JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilianzishwa rasmi Septemba Mosi mwaka 1964, lengo likiwa kulinda uhuru wa nchi na mipaka ya Tanzania. Historia inaonesha tangu kuanzishwa kwake, imefanya mengi yakiwamo yanayoendelea kuweka kumbukumbu njema kwa wananchi.
Vyombo kadhaa vya habari vya ndani na nje ya nchi vimeripoti baadhi ya matukio hayo, yanayoonesha umahiri wa askari wa JWTZ, ikiwamo tukio la mwaka 1978, vita vya kumshikisha adabu Nduli Iddi Amini Dadah, aliyeichokoza Tanzania akitaka kumega ardhi ya Mkoa wa Kagera.
Aliyekuwa Rais wakati huo na Amiri Jeshi Mkuu, Mwalimu Julius Nyerere, hakumpa nafasi Nduli huyo kupata alichotamani, badala yake alimtangazia vita mchokozi Iddi Amini, akitamka Dadah: “Ametuchokoza; uwezo wa kumpiga tunao, sababu ya kumpiga tunayo, nia ya kumpiga tunayo, hivyo tumeamua kupambana naye."
Majeshi ya Tanzania yakiongozwa na JWTZ yalipambana na kushinda vita hiyo, Iddi Amini Dadah, baada ya kuelemewa alikimbilia nchini Libya kutafuta hifadhi. Ni wazi alishikishwa adabu hadi akaikimbia nchi yake.
Askari wa JWTZ wameshiriki kulinda amani kwenye nchi kadhaa barani Afrika miongoni mwao wapo wachache waliopata ulemavu, pia kadhaa walipoteza maisha yao, Mwenyezi Mungu awajalie pumziko la amani askari wa JWTZ waliopoteza maisha yao kwenye vita tofauti ikiwamo hiyo ya Uganda, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Liberia na Lebanon.
Askari hao, siyo mahiri kwenye vita pekee bali hata kwenye shughuli za kijamii wamekuwa wakijitokeza mstari wa mbele kama vile kwenye uchangiaji wa damu salama, shughuli za JWTZ limeadhimisha Siku ya Mazingira Juni 5 mwaka 2021, walifanya shughuli za utunzaji mazingira ikiwa ni pamoja na upandaji miti, kufanya usafi na michezo.
Walishiriki kwenye usafi mikoa tofaut,i ikiwamo mkoani Dodoma Soko la Ndugai, Hospitali ya Mkoa, Hospitali ya Makole mkoani Morogoro walisafisha Shule ya Msingi Mwenge iliyopo Kijiji cha Pangawe, Tabora, Hospitali ya Rufaa ya Kitete na wakati Dar es Salaam walifanya usafi, Hospitali ya Kigamboni, Shule ya Msingi Changanyikeni, Hospitali ya Vijibweni, na Barabara ya Tungi Ferry Kigamboni.
Pia, JWTZ imeshiriki katika matukio ya utoaji msaada wa uokoaji yanapotokea majanga, ikiwamo lililotokea mwishoni mwa Desemba mwaka 2023, katika maporomoko ya tope Kateshi Hanang mkoani Manyara, tarehe 26, mwezi uliopita katika maadhimisho ya miaka 60 tangu kuazishwa kwake limetoa huduma za matibabu bure kwa wananchi Nachingwea katika viwanja vya shule ya Msingi Majengo.
Matibabu yaliyotolewa hapo ni pamoja uchangiaji wa damu, wametoa huduma ya uchunguzi wa saratani ya matiti na shingo ya kizazi, saratani ya tezi dume kwa njia ya damu, upimaji wa homa ya Ini, kisukari, Kaswende, shinikizo la damu(BP), Upimaji wa VVU na uchunguzi wa kinywa na meno.
Ni wazi wananchi waliojitokeza kupata huduma hiyo, baadhi wamekaririwa wakielezea kufurahishwa na huduma hizo.
JWTZ, pia katika maadhimisho ya sherehe kadhaa za kimataifa wamekuwa wakishiriki na kuwavutia wengi hasa kwa maonyesho kadhaa ambayo hufanywa na askari wake ikiwamo wa kikosi cha Makomandoo, hivyo kwa namna fulani imekuwa ikitoa burudani ya aina yake ambayo hufurahisha hivyo kupunguza ama kuondoa msongo wa mawazo kwa baadhi ya wananchi.
Nimetaja matukio machache kati ya mengi yaliyofanywa na JWTZ, naamini yapo ambayo sitayataja kwa sababu ya nafasi kuwa dogo, lakini kwa hakika matendo wanayoonyesha umuhimu wa jeshi hilo kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Dhima ya JWTZ ni kulinda nchi na kutetea maslahi ya taifa la Tanzania, kutoa msaada kwa mamlaka za kiraia na kuwezesha kufikiwa kwa malengo ya kitaifa na kimataifa.
Majukumu yake ni kulinda Katiba na Uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Ulinzi wa mipaka ya Tanzania;Kufanya mafunzo na mazoezi, kujiweka tayari kivita wakati wote; Kufundisha umma shughuli za ulinzi wa taifa.
Aidha, inashirikiana na mamlaka za kiraia kutoa misaada ya kibinadamu na uokoaji wakati wa maafa; kukuza elimu ya kujitegemea na uzalishaji kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT); na kushiriki katika ulinzi wa amani Kimataifa.
JWTZ ni mfano mzuri wa kuiga kwa namna wanavyomudu kutimiza majukumu yao na kujenga imani kwa wananchi, kwa hakika wameweza. Inatarajiwa kuendelea kuwa bora zaidi na zaidi, pongezi walizopewa hivi karibuni ikiwamo za kutoka kwa Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan zinastahili kutokana na uwajibikaji wao .
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED