‘Vikundi rejesheni mikopo h/shauri’

29May 2020
Na Mwandishi Wetu
SIMANJIRO
Nipashe
‘Vikundi rejesheni mikopo h/shauri’

VIKUNDI vilivyopata mikopo kutoka Halmashauri na taasisi nyingine za kifedha vimeshauriwa kujenga uaminifu katika marejesho ili na wengine waweze kunufaika na fedha hizo.

Hayo yamebainika jana katika hafla ya kukabidhi hundi za mikopo awamu ya nne kwa baadhi ya vikundi vya Halmashauri Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.

Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati, Nsolo Mlozi, alisema benki hiyo ilikabidhiwa jukumu la kutoa elimu kwa vikundi pamoja na kuwafungulia akaunti, jambo ambalo wamelifanya kwa makini na vikundi vyote walifanikiwa kupata fursa hiyo.

“Mbali ya elimu ya fedha, NMB tunashirikiana na halmashauri hii kwa kutoa misaada mingine kwenye jamii hasa sekta ya elimu, afya na kwenye majanga mbalimbali,” alisema Mlozi.

Alisema benki hiyo imeendelea kutenga asilimia moja ya faida yake kila mwaka kurudisha kwenye jamii ikiwa ni juhudi za kuunga mkono Serikali ya Rais John Magufuli.

Mkurungenzi wa Halmashauri ya Simanjiro, Yefred Myenzi, alisema jumla ya fedha zilizokopeshwa kwenye vikundi ni zaidi ya Sh. milioni 244.6 kutoka mapato yake ya ndani.

“Walionufaika ni  wananchi 1,412 ndani ya halmashauri hii, wakiwamo wanawake 1,074 vijana 372 na walemavu 40. Halmashauri hii  haidaiwi, imeshalipa madeni yote yakiwamo mikopo benki na makandarasi waliofanyakazi ya eneo hili.”

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mhandisi Zacharia Chaula, alivitaka vikundi vilivyopata fursa ya kupewa mikopo kutoka mfuko wa halmashauri kuhakikisha wanarejesha kwa wakati ili wengine waweze kufaidika na mikopo hiyo.

Alisema: “lengo la serikali kutoa mikopo hiyo kupitia halmashauri ni kuwajengea uwezo wa kiuchumi makundi maalumu yaliyoorodheshwa kisheria katika mikopo hiyo.”

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Simanjiro, Sendeu Laizer, alimshukuru Mkurungenzi wa Halmashauri hiyo na baraza la madiwani kwa kuhakikisha anatenga fedha hizo kwa kuwahudumia makundi maalumu.

Laizer aliishukuru benki ya NMB kwa kuwajengea makundi hayo uwezo wa elimu ya kifedha.

Habari Kubwa