Kuelekea Olimpiki Paris 2024, TOC, RT zavutana

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:57 AM Jul 16 2024
Olimpiki Paris  2024.
Picha: Maktaba
Olimpiki Paris 2024.

WAKATI homa ya Michezo ya Olimpiki ya majira ya joto itakayoanza kutimua vumbi Julai 26 na kumalizika Agosti 11, mwaka huu, jijini Paris, Ufaransa likizidi kupanda, msuguano mkali umeibuka nchini baina ya Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), imefahamika.

Kawaida TOC ndio mratibu wa ushiriki wa Tanzania katika michezo hiyo itakayofunguliwa na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, ambako Tanzania itawakilishwa na wanamichezo saba tu, kutoka katika michezo mitatu ya Riadha (wakimbiaji wanne), Judo (mchezaji mmoja) na Kuogelea (waogeleaji wawili).

Katika riadha, Tanzania itawakilishwa na Alphonce Simbu na Gabriel Geay (marathon wanaume), Jackline Sakilu na Magdalena Shauri (marathon wanawake), judo itawakilishwa na Andrew Mlugu, huku Collins Saliboko na Sophia Latiff wao wakibeba bendera ya uogeleaji (wanaume na wanawake).

Tayari nyota hao wanaendelea na mazoezi yao ya mwisho yanayosimamiwa na vyama vya michezo yao au kwa udhamini wa TOC na Olympic Solidality (OS), lakini tayari msuguano umeibuka unaoitishia ari ya ushiriki ya baadhi yao, idadi yao na hata ustawi wa mafanikio yao na michezo kwa ujumla.

Kwa mujibu wa taarifa, RT mwaka jana lilisaini mkataba wa ufadhili na udhamini wa vifaa vya michezo na pesa za bonasi na Kampuni ya Xtep ya China, unaoitaka kampuni hiyo kuzivalisha timu zote za riadha zitakazoshiriki mashindano ya kimataifa, pamoja na bonasi ya fedha kwa washindi.

Kupitia mkataba huo, Xtep mwaka jana ilitoa mafungu 50 ya vifaa vya michezo ikiwamo mavazi na viatu, ambako mwaka huu inaipa RT mafungu 250 ya vifaa hivyo, pamoja na bonasi ya Dola 50,000 kwa mshindi wa medali ya Dhahabu, Dola 30,000 medali ya Fedha na Dola 20,000 kwa medali ya Shaba.

Lakini zikiwa zimebaki wiki mbili kuelekea ufunguzi wa Olimpiki ya Paris, Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi, kupitia mahojiano maalum, ameweka wazi kwamba hawautambui mkataba huo na kwamba jukumu la kuwavalisha wachezaji wanaoshiriki Olimpiki na Michezo ya Jumuiya ya Madola ni la TOC, kupitia mdhamini wao, Asics.

Akizungumza na mwandishi wetu alipotaka kujua suala la RT kutumia udhamini wa Xtep, Bayi alisema, “kwa kifupi jibu la swali lako ni hawana nafasi kabisa. Michezo ya Olimpiki siyo ya Judo, Riadha na Kuogelea tu, kuna michezo zaidi ya 30 itakayoshiriki Paris 2024.

“Kwa mfano Tanzania iwe na wawakilishi wa michezo zaidi ya mitano, kwa hiyo kila mchezo uwe na udhamini wa vifaa vyake watakavyotumia katika Michezo ya Jumuiya ya Madola au Olimpiki, hiyo itakuwa timu ya Taifa au itakuwa vurugu? Alihoji na kuendelea;

“Katiba ya TOC na ‘Olympic Charter,’ mamlaka ya kupeleka na kuvalisha timu ya kushiriki Jumuiya ya Madola au Olimpiki ni ya Kamati za Olimpiki na si vinginevyo. Kabla ya vyama/mashirikisho ya michezo kuingia mikataba yao, nashauri wasome Katiba ya TOC na ‘Olympic Charter."

Aliendelea kufafanua, “TOC na IOC inaheshimu utumiaji wa viatu vya mashindano (spikes/marathon race shoes) kwa wanamichezo wenye mikataba yao binafsi, lakini siyo training shoes na mavazi wakati wa michezo ya Olimpiki.

“Vyama vya michezo vina Mashindano yao Kimataifa, (Kanda, Bara na Dunia), ambavyo wanaweza kusaini mikataba kwa ajili ya mashindano hayo tu, si Olimpiki na Jumuiya ya Madola. Natoa rai kwa vyama vya michezo, wanaposaini mikataba na makampuni ya vifaa vya michezo wasihusishe michezo ya Jumuiya ya Madola na Olimpiki.

Alipoulizwa kuhusu kambi ya pamoja ya wawakilishi wote wa Olimpiki 2024, Bayi akajibu; “TOC haitakuwa na kambi kama ilivyozoeleka, kwani wachezaji wote waliofikia viwango vya Paris 2024 wa Riadha wawili wa kiume (Simbu na Geay) walikuwa kwenye udhamini mzito wa Olympic Solidarity.

“Wanariadha wa kike wawili (Magdalena na Jackline) waliofikia viwango vya kushiriki Paris 2024 watakuwa na udhamini wa TOC mpaka Julai 30, 2024.

Kuhusu wachezaji wengine; (Mlugu anayecheza judo) na (Collins - kuogelea), wao walikuwa kwenye udhamini wa Olympic Solidarity na World Aquatics, isipokuwa Sophia Latiff, ambaye licha ya kutofikia viwango, alipewa nafasi ya upendeleo (Universality),” anamaliza Bayi. 

Alipotafutwa Kaimu Katibu Mkuu wa RT, Wakili Jackson Ndaweka, alikiri wazi kwamba uhalali wa kuvalisha wanamichezo wanaoshiriki Olimpiki ni wa TOC, lakini isingekuwa rahisi kwao kukataa udhamini wa Xtep, uliokuja miaka 16 tangu walipovunjiwa mkataba kwa mtindo huo huo mwaka 2008 kuelekea Olimpiki ya Beijing, China.

“Kwa nafasi yake (Bayi) kama Katibu wa TOC, aliwahi kutuandikia barua RT kuuliza juu ya uwapo wa mkataba baina yetu na Xtep, nilimjibu kwa maandishi kuwa ni kweli na nikaenda mbali zaidi kwa kumueleza moja ya matakwa ya kimkataba ni kutumia vifaa vyao katika Olimpiki.

“Pia nikamweleza kwamba kwa zaidi ya miaka 16 tangu TOC waliposababisha mkataba wetu na Kampuni ya Li Ning kuvunjika baada ya kuvalisha wanamichezo wetu vifaa vya Kampuni ya Puma, RT haikuwa na mdhamini wa vifaa, jambo ambalo limetupa wakati mgumu sisi kama shirikisho na Serikali, ambao tulilazimika kununua vifaa.

“Kupitia barua yangu hiyo kwake, nikaiomba TOC ituruhusu wanariadha wetu wavae vifaa vya Xtep, ili si tu kumlinda mdhamini wetu ambaye ataendelea kutupa vifaa hata baada ya Olimpiki, bali kutopoteza bonasi kubwa zilizoko mezani kwa wanariadha wetu iwapo watarudi na medali katika Olimpiki 2024.

“Xtep wameweka mezani Dola 50,000 kwa mwanariadha atakayetwaa medali ya Dhahabu, Dola 30,000 kwa medali ya Fedha na Dola 20,000 kwa medali ya Shaba, hizi ni bonasi ambazo hata ukiwatafuta kina Simbu, Geay na wengineo, watakwambia wanavyopambana kupata pesa za ushindi na bonasi hizo.

“Sasa kama TOC watashikilia msimamo kwamba wanaraiadha wetu watavalishwa vifaa vya Asics na si Xtep, sisi kama shirikisho tutachukua hatua. Wanayo mamlaka ya kuwavalisha Assics, lakini sisi ili kuondoa hatari hiyo ya kuwavalisha vifaa vya mpinzani wa mdhamini wetu.

“Hatutaruhusu wala kukubali watuvunjie mkataba ambao una manufaa kwetu hata baada ya Olimpiki, tutapata sapoti gani kutoka kwao kupitia mdhamini wao baada ya Olimpiki? Wachezaji watanufaikaje na kutumia vifaa vya mdhamini wao baada ya mshindano? Hapa ndipo tunaposema tutachukua hatua," alisema.

 Alphonce Simbu afunguka

Kwa upande wake, Simbu alikiri kupata kizungumkuti, kwani anaamini unahusisha mamlaka ambazo zinapaswa kukaa kwenye meza ya mazungumzo ili kupata suluhu itakayowapa fursa ya wao kushindana wakiwa kwenye mavazi ya Xtep, kwani wana ari kubwa ya kutwaa dola za bonasi hizo

“Kimantiki RT ndio yenye wachezaji na mikataba mingi inasainiwa na RT, na kama Xtep ni mdhamini wa shirikisho, basi ni bora wakatuacha tukatumia vifaa vyao, ingawa pia natambua kwamba wenye mamlaka ya kutuvalisha ni kamati na sio shirikisho."

Naye Mjumbe wa Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam (DAA), na Kocha wa siku nyingi, Kapteni Mstaafu Lucas Nkungu, alisema hatamani kuona tukio la 2008 likijirudia tena, kwani itakuwa pigo kwa mchezo wa riadha na kuomba serikali kupitia wizara yenye dhamana, kuingilia kati na kuhakikisha muafaka unapatikana.