2020.

Takwimu za hivi karibuni kimataifa, zinaonyesha katika nchi za Kusini Jangwa la Sahara, takribani watoto milioni 202 wenye miaka kati ya minne hadi 14 hawawezi kusoma kwa ustadi baada ya kuhitimu.

Dk. Nabwera, anasema umri wa miaka mitatu hadi sita, mtoto anaanza kuonyesha hisia zake, mfano ukimwambia kitu hajibu wala hafanyi bali anatoa machozi.  

Anaeleza kuwa mtoto akiwa darasani unamwambia nenda mbele kasome au kalale hatekelezi fahamu kuna shida. 

Anamtaja mtoto anayempiga mwenzake na aliyepigwa asimrudishie fahamu, aliyempiga hawezi kumudu hisia zake lakini ambaye hakumrudishia anazimudu hisia zake.

 Watoto wanatakiwa kufanya kanuni za darasani au nyumbani, watoto wengine utakuta amekaa dawati hili ameshafika nyuma, au keshatoka nje. Muda wa kula  anataka kuimba, wa kuoga e anataka kula, hii ni dalili ya mtoto ameshindwa kumudu hisia zake na majukumu kijamii.

Anasema utafiti hutumia maswali kuuliza  watoto kubaini wana tabia mbaya au nzuri, mfano mwalimu anamwambia usifanye hiki anafanya, au mzazi anamkataza usiende nyumba fulani kuna hiki au mtoto anang'oa maua au ukoka uliopandwa.

Anataja tatizo la aibu, ukimwambia nenda mbele analia, mwalimu akimpa kazi anasema anaumwa tumbo. 

Anazungumzia  mtoto kushindwa kutengeneza marafiki, usimhukumu chunguza kuna tabia ambazo anazo na wen,ake hawazikubali, akiwa nao anawapiga, anahatibu vitu vya wenzake.

“Watoto 131 ‘Wana conduct problem’ tabia mfano za uchokozi, kuiba kalamu, kuchukua saa ya mwenzie kaiharibu. Wanafunzi wengi katika wilaya tatu  hizo wana tatizo la akili.” 

Asilimia 58 ya hao 403 walipata chini ya asilimia 50 ya mtihani wa ‘pre reading’ hawajui mbinu za kusoma. 

Tabia ya mtoto ya utulivu au kinyume chake, inauhusiano mkubwa na uelewa na uwezo wake darasani. Kwa sababu watoto wa aina hiyo ni wasikivu pale mwalimu anapofundisha darasani

Mtoto ambaye hana ujasiri labda kuimbisha wimbo anaweza asijue kusoma haraka.  Tatizo  la akili ni kubwa na linaweza kuathiri jamii ya kesho, niliowatafiti ndio wazazi na wanajamii wajao.”

Anashauri elimu ya saikolojia iwafikie watoto na elimu ya afya ya akili. Malezi yaanzie tangu tumboni analelewaje? 

Anakumbusha kuwa watoto wanahitaji kuwa karibu na mzazi au mlezi katika umri mdogo kwa sababu wanajifunza akianza katika umri wa miaka mitatu hadi 12. 

Anaeleza kuwa akienda bweni, atachukua tabia za huko kwa asilimia kubwa, lakini pia huwa na upweke licha ya kwamba wengi hudhani kuwapeleka shule nzuri inatosha.

Anasema unakuta mtoto mkimya, mpole lakini  mkali kwa sababu hisia zake zinamwambia mzazi alimtelekeza akiwa mdogo.