Agizo la Makamba kwa waliobomolewa lageuzwa dili

14Jan 2016
Mary Geofrey
Nipashe
Agizo la Makamba kwa waliobomolewa lageuzwa dili

SIKU chache baada ya serikali kuagiza wakazi waliobomolewa nyumba zao katika Bonde la Mkwajuni, jijini Dar es Salaam na kuendelea kubaki kwenye eneo hilo kwa kulala nje waorodheshwe majina yao ili kupatiwa msaada, wakazi wengine waliokuwa wakiishi eneo hilo wamemiminika ili waweze kupata fursa hiyo.

SIKU chache baada ya serikali kuagiza wakazi waliobomolewa nyumba zao katika Bonde la Mkwajuni, jijini Dar es Salaam na kuendelea kubaki kwenye eneo hilo kwa kulala nje waorodheshwe majina yao ili kupatiwa msaada, wakazi wengine waliokuwa wakiishi eneo hilo wamemiminika ili waweze kupata fursa hiyo. Nipashe jana lilifika eneo hilo na kushuhudia vibanda vikiwa vimeongezeka eneo hilo tofauti na ilivyokuwa awali, huku watu wengine wakiwa maeneo hayo bila ya kuwa na vibanda.
Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wakazi wa maeneo hayo, walisema vibanda vimeongezeka ghafla pamoja na idadi ya watu wanaokwenda kushinda eneo hilo ikilinganishwa na kabla ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba, kusema kwamba watu wenye mahitaji maalum watasaidiwa.
“Kabla Waziri Makamba hajafika hapa tulikuwa wachache na tunafahamiana, idadi ilikuwa ikiongezeka usiku wakati wa kulala lakini mchana tulikuwa wachache. Juzi Makamba alivyokuja akasema tuandikishwe majina kwa ajili ya msaada, tangu siku hiyo watu wameongezeka na wameanza kushinda hapa,’’ alisema Maimuna Kassim.
Maimuna ambaye alikuwa akimiliki nyumba ya vyumba vitatu eneo hilo, alisema juzi maofisa wa serikali walifika eneo hilo na kuwahoji sababu za kutoondoka eneo hilo, hali ambayo imewafanya wengine kurudi ili kupata msaada endapo utatolewa.
Baadhi ya wananchi waliokuwa eneo hilo ambao walionekana tofauti na wale wa siku zote kimavazi, walikuwa wakiwauliza waandishi wa habari kama wanaorodhesha majina ili kupata msaada wowote.
Nipashe pia lilishihudia vijana wakiendelea na shughuli za kusomba vifusi vya mchanga na matofali kwa ajili ya kuuza ili kujipatia fedha.
Benson Dianis aliyekuwa mkazi wa eneo hilo mwenye mke na watoto watatu, alisema kwa sasa anazoa kifusi cha wenye nyumba zilizobomolewa ili kujipatia riziki.
“Sina kazi ya kufanya, watoto nimewaombea kwa ndugu maeneo ya Kimara Matosa, hiki kifusi nikizoa napata fedha ya kula na familia yangu,” alisema.
Pia eneo la barabara ya Kawawa matofali yaliyotumika yalikuwa yamepangwa barabarani yakiuzwa kwa Sh. 400 kwa moja na wakazi hao ili kujipatia riziki.
Aidha, magari matatu aina ya Tingatinga, yalionekana yakiendelea na shughuli za kusawazisha eneo hilo kwa ajili ya shughuli nyingine zitakazofanyika, huku yakiacha vibanda vilivyoezekwa eneo hilo.
Kazi ya kusafisha eneo hilo inatarajiwa kukamilika leo, huku kazi ya uwekaji wa alama ya X katika nyumba ambazo zimejengwa mabondeni kwa ajili ya kubolewa ikiendelea leo eneo la Kigogo.

Habari Kubwa