Askofu Mkuu KKKT afunguka

24Jan 2016
Nipashe Jumapili
Askofu Mkuu KKKT afunguka

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Frederick Shoo, amesema kasi ya Rais John Magufuli, ya kutumbua majipu inaridhisha na amemtaka akaze kamba kwani watanzania wako nyuma yake.

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Frederick Shoo

Aidha, Askofu Shoo amewasihi viongozi wenzake wa dini na madhehebu tofauti kuungana kumuombea Rais Magufuli ili kumnusuru na jambo baya kwasababu kazi anayofanya ni ngumu na inahitaji maombi.
Aliyasema hayo jana wakati akifanya mahojiano maalumu na gazeti hili kuhusu siku 80 za Rais Magufuli Ikulu.
Kwa tathmini ya Askofu Shoo, Magufuli ameonyesha uongozi mzuri na ushupavu, na ni kiongozi anayepaswa kuigwa na marais wengine duniani.
Alisema anafurahishwa na kasi ya utendaji kazi ya Rais kwasababu ndani ya muda mfupi ameonyesha umahiri kwa kuokoa mabilioni ya fedha zilizokuwa zikitafunwa na "wezi".
Askofu Shoo alisema kazi ya Rais Magufuli inatia moyo kwa taifa na kanisa kwa ujumla, hivyo alimuasa aendelee na kasi hiyo kuibua ufisadi ambao ulikuwa ukisababisha kupotea kwa mabilioni.
Alisema wakati wa uongozi wa Hayati Mwalimu Julias Nyerere, uchumi ulikuwa imara na nchi ilikuwa ikijiendesha kwa rasilimali zilizoko, lakini baada ya kupita utawala wake mambo yamekuwa tofauti.
Alisema haijawahi kutokea katika historia ya nchi kwa kiongozi mkakamavu kama Magufuli kujitoa kwa maslahi ya taifa kwa kufichua wezi na kuwafukuza kazi kwani kwenye serikali zilizopita hawakuguswa.
“Labda niseme tu inawezekana Mungu amemwonyesha njia mtumishi wake Magufuli, kwa makusudi ili afichue mambo ambayo yakiboreshwa na kusimamiwa yataweza kuibadilisha nchi na kuwa miongoni mwa nchi za kuigwa kupitia ukuaji wa uchumi,” alisema Askofu Shoo.
Alisema anatarajia kutoa tamko lake mwanzoni mwa wiki ijayo kuhusu utendaji kazi wa Magufuli katika hatua za mwanzo za utawala wake, na kuwasihi viongozi wa dini mbalimbali kuungana katika maombi ili kumnusuru na jambo baya dhidi yake.
Alipoingia tu madarakani, Magufuli alisababisha mtikisiko mkubwa ndani ya Mamlaka ya Bandari (TPA) na kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kubaini mianya ya ukwepaji wa kodi hivyo kulazimika kuchukua hatua kali ikiwemo kuwasimamisha kazi vigogo kadhaa wa mamlaka hizo mbili.

WALIOSIMAMISHWA KAZI
Miongoni mwa vigogo ambao walianza kuonja chungu ya serikali ya Rais wa tano ni pamoja na Kamishna Mkuu wa Mamalaka ya Mapato Nchini (TRA), Rashed Badi aliyesimamishwa kazi pamoja na vigogo wengine saba walikamatwa na polisi akiwemo Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa, Tiagi Masamaki, kutokana na kutolewa kwa makontena 329 yaliyotoka bila ushuru.
Katika sakata hilo zaidi ya wafanyakazi 40 wa TRA walishikiliwa na Jeshi la Polisi kuhusina na tuhuma hizo ambazo zimeisababishia serikali hasara ya mabilioni ambapo pia Magufuli alivunja Bodi ya Mamlaka ya Bandari.
Mbali na kuvunja bodi hiyo, pia alitengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Profesa Joseph Msambichaka na kumsimamisha kazi Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Shaaban Mwinjaka kwa kushindwa kusimamia utendaji wa TRL na TPA.
Wengine waliokwisha kumbana na rungu la Rais Magufuli ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, ambaye ilielezwa kuwa Rais hakuridhishwa namna taasisi yake ikitekeleza majukumu na kushindwa kukabiliana na vitendo vya rushwa hususani kwenye upotevu wa mapato ya serikali katika bandari ya Dar es Salaam.
Pia Dk. Magufuli alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Benhadard Tito ili kupisha uchunguzi wa kina kutokana na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi, uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa Reli ya Kati.
Rais Magufuli amevunja rekodi ya ukusanyaji wa mapato kutoka Sh. bilioni 900 hadi trilioni 1.4 mwezi Desemba 2015.

Habari Kubwa