TAASISI za umma na binafsi nchini zimekuwa zikifanya ujenzi wa miundombinu mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya sekta kadhaa kama vile elimu, afya, uchukuzi na usafirishaji na nyumba za makazi. Lengo la kujenga miundombinu hiyo ni kuwaondolea wananchi kero na kuleta ufanisi katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya wadau na taifa kwa ujumla.
Katika ujenzi wa miundombinu hiyo kama vile barabara, hospitali na vituo vya afya, viwanja vya ndege, vituo vya mabasi, shule na vyuo, miongoni mwa mambo yanayosisitizwa ni kuwapo kwa mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu. Katika ujenzi wa majengo kama hospitali na shule kwa mfano, kumekuwa na kasi ya ujenzi wa maghorofa jambo ambalo kama suala la wenye ulemavu halitazingatiwa, kuna hatari ya kundi hilo kupata matatizo wanapokwenda kupata huduma stahiki.
Hivi sasa kwa mfano, kumekuwa na kasi ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambayo tayari imeshaanza kutoa huduma kati ya Dar es Salaam na Dodoma huku vipande vingine vya Makutopora hadi Tabora; Tabora hadi Mwanza na Mwanza hadi Isaka ujenzi wake ukiwa unaendelea. Mbali na ujenzi wa reli ya SGR, katika Mkoa wa Dar es Salaam, ujenzi wa miundombinu ya mabasi ya mwendokasi unaendelea katika sehemu kadhaa.
Kuwapo kwa ujenzi wa miundombinu hiyo ya uchukuzi, kumeibua maswali kama suala la mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu hasa kwenye stesheni za SGR unazingatiwa.
Juzi, jijini Dodoma, wakati wa mkutano wa Bunge unaoendelea, Naibu Spika, Mussa Zungu, aliielekeza serikali kuchukua hatua za haraka kuimarisha huduma kwa watu wenye mahitaji maalum kwenye stesheni za reli ya mwendokasi. Zungu alitoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Asha Abdallah Juma, kuhoji lini serikali itaongeza idadi ya viti mwendo kwa ajili ya abiria wenye mahitaji maalum kwenye viwanja vya ndege na stesheni za SGR.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, watu wenye mahitaji maalum wanapata shida sana kusafiri hasa kwenye stesheni za SGR kutokana na kutokuwapo kwa mazingira rafiki kwao, hususan kukosekana kwa viti mwendo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, alisema serikali imeshapeleka viti mwendo vya umeme ambavyo vinasimamiwa na watoa huduma katika maeneo hayo. Pia, alisema watu hao wakiwamo madaktari kwenye viwanja vya ndege na stesheni za SGR wamepatiwa mafunzo kwa ajili ya huduma hizo.
Licha ya Naibu Waziri kutoa majibu hayo, Naibu Spika huyo alielekeza hatua za haraka zichukuliwe ili kuimarisha huduma kwenye stesheni hizo ili watu wenye mahitaji maalum waondokane na adha wanayoipata.
Kwa maagizo na maelekezo ya serikali katika mchakato wa ujenzi wa miundombinu, suala hilo limekuwa likisisitizwa na kwa sehemu kubwa linatakelezwa. Hivi sasa hakuna sehemu ambayo mtu anaweza kwenda na kukuta hakuna miundombinu ya kundi hilo la watu wenye ulemavu.
Pamoja na kuwapo huko, kama alivyohoji mbunge kuwa wenye ulemavu wanapata adha kutokana na kutokuwapo huduma toshelevu, ni vyema serikali ikajielekeza zaidi katika kutatua suala hilo. Mpaka mbunge kuhoji hivyo na naibu spika kutoa msisitizo, inawezekana kuna changamoto katika eneo hilo.
Jambo la msingi na la kuzingatiwa katika hilo ni kwamba mifumo ya miundombinu irekebishwe ili kuwawezesha wenye ulemavu kuondokana na adha ya kukumbana na vikwazo katika kupata huduma mbalimbali. Pia, katika miradi inayoendelea, taasisi maalumu za serikali zifuatilie takwa hilo la kuwapo kwa miundombinu ya watu wenye ulemavu.
Kwa kuwa ujenzi wa miundombinu ya kijamii na kiuchumi ni endelevu, taasisi zinazohusika na kazi hiyo, hazina budi kutambua kuwa jambo hilo si la kuibua mjadala bali kinachotakiwa ni utekelezaji pekee.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED