HATA kama yatapuuzwa au wahusika kuziba masikio, lakini kuna kelele na manung'uniko kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka kwenye mitandaoni ya kijamii na kupitia baadhi ya vyombo vya habari, kuhusu Kampuni ya GSM kudhamini zaidi ya timu moja kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wala huwezi kuuliza kuwa yanatoka wapi zaidi ya wanachama na mashabiki wa Simba, ambao wanaona hakuna haki kwa kampuni hiyo kudhamini timu takriban sita hivi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hapa hatusemi wapo sahihi au la, lakini manung'uniko yanapozidi siku hadi siku, yanapaswa wenye mamlaka na soka la Tanzania Bara kukaa chini na kutafakari kwa kina, kwani walalamikaji wanaonekana kuwa na hoja.
Tumewasikia baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kwa nyakati tofauti wakisema hakuna kanuni inayozuia na pia udhamini huo unaziingizia timu ambazo nyingi hazina uwezo mkubwa wa kipato.
Kwa hilo la kipato tunadhani wapo sahihi, lakini ni lazima liangaliwe kama hicho kipato kipo katika njia sahihi ambayo haiwezi kwa namna yoyote kuhusika katika upangaji wa matokeo.
Hebu hapa twende sawa, klabu ya Arsenal inadhaniwa na Shirika la Ndege la Emirates na ni klabu pekee nchini humo inayodhaminiwa na shirika hilo, zingine nje ya hapo ni PSG ya Ufaransa, AC Milan ya Italia na Real Madrid ya Hispania.
Hata hivyo, japo timu hizo zinaweza kukutana kwenye michuano ya Ulaya, lakini udhamini wa Emirates hauna chembe yoyote ya vinasaba na moja kati ya klabu hizo mbali na udhamini kibiashara, hivyo hautiliwi shaka kwamba kunaweza kuwapo na aina yoyote ya upangaji wa matokeo kwani haijawekeza kwenye klabu yoyote zaidi ya kudhamini tu.
Ukiangalia hapa nchini GSM, inaonekana amejikita kabisa katika Klabu ya Yanga. Ndiyo inayohusishwa na sapoti kubwa katika usajili na kuiendesha timu, huku ikionekana kusaidia pakubwa mchakato wa uwekezaji.
Hivyo, inakuwaje kampuni hiyo hiyo inakwenda kudhamini timu zingine kwenye Ligi Kuu? Hata kama hakuna kanuni, hata busara tu haielekezi? Hivi mtu kama Mohamed 'Mo' Dewji akianza kudhamini timu za Ligi Kuu, wakati tayari anautaka uwekezaji Klabu ya Simba, unatarajia nini baada ya kuzidhamini zingine?
Kama ambavyo walioainisha kwamba kunaweza kuwapo na upangaji wa matokeo kwa kampuni tu ambayo haipo kwenye klabu yoyote kudhamini zaidi ya timu moja kwenye ligi moja, inakuajie kwa Ligi Kuu Bara?
Kwa mtazamo wetu tunaona kama tunaanza kurudi nyuma, wakati tulishatoka huko zamani. Tunakumbuka kulikuwa na timu za Mgambo JKT, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, zote zikimilikiwa na taasisi moja ya Jeshi la Kujenga Taifa na zilikuwa Ligi Kuu, lakini moja kati ya maazimio ya Bagamoyo mwanzoni mwa miaka ya 2000 kutoka FIFA, ulizitaka klabu zote za aina hiyo kuwa na timu moja tu kwenye ligi.
FIFA iliona hakutakuwa na haki na usawa, kwani JKT Ruvu kama inahitaji pointi moja ili isishuke daraja na inacheza na Ruvu Shooting ambayo ipo salama kwa alama zake, haiwezi kuikosa kwa sababu mwajiri wao ni mmoja, hivyo kuzuia haki kwa timu ambazo hazina timu zenye vinasaba na nyingine kushinda kwa haki.
Ndiyo maana kwa sasa kuna JKT Tanzania, pia kuna Polisi Tanzania, badala ya Polisi Dodoma na Polisi Morogoro ambazo kuna kipindi zote zilikuwa Ligi Kuu kwa wakati mmoja.
Hivyo, kwa hili la udhamini huu wa GSM kwa timu takriban sita Ligi Kuu tunaona wadau wa soka wana hoja na TFF na Bodi ya Ligi hawapaswi kulifumbia macho kwani litaturudisha nyuma kwa kushindwa kupata bingwa aliyestahili kwa ligi yetu ambayo sasa tunatamani itoke kuwa namba sita kwa ubora Afrika na kupanda juu zaidi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED