Elimu matumizi nishati safi ya kupikia muhimu kufikia malengo

Nipashe
Published at 11:25 AM Sep 04 2024
Elimu matumizi nishati safi ya  kupikia muhimu kufikia malengo
Picha: Mtandao
Elimu matumizi nishati safi ya kupikia muhimu kufikia malengo

TANZANIA imeanza kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia. Mkakati huo wa miaka 10 kuanzia mwaka 2024 hadi 2034, Pamoja na mambo mengine unalenga kupunguza athari za tabianchi ambazo kwa sasa ni janga la dunia kutokana na kasi ya uharibifu wa mazingira.

Kasi hiyo inatokana na ukataji miti ovyo kwa ajili ya kuni na mkaa ambayo ni nishati inayotumika kwa wingi kwa kupikia mijini na vijijini. Hatua hiyo imesababisha mabadiliko ya tabianchi. Kwa kutambua hilo, serikali ya sasa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imechukua hatua madhubuti za kukabiliana na uharibifu wa mazingira na athari zake kiuchumi. 

Hatua hiyo inaeleza kinagaubaga kwamba  ongezeko la uharibifu wa mazingira lina athari kubwa kiafya, kiafya kiuchumi na kijamii hasa kutokana na mahitaji makubwa ya nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia ambayo si salama. 

Kutokana na ukweli huo, serikali imeanzisha mkakati huo jumuishi, ambao umeandaliwa ili kutekeleza Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015 ambayo pia inaweka bayana kwamba ongezeko la matumizi ya nishati isiyo safi na teknolojia zisizo sanifu za kupikia, yamechangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira na matatizo ya kiafya kwa watumiaji. 

Kwa mantiki hiyo, mkakati huo unalenga kuboreha maisha ya wananchi kupitia matumizi ya nishati za kisasa za kupikia ikiwamo matumizi ya majiko na vifaa sahihi vya kupikia ambavyo ni mbadala wa kuni na mkaa. Msisitizo mkubwa katika hilo ni matumizi ya gesi ya kupikia pamoja na majiko sanifu yanayotumia teknolojia ya kisasa.

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, alisema juzi wakati akifungua Jukwaa la 24 na Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Fedha ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) kuwa  kupitia mkakati huo, hadi kufikia mwaka 2034 lengo ni kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati hiyo safi.   

Dk. Mpango alisema Tanzania imekuwa kinara wa bara la Afrika kwa ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nyumbani (AWCCSP) kupitia Rais Samia ambaye amekuwa bingwa wa kipaumbele katika kusimamia suala hilo. Rais Samia amekuwa mstari wa mbele katika ajenda hiyo ambayo lengo mojawapo ni kuwaondolea wanawake mzigo wa kutumia kuni na mkaa kupikia. 

Kwa ujumla, lengo la kufikia  asilimia 80 wakati wa kutamatika kwa mkakati huo ni zuri kwa kuwa litawezesha maisha ya Watanzania kuimarika kiuchumi na kijamii pamoja na  kiafya kutokana na matumizi ya nishati safi. Ukataji ovyo wa misitu  hatimaye kusababisha jangwa na kutoweka kwa baadhi ya viumbe adhimu, yatapungua. 

Licha ya kuwapo kwa malengo hayo,  kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu kwa kiasi kikubwa kwa watu ili kutambua umuhimu wa matumizi ya nishati hiyo kwa ustawi wa maisha. Mkakati huu nimtambuka kwa maana kuwa unahusisha sekta mbalimbali, hivyo kila mdau anapaswa kushiriki kwa nafasi yake.

Pamoja na kutolewa kwa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, suala la gharama za gesi na majiko sanifu ya nishari rafiki zinapaswa kupewa kipaumbele ili kuwezesha Watanzania wengi kutumia nishati hiyo. 

Uwezo wa kiuchumi wa wananchi hasa waishio vijijini ni mdogo, jambo ambalo linaweza kuwa kikwazo kwao kununua, hivyo inaweza kuwa chanzo cha kutofikiwa kwa malengo hayo. Kutokana na ukweli huo, ni vyema serikali ikaangalia uwezekano wa kupunguza gharama ikiwamo kutoa ruzuku katika gesi.