Wapo wanaotaka kulirudisha soka la Tanzania enzi zile za FAT

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:08 AM Aug 19 2024
 Rais Wallace Karia.
Picha:Mtandao
Rais Wallace Karia.

LIGI ya Tanzania inashika nafasi ya sita kwenye ubora wa Ligi za Afrika, na kwa sasa ina mvuto mkubwa kwa mashabiki mbalimbali duniani ambao wamekuwa wakiifuatilia.

Haikuja kwa bahati mbaya, bali kuna wadau wa soka walipambana usiku na mchana, chini ya Rais Wallace Karia kuhakikisha mpira wa Tanzania unapiga hatua.

Ligi ya Tanzania imetoka kule ambapo ilikuwa haionyeshwi kwenye televisheni, lakini kwa sasa asilimia 90 ya mechi zote zimekuwa zikionekana.

Ubora wa Ligi ya Tanzania umechangiwa na vitu vingi mno, ikiwamo viongozi wake mara kwa mara kuumiza vichwa na kuangalia wapi kunaweza kuboreshwa ili soka liwe juu.

Kuna wachezaji wengi bora wa kigeni kwa sasa ambao wameruhusiwa kuingia na kuifanya ligi kuwa na ushindani mkubwa, timu za Tanzania kufanya vema katika michezo ya kimataifa na hata wachezaji wa Kitanzania kujifunza kutoka kwao na kuikomaza Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Binafsi hili nalipongeza na naomba viongozi washikilie msimamo huo huo, badala ya kusikiliza maneno ya watu ambao wamekuwa wakionekana kupinga sana idadi ya wachezaji 12 wa kigeni kuwapo katika kila timu.

Nadhani hii ni kwa sababu zao binafsi, labda wengi wao ni mawakala wa wachezaji wa Kitanzania, lakini hawafanyi hivyo kwa manufaa ya maendeleo ya soka la Tanzania na ligi kwa ujumla.

Lakini pamoja na hayo, bado nina wasiwasi kuwa baadhi ya mambo yanavyokwenda ni kama vile yanaanza kuturudisha nyuma enzi ya Chama cha Soka nchini (FAT), wakati kipindi hichi ni cha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Sina maana kuwa nabeza soka la kipindi hicho, la hasha, ila nyakati na kutokuwapo kwa mawasiliano bora na miundombinu ilisababisha vitu viende ndivyo sivyo. Huwezi kuwalaumu kwa sababu huwezi kupishana au kushindana na nyakati.

Nashangaa eti mpaka leo, bado kuna kesi za wachezaji kusaini timu mbili, wakati kwa wenzetu walioendelea huwezi kukuta hilo.

Ni Tanzania pekee ndiyo bado kuna kesi za wachezaji kusaini mara mbili, lakini pia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji haitoi maamuzi, badala yake inataka klabu zilizoshindwana kwenda kuzungumza nje ya kamati hiyo.

Kamati ambayo ina hadhi sawa na ile ya FIFA kwa ngazi ya nchi, inaposhindwa kutoa maamuzi ya kesi za klabu ni ajabu kidogo. Sijawahi kusikia CAS ikirudisha kesi ya wanaopingana, badala yake inatumia sheria na kanuni ilizojiwekea kuamua. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, yenyewe haifanyi hivyo kwa baadhi ya kesi. 

Lakini pia sijawahi kuona FIFA ilimrudisha mchezaji kwenye timu aliyoondoka kama kuna tatizo la kimkataba inamuuliza wapi anataka kucheza huku kesi ikiendelea, na yeyote atakayeonekana amekiuka taratibu anaadhibiwa, bila kuathiri mahusiano na kazi za watu.

Ukishangaa ya Mussa utaona ya Firauni, katika mechi ya Pamba Jiji dhidi ya Prisons tumesikia kuna baadhi ya wachezaji wa Pamba hawakuwa na leseni.

Katika dunia hii ya sasa kweli ligi kama hii ya Tanzania inaanza baadhi ya wachezaji kweli hawana leseni? Siku zote viongozi wa klabu na TFF walikuwa wapi? Nani mzembe kwa hili?

Kocha Goran Copunovic amelalamika sana kuhusu hilo, akadai amepanga kikosi chake, lakini kila akifanya hivyo anaambiwa kuna wachezaji hawaruhusiwi kucheza.

"Kabla ya mchezo kuna watu waliniambia TFF wamesema kuna wachezaji hawana leseni. Nikabaki na wachezaji tisa tu. Nimebadili kikosi mara tano kabla ya mchezo. Hii si sawa. Mambo ya leseni wanaohusika ni viongozi, sijui tatizo ni nini. Nitaondoka leo kama mimi ndio tatizo. Hiki ni kitu gani jamani?" akalalamika kocha huyo.

Pamoja na hayo, inadaiwa viongozi wa Prisons wamekata rufani kuwa Pamba ilichezesha wachezaji ambao hawaruhusiwi.

Jamani katika dunia hii ya leo, bado mambo haya yapo? Karne hii ya 21, kwenye Ligi Kuu ya sita kwa ubora? Nadhani kuna sehemu tumeanza kurudi nyuma enzi zile za FAT. Mbona hatujawahi kuviona huko kwenye ligi za wenzetu? Kama ni viongozi wa klabu, au ndani ya TFF waanze kuangaliana mapema kabla mambo hayajaharibika na kulitia aibu taifa.