Asimilia 10 kumng'oa Katibu Mkuu Yanga

19Jan 2016
WAANDISHI WETU
Nipashe
Asimilia 10 kumng'oa Katibu Mkuu Yanga
  • *** Tangu atue Jangwani Januari 2015, Tiboroha amedhibiti mianya ya ufujaji wa fedha za klabu hiyo kongwe nchini ...

MINONG'ONO ilianza wakati kikosi cha Yanga kilipokuwa visiwani Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi kwamba Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Jonas Tiboroha, amekalia kuti kavu kwenye nafasi hiyo.

katibu mkuu yanga jonas Tiboroha

Taarifa hizo zimeendelea kuzagaa huku moja ya sababu ya kutaka kung'olewa kwa msomi huyo mwenye Udaktari wa Falsafa (PhD) katika Michezo, ikielezwa ni kitendo chake cha kuziba 'mianya ' ya watu kupiga pesa wakati wa usajili wa wachezaji wa klabu hiyo.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga ambaye aliomba hifadhi ya jina lake kwa vile si msemaji wa klabu hiyo, aliiambia Nipashe jana kuwa wapo baadhi ya wajumbe wa kuteuliwa kwenye kamati mbalimbali ambao wanamwona Tiboroha kama kikwazo kwao kwenye 'upigaji wa pesa' za usajili kupitia utaratibu uliokuwa umezoeleka Jangwani wa 'Ten Percent' (Asilimia 10).
"Hii ilizoeleka na ipo kwenye klabu hizi kubwa za (... anataja moja ya klabu za Ligi Kuu) na Yanga za kutaka kuongeza cha juu kwenye usajili wa wachezaji, ila kwa sasa kwenye klabu yetu watu hao wamekutana na kizingiti ambacho si kingine, bali Katibu (Tiboroha).
"Tiboroha ana msimamo, na msimamo wake huo unaonekana kuwa kikwazo kwa baadhi ya wajumbe, uongozi unaweza ukakataa jambo hili halipo, lakini ukweli ni huo, kuna watu wanataka Tiboroha aondolewe," alisema zaidi mjumbe huyo.
Alipotafutwa na Nipashe kwa simu jana saa 12:15 jioni kuzungumzia suala hilo, Tiboroha alikiri kuwapo kwa changamoto hiyo.
"Ni kweli nimepata taarifa hizo ingawa si rasmi. Kwa sasa siwezi kulizungumzia zaidi suala hilo. Wapo watu wanaona hivyo kuhusu mimi, lakini kiongozi rasmi wa Yanga hakuna aliyenifuata na kunieleza chochote," alisema Tiboroha.