Viongozi wakiwajibika ipasavyo kero za wananchi zitatatuliwa

Nipashe
Published at 02:21 PM Aug 20 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: Ikulu
Rais Samia Suluhu Hassan.

KILA mara Rais Samia Suluhu Hassan anapofanya mabadiliko ya viongozi katika ngazi mbalimbali na kuwaapisha wateule hao, amekuwa akiwasisitiza kwenda kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu. Pia amekuwa akiwataka kuwa wabunifu katika kutatua kero zinazowakabili wananchi.

Sambamba na hayo, Rais Samia amekuwa akiwakumbusha wateule hao wakati wa kuwaapisha na kila anapofanya ziara mikoani kwamba wasijifanye miungu watu kwa kunyanyasa wananchi na kusujudiwa bali watambue kuwa ni watumishi wa wananchi. Kwa mantiki hiyo viongozi hao wamekuwa wakisisitizwa kutokukaa ofisini badala yake waende kwa wananchi kusikiliza kero zinazowakabili na kuzitatua. 

Licha ya maagizo hayo, baadhi ya wateule hao wamekuwa wakidaiwa kutumia nafasi zao vibaya kwa kuwanyanyasa wananchi huku muda mwingi wakikaa ofisini badala ya kwenda kusikiliza kero na kuzitatua. 

Hata hivyo, wako baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakifanya vizuri katika utatuzi wa kero za wananchi kama vile ubovu wa miundombinu, uhaba wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo, migogoro ya ardhi na upatikanaji wa maji safi na salama. Wateule hao, akiwamo mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, wameonyesha mfano katika kushughulikia kero za wananchi na zingine kuzipatia ufumbuzi. 

Kiongozi huo aliporipoti Arusha kuanza majukumu yake, alitembelea halmashauri zote na kubaini matatizo mengi yanayowakabili wananchi na kuhoji baadhi ya watendaji kwa nini wameshindwa kutafutia ufumbuzi. Kwa ujumla, mambo aliyoyaibua katika ziara yake hiyo, yalionesha kwamba watendaji wengi wameshindwa kutekeleza wajibu wao kwa kusimamia kazi zao pamoja na kuzipatia ufumbuzi kero zinazowakabili wananchi. 

Moja ya kero aliyoiibua na kuanza kuishughulikia ni migogoro ya ardhi huku baadhi ya wananchi wakilalamika kuwa baadhi ya watendaji kwenye sekta hiyo wamekuwa sehemu ya matatizo hayo. 

Kwa maneno mengine, watendaji hao wamekuwa wakishiriki kuuza ardhi au kupindisha ukweli ili kunufaika  kwa kupewa kiasi cha fedha na  matokeo yake kusababisha wanyonge wengi kukosa haki. 

Aidha, Makonda katika kampeni ya upimaji wa afya ambayo ilifanyika katika mikoa yote, alikuja na ubunifu wa kipekee kwa madaktari bingwa kutoka mkoani humo na taasisi kubwa kama Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Dk. Peter Kisenge, kwa ajili ya kufanya uchunguzi na kutoa tiba. Pia ziliandaliwa helikopta kwa ajili ya kuwapeleka wagonjwa waliobainika kuwa na maradhi makubwa yanayohitaji matibabu ya kibingwa kwenye hospitali kubwa. 

Ubunifu huo ulipongezwa na viongozi wa ngazi ya juu akiwamo Rais Samia kuwa ni mfano wa kuigwa kwa viongozi wengine. Kwa hakika ubunifu kama huo ni chachu kwa viongozi mbalimbali, kwa nafasi zao, kufanya kile kinachotakiwa katika kutatua kero za wananchi. 

Kumekuwa na msemo kwamba kama wao wanaweza kwa nini sisi tushindwe? Kutokana na msemo huo, ni kwa nini mtu mmoja aoneshe kwamba utatuzi wa kero unawezekana na wengine wanashindwa? Aidha, kwa nini wateule hao wamekuwa wakisisitizwa katika awamu zote za uongozi wa nchi kuwa wabunifu na kutambua kuwa ni watumishi wa wananchi na si watu wa kutumikiwa lakini wameshindwa kutekeleza maagizo hayo?          

Ni wazi kwamba kutokupatikana kwa suluhu ya kero zinazowakabili wananchi, kunatokana na baadhi ya wateule hao kujiona kuwa miungu watu na wamezipata nafasi hizo ili kujinufaisha badala ya kumsaidia Rais kushughulikia matatizo ya wananchi. 

Ni wakati mwafaka sasa wateule wa Rais, kwa maana ya wakuu wa mikoa na wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na watendaji walio chini yao, wakarejea maagizo wanayopewa katika utekelezaji wa majukumu yao. Kwa kufanya hivyo, ni dhahiri kwamba kero nyingi za wananchi zitapatiwa ufumbuzi.