KWA miaka ya hivi karibuni Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inaonekana haifanyi kazi yake ipasavyo.
Timu zinaposhindwa kupata mwafaka na kupeleka malalamiko kwao ili kupata ufafanuzi wa kisheria na kuamua, lakini inawarudishia 'mpira' eti wakapatane wenyewe.
Wameshindwaje kupatana mwanzo na safari hii iwezekane?
Hii inashangaza kidogo, ni sawa na ugomvi na mume na mke ambao wamegombana huko na wamekwenda kwa mtu nzima wanayeamini anaweza kuwasuluhisha na kuwapatanisha, badala yake mtu huyo anawaambia waende wakamalizane wenyewe, msuluhishi huyo anashindwa kutambua wao hawakuelewana ndiyo maana wamefika kwake.
Tumeona kesi nyingi, na hasa msimu huu ndiyo kumekuwa na matatizo hayo, tangu kesi ya Lameck Lawi kati ya Simba dhidi ya Coastal Union, pia tumeona pia kesi ya KMC na Simba dhidi ya mchezaji Awessu Awessu.
Tushukuru Mungu pamoja na yote, Simba na KMC wamekaa kama walivyoambiwa na kulimaliza suala hilo, na kwa hivi tunavyozungumza, Awessu na mali ya Simba.
Pamoja na hayo yote kunaonekana kuna matatizo kidogo katika kamati hiyo, hasa linapokuja suala la kufanya uamuzi wa kimkataba kuhusiana na wachezaji husika.
Sidhani kama kuna utofauti kati ya kamati hii na ile ambayo ipo Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), ambako hatujawahi kusikia wamepelekewa kesi na wameamua kuwaridishia wenyewe waelewane.
Wao wanakwenda moja kwa moja kuangalia sheria na kanuni zinasemaje na wakaamua kulingana na jinsi walivyojiwekea, bila kujali litamuumiza mtu fulani au litamfurahisha.
Sasa unashangaa ni kwa nini Kamati ya TFF huwa haitumii sheria na kanuni zake kuamua badala yake ni kama vile inatumia busara hivi kwa kuogopa labda watu fulani watakasirika.
Sheria zipo, kanuni zipo, kwa nini hawazitumii kuamua kesi za kimkataba wa wachezaji? Na kitendo chao cha mara kwa mara kuamua klabu zikaelewane wanaweza kuwa wanatengeneza mwanya kwa wachezaji wasio waaminifu, na klabu ambazo haziheshimu mikataba kurudia makosa ya aina hiyo.
Inawezekana labda ni kwa sababu kamati hiyo ina baadhi ya watu ambao si wanasheria.
Kwa maana hiyo, ipo haja sasa ya kuiangalia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, mbali na Mwenyekiti na Makamu wake kuwa na taaluma ya sheria, basi hata wajumbe wake wawe ni wanasheria ili waamue kutokana na sheria inavyowaelekeza na si vinginevyo.
Nikisema sheria nina maana ya sheria za mpira wa miguu, yaani wawe wamejikita kwenye sheria za mchezo huo na si za mikataba ya nyumba, magari au viwanja.
Kuna mwanasheria mmoja ameniambia mikataba ya wachezaji ambayo ipo kwenye sheria za soka, haifanani kabisa na mikataba mingine kama ya nyumba magari, viwanja, hivyo wanaotakiwa hata kuwasimamia wachezaji na klabu wawe ni watu wanaoijua.
Nadhani hata kamati nayo inatakiwa iwe na watu hao. Ndiyo maana utaona hata mchezaji akifanya makosa, siku hizi hafungiwi miezi sita au mwaka, badala yake analipishwa faini na fidia, uharaka wa kulipa ndiyo unatamfanya kuchelewa au kuwahi kuwa huru.
Kitendo cha Kamati kumrudisha Awessu katika klabu yake ya KMC binafsi naona hakikuwa sahihi kwa sababu alionekana hawezi tena kuitumikia kiasi cha kutamka kuwa yupo tayari kurejea Zanzibar kuvua samaki.
KMC nao wamekuwa waungwana, wangeweza kutumia mwanya huo kumkomoa kwa sababu wameshapewa mpini na mchezaji ameshika kwenye makali. Ndiyo maana FIFA haikubali kumrudisha mchezaji katika klabu ambayo haitaki tena. Hata kama ana kesi, wakati inaendelea inamuuliza klabu anayotaka kucheza. Huku ndiko wenzetu walipofika, lakini sisi bado tunaamua kwa 'busara' ili tusionekane wabaya.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED