KILA mara wazazi na walezi wamekuwa wakitupiwa lawama kuwa ni chanzo cha watoto wao kukithiri kwa utoro shuleni, watoto wa mitaani na kujihusisha na vitendo viovu kwa kujiunga katika makundi yasiyofaa.
Migogoro ndani ya ndoa, nayo imekuwa ikielezwa kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watoto wengi wa mitaani, kukosa mwelekeo kwa kuwa na tabia mbaya na kupata malezi mabaya.
Hayo yote inawezekana kuwa yapo, isipokuwa ni zipo njia za kuhakikisha kwamba hayaendelei kutokea katika jamii kwa kuziba viashiria vyake.
Mbaya zaidi na jambo la kusikitisha, ni kitendo cha baadhi ya wanafunzi kuonekana wakizagaa mitaani na kwenye maeneo yasiyofaa kwa ajili ya ustawi wa makuzi yao.
Hapo ndipo baadhi ya watu waliposikika wakilalamikia baadhi ya shule kuwa zinachangia wanafunzi kukithiri kwa utoro kutokana na kurudishwa nyumbani bila ya wazazi na walezi wao kupewa taarifa kwa njia ya barua na simu.
Tangu shule zilipofunguliwa siku chache zilizopita, wanafunzi wengi wameshuhudiwa wakizagaa mitaani wakizurura huku na kule bila ya kuwa na sababu za msingi.
Wanafunzi wengine wameonekana maeneo ya sokoni ‘wakichakura’ mabaki ya bidhaa zilizotupwa, wengine wakiwinda ndege kwenye miti kwa kutumia manati na wengine mtoni na mabwawa wakivua samaki.
Wapo waliokutwa wakicheza mpira kwenye maeneo yaliyowazi na majumba makuu ambayo ujenzi wake haujamilika.
Wengine walikuwa wakicheza mchezo wa bao, kamari na mingine katika vichaka.
Mbaya zaidi, wako waliokutwa maeneo kunakoendeshwa biashara za vileo kwenye makazi ya watu, wakipambana kucheza kamali kwenye mashine maarufu kama bonanza.
Mchezo huo uliokolea kwelikweli kutokana na wanafunzi hao kugawanyika katika timu mbili.
Kila upande ulikuwa ukishangilia mmoja unapoliwa na mwingine unapokula fedha ambazo zilipatikana kwa wao kuchangishana.
Kitendo hicho kiliwafanya hata wapiti njia katika sehemu hizo za biashara, kusimama ili kufahamu kulikoni, huku wengine wakipigwa na butwaa kutokana na vitendo hivyo kufanyika wakati wanafunzi hao wakitakiwa kuwa shuleni kwa kuwa ni muda wa masomo.
Wanafunzi hao walipoulizwa kulikoni, wakasema wameamriwa na walimu kurudi nyumbani kwa wazazi na walezi wao kwenda kuchukua fedha kwa ajili ya kuchangia chakula cha mchana shuleni.
Ni kweli makuzi ya mtoto na malezi bora huanzia kwa mzazi na mlezi nyumbani, na anapokabidhiwa shuleni, inakuwa ni jukumu la mwalimu kuhakikisha anapata elimu bora.
Chakula cha mchana shuleni kwa mwanafunzi ni muhimu kwa sababu kinasaidia kumjenga katika afya bora, akili na kuwa na usikivu darasani.
Kwa maana hiyo, kamati za shule zingetakiwa kuwasiliana na wazazi na walezi wa wanafunzi ambao hawajalipa fedha kwa ajili ya kuchangia chakula hicho badala ya kuchukua hatua ya kuwarudisha nyumbani bila ya kuwapa taarifa.
Matokeo yake wanafunzi hao wamekuwa wakitoka nyumbani asubuhi na kuishia mitaani wakijihusisha na vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikichangia kumomonyoka kimaadili.
Watoto hao wanapoamka asubuhi na kuaga wanakwenda shule, wako wanaopewa fedha kwa ajili ya kununua maji, matokeo yake wanaelekeza katika michezo ya kamari, mchezo ambao kwa mujibu wa sheria hauruhusiwi kuchezwa na vijana wenye umri chini ya miaka 18.
Kwa mujibu wa wanasaikolojia, mtoto anapoanza kuwa na akili, ndicho kipindi cha kuanza kumdhibiti kitabia.
Wanasema, akiachwa katika kipindi hicho, ndipo anapoanza kuiga tabia mbaya na njema. Shime wazazi, walezi na walimu tushirikiane katika malezi na makuzi ya watoto kwa kupeana taarifa wanapokuwa shule na nyumbani.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED